Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Msanii anayefanya vizuri katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini Nigeria, Idahams amefanikiwa kuvuka kikwazo cha Covid-19 kwa kuachia albamu fupi (Extended Play- EP) iitwayo ‘Man On Fire’ yenye jumla ya nyimbo saba zilizobeba ujumbe wa kuwafariji na kuwapa moyo watu katika kipindi hiki cha janga hilo.
Nyimbo zilizomo ndani ya albamu hiyo ni mchanganyiko wa mahadhi ya Afro Pop, Rap na aina nyinginezo za Afrika huku akiwashirikisha wasanii Falz, Shima, Peruzzi na Seyi Shay.
Katika albamu hiyo, Idahams anaendeleza moto aliouwasha mwaka 2020 kwa kutoa nyimbo kali zaidi ya zile zilizopo kwenye albamu yake iliyopita kama Belle, God When na No One Else alioutoa mwaka 2018 ambao ulisababisha asainiwe na lebo kubwa za Universal Music na Grafton Records.
Akizungumzia mafanikio ya kukamilika kwa EP hiyo, Idahams amesema:
“Niliamua kuongeza nyimbo tatu kwenye EP yangu ya 2021 ya Deluxe kwa sababu nilihisi kuwa mwaka huu mashabiki wangu wanapaswa kuwa na zaidi kutoka kwa toleo la asili la EP ya ‘Man On Fire’ ya 2020.
“Jibu ni kwamba imekuwa kubwa na ninaweza kuona mashabiki wakiwa wabunifu wa nyimbo, najivunia sana mafanikio haya kwa kweli,” amesema.
Aidha, amesema katika mipango yake ya mwaka huu ni pamoja na kufanya kazi na msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz ambaye amesema kwake, ndiye msanii anayeona ana uwezo mkubwa zaidi.