Benjamin Masese -Ilemela
SIKU chache baada ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kupokea kivuko cha MV. Ilemela na kuanza kusafirisha abiria kutoka Kayenze hadi Kisiwa cha Bezi mkoani Mwanza, baadhi ya wakazi wa visiwa vingine wameomba Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dk. Angeline Mabula kuishauri serikali ili iweze kuweka ratiba ya usafiri huo na ifike katika visiwa vingine.
Maombi hayo ya wananchi yalitolewa jana wakati wakizungumza na waandishi baada ya kivuko hicho kuanza kazi ya kuwasafirisha abiria kutoka Kayenze hadi Kisiwa cha Bezi kwa Sh 1,000 huku wale wanaoishi Kisiwa cha Tefu, wakiomba kusaidiwa usafiri huo.
Mkazi wa Tefu, Salome Isack alisema anaomba usafiri wa kivuko hicho cha MV Ilemela kiweze kufika hadi katika kisiwa chao kwani wamekuwa wakikabiliawa na changamoto ya usafiri.
Naye Afuadi Issa mkazi wa Kayenze alipongeza uwepo wa Kivuko cha MV Ilemela na kusema kwamba usafiri huo utakuwa wa kudumu na utawasaidia kusafiri kwa usalama zaidi tofauti na ilivyokuwa kwa usafiri wa mitubwi na boti.
Kutokana na kilio hichocha wananchi, MTANZANIA ilimtafuta Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Japhet Masele ili kutoa ufafanuzi kuhusu maombi hayo ya wananchi, alisema kivuko cha MV Ilemela hakitaweza kwenda Kisiwa cha Tefu kwa sababu kuna mawe makubwa ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa kivuko na abiria.
Alisema baada ya Kivuko cha MV Ilemela kuanza kazi ya kubeba abiria wa Bezi na Kayenze, wamekubaliana na wamiliki wa boti na mitumbwi iliyokuwa ikifanya kazi Kayenze na Bezi itaelekezwa Tefu na maeneo mengine.