33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kipigo cha Stars chazua tafrani

*Wabunge waliokuwa Misri, warejea na kumshukia Amunike

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

WABUNGE waliokuwa Misri kuishangilia Taifa Stars, wamerejea jana nchini, huku wakitofautiana kuhusiana na kipigo cha timu hiyo ya Taifa walichokipata kutoka kwa Senegal.

Katika mchezo huo wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon2019), Stars ilianza vibaya kwa kufungwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa June 30, jijini Cairo.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, wapo Wabunge waliokiri Stars kuzidiwa uwezo na Senegal, huku wengine wakimtupia lawama kocha wake kikosi hicho, Emmanuel Amunike.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema kuna kila sababu ya kuendelea kuwasapoti wachezaji wa Stars kwani wamecheza na timu ambayo inashika namba moja kwenye viwango vya soka Afrika.

“Senegal ina wachezaji wengi wazuri ambao wanacheza nje, hivyo kwa matokeo yale, inatubidi tuendelee kuwasapoti wachezaji wetu kwani hata baada ya mechi kwisha, walituahidi watafanya vizuri kwa mechi zilizobaki,” alisema.

Alisema pamoja na yote, michuano hiyo imetoa funzo kwani kuna haja ya kuwekeza katika michezo, hasa soka, kutoa mafunzo kwa makocha, waamuzi na kuondoa rushwa kwenye michezo.

Alisema wao kama bunge wataangalia katika bajeti ijayo kuweza kutoa kiasi cha fedha kwa ajili ya Taifa Stars.

Naye Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, alisema kuna haja ya kuanzishwa kwa kituo cha soka la vijana (academy).

“Ni vizuri mpira wa miguu ukaanzia kwenye shule za msingi, sekondari, wachezaji wakapatiwa vifaa vya michezo, hii itatusaidia kufanya vizuri baadaye,” alisema.

Wakati hao wakisema hayo, Mbunge wa Kuteuliwa, Abdallah Bulembo, alilishukia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Amunike kutokana na kile alichodai upangaji mbovu wa kikosi kilichoivaa Senegal.

“Timu iliyopangwa, sehemu ya viungo ilionekana kuzidiwa, kocha alitakiwa kuangalia mapema ni wapi tulizidiwa ili aweze kufanya marekebisho mapema,” alisema.

Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia, alisema: “Kocha wa timu ya Taifa ana rekodi gani hadi apewe timu? Nilikaa na Rais wa Chama cha Soka Nigeria, alisema kama angepata nafasi ya kutupa ushauri, angetuambia yule sio kocha, lakini pamoja na yote, Tanzania tunatakiwa tuwekeze kwenye timu ya Taifa.”

Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta, alisema vijana wapo vitani, lugha ambayo inatakiwa itumike ni kuwapa moyo.

“Mheshiwa Spika wa Bunge ameongea vizuri, tunaiomba serikali kupitia michango yao, kuwe na na bajeti itakayoenda kwenye timu ya Taifa,” alisema.

Mbunge wa Kuteuliwa, Mama Salma Kikwete, alisema kabla ya kuhudhuria mechi, walikutana na wachezaji, kitendo ambacho kiliwapa hamasa kubwa.

“Maoni yote yaliyotolewa ni vema yakafanyiwa kazi kwani kwenye uwekezaji wa mpira, inatakiwa uanze chini, lakini pia tunawapongeza watanzania waliojitokeza kwenda kuisapoti timu yetu,” alisema.

Mbunge wa Busega, mkoani Simiyu, Raphael Chegeni, alisema: “Misri ina viwanja wa mpira kama wa Taifa 12, hivyo wao wamewekeza sana na wameendelea na sisi tunatakiwa tuendelee na kasi hii tufanya vizuri zaidi.”

Stars imepangwa Kundi C la michuano hiyo, ikiwa pamoja na Senegal, Kenya na Algeria ambapo mechi ijayo ya Tanzania itakuwa dhidi ya Harambee Stars, keshokutwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles