25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

OSHA yazindua mpango wa kusajili na kukagua maeneo ya wajasiriamali wadogo

Na Mwandishi Wetu

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umezindua mpango maalum wa kuwasajili na kuwahudumia wajasiriamali wadogo kupitia ukaguzi wa sehemu za kazi, kuwapa mafunzo na ushauri wa kitaalam kuhusiana na masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

Baadhi ya washiriki wa maonesho ya wajasiriamali na wawekezaji wakifuatilia mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA wakati wa maonesho hayo.

Mpango huo umezinduliwa rasmi katika maonesho ya wajasiriamali na wawekezaji yaliyohitimishwa mwishoni mwa wiki katika kituo cha uwezeshaji wanachi kiuchumi mjini Kahama mkoani Shinyanga.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mpango huo mahsusi umeandaliwa na Taasisi yake baada ya kuendesha programu ya mafunzo kwa wajasiriamali wadogo kwa miaka mitano na kubainisha ombwe katika usimamizi wa usalama na afya miongoni mwa kundi hilo muhimu.

“Tumekuwa na programu ya mafunzo kwa wajasiriamali wadogo kwa zaidi ya miaka mitano lakini hivi karibuni tulifanya tathmini ya mpango husika na tukabaini kwamba tunahitaji kuwa na utaratibu mzuri na rahisi zaidi kwa ajili ya kundi la wajasiriamali wadogo kuweza kukidhi viwango vya usalama na afya mahali pa kazi. Hivyo, tukaone tutengeneza mfumo wa kieletroniki utakaotuwezesha kuwasajili na kisha kuwafikia katika maeneo yao ili kuwaelimisha pamoja na kushauri namna bora ya kuboresha mazingira yao ya kazi,” alisema Mwenda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa GS1 Tanzania ambao ndio waratibu wa maonesho hayo kwa kushirikiana na kituo cha uwezashaji wanachi kiuchumi Kahama, Fatma Kange, amesema Taasisi yake inashirikiana na OSHA katika kuwawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao pamoja na kuwapa miongozo ya kuboresha mazingira yao ya kazi.

Afisa Usajili wa OSHA, Glory Bonventure, akiwaongoza wajasiriamali wadogo kusajili maeneo yao ya kazi kupitia mtandao wa WIMS (Workplace Information Management System) wakati wa maonesho ya wajasiriamali na wawekezaji Kahama.

“Miaka kumi ijayo tunaanza kazi na OSHA na ndio maana unaona katika maonesho haya OSHA amekuwa mdhamini muhimu sana kwa lengo la kuja kuelimisha wajasiriamali wetu ili wafanye uzalishaji kwa kuzingatia afya na usalama wao. Kama tunavyofahamu OSHA wana wajibu mkubwa wa kulinda rasilimali uhai na afya ya kila mtanzania. Hivyo, tunataka wazalishaji wetu watambue nafasi ya afya katika shughuli zao za kila siku” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa GS1 Tanzania.

Baadhi ya wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo na kupata fursa ya kusajili maeneo yao ya kazi pamoja na kupatiwa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi wameeleza jinsi walivyoupokea mpango huo pamoja na mafunzo waliyoyapata.

“Kupitia maonesho haya kuna mafunzo mbali mbali na miongoni mwa mafunzo hayo ni mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA. Kwakweli mafunzo haya nimeyafurahia sana kwasababu yametupatia nyenzo za kujikinga zaidi katika kazi zetu ili kujiepusha na madhara tunayoweza kuyapata tukiwa kazini au baada ya kustaafu,” alisema Amina Madeleka, Mjasiriamali aliyeshiriki maonesho na mafunzo yaliyotolewa na OSHA.

OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambayo husimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Majukumu yake ya msingi ni pamoja na kusajili maeneo ya kazi, kufanya kaguzi za usalama na afya mahali pa kazi, kuchunguza afya za wafanyakazi, kufanya tafiti na kuishauri serikali kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,226FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles