Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wakazi wa Mtaa wa Kipunguni wanaotakiwa kuhama kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wameiomba serikali kutekeleza ahadi waliyoitoa ya kuwalipa fidia Agosti mwaka huu.
Wakazi hao wamesema wamesubiri fidia hizo kwa muda mrefu tangu walipoanza kufanyiwa tathmini mwaka 1997 hali inayosababisha kushindwa kuendeleza makazi yao na kuishi maisha ya taabu.
Wakizungumza Julai 18,2024 wakati wa mkutano wa hadhara uliohitishwa na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, na kufanyika katika Mtaa wa Mogo Kata ya Kipawa, wamesema wamekuwa wakiahidiwa kulipwa fidia bila mafanikio na kuiomba serikali imalizane nao waweze kuhama.
“Tangu mwaka jana tuliaminishwa kulipwa na tumeahidiwa tena kwenye kikao cha Mwenezi (Amos Makala), tunaomba hili zoezi likamilike wananchi wa Kipunguni tumechoka,” amesema mkazi wa Kipunguni, Fausta Richard.
Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, amesema kuna michakato inayoendelea ambayo inaashiria serikali iko tayari kuwalipa wakazi hao na kuwaomba waendelee kuwa wavumilivu na kuiamini serikali.
“Tumefanya mambo mengi ambayo yanaashiria serikali iko tayari kulipa, naendelea kuwahakikishia fedha zenu mtalipwa na mimi niko na ninyi mpaka mpate haki yenu,” amesema Bonnah.
Julai 8,2024 Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, aliwahakikishia wakazi hao kuwa watalipwa fidia hizo Agosti mwaka huu.
Mwigulu alitoa ahadi hiyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Shule ya Sekondari Liwiti, baada ya kutakiwa na Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, Amos Makala, kutoa majibu ya suala hilo.
“Jambo la Kipunguni nalifahamu vizuri na nilishafika Kipunguni kulielezea, tulitoa kauli ya serikali. Mheshimiwa mbunge (Bonnah) amelifuatilia mara nyingi, amelifikisha kwenye vikao kadhaa vya viongozi wakuu na vyote kauli ya serikali ilikuwa ni kuanza kulipa fidia mara moja.
“Tumechelewa tofauti na tulivyoahidi kwa sababu ya dharura iliyojitokeza katika mwaka wa fedha uliopita, tulikuwa na dharura kubwa ambazo zilikuwa zinalikata taifa vipande vipande yakiwemo mafuriko ya Mikoa ya Kusini.
“Nilikutana na ujumbe wa viongozi 10 kutoka Kipunguni niliwapa majibu kwamba baada ya kuanza mwaka mpya wa fedha tunatarajia mwezi mmoja utatumika kuweka sawa mifumo mipya ya malipo…tunatarajia kuanzia mwezi wa nane tuanze kulipa wananchi wa Kipunguni,” alisema Dk. Nchemba.