Addis Ababa, Ethiopia
Kiongozi wa Jeshi la nchini Ethiopia, Jenerali Seare Monnen, ameuawa kwa kupigwa risasi na mlinzi wake mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Waziri Mkuu Abiy Ahmed alisema mkuu huyo na ofisa mwingine walipoteza maisha katika mji wa Amhara wakijaribu kuzuia mapinduzi dhidi ya utawala nchini humo.
Mjini Ahmara kwenyewe, gavana wa mji huo Ambachew Mekonnen aliuawa pamoja na mshauri wake.
Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yameikumba Amhara na miji mingine miaka ya hivi karibuni.
Waziri mkuu alikwenda kwenye kituo cha Televisheni akiwa na mavazi ya kijeshi kukemea mashambulizi hayo.
Tangu uchaguzi wa mwaka jana, Abiy amekua akipambana kumaliza mvutano wa kisiasa kwa kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, kuondoa makatazo dhidi ya vyama vya kisiasa na kuwashtaki maofisa wanaoshutumiwa kukiuka haki za binaadamu.
Marekani imewatahadharisha wafanyakazi wake mjini Addis Ababa kutotoka nje, ikisema ina taarifa kuhusu mashambulizi ya risasi siku ya Jumamosi.
Jenerali Seare aliuawa sambamba na Jenerali mwingine, Gezai Abera, na mlinzi ambaye sasa anashikiliwa, ofisi ya habari ya waziri mkuu imeeleza.
Mjini Amhara gavana aliuawa sambamba na mshauri wake mkuu Ezez Wasie, huku mwanasheria wa mji huo akijeruhiwa. Lake Ayalew ameteuliwa kuwa gavana mpya wa mji huo.
Ofisi ya waziri mkuu imemshutumu mkuu wa usalama wa mji wa Amhara, Asaminew Tsige, kwa kupanga mapinduzi. Haijajulikana kama amekamatwa.
“Jaribio la mapinduzi mjini Amhara ni kinyume cha katiba na chenye nia ya kuharibu amani ya eneo hilo,” ofisi hiyo ilieleza katika taarifa yake na kuongeza:
“Tukio hili linapaswa kukemewa na raia wote wa Ethiopia na Serikali ina uwezo wa kupambana na kundi hili lenye silaha.”
Wakazi wa makao makuu ya mji wa Amhara, Bahir Dar, waliripoti kusikia milio mikubwa ya risasi.
Hiki ni kipindi kigumu kwa Ethiopia na waziri mkuu Abiy, ambaye anakabiliwa na mizozo ya wenyewe kwa wenyewe.
Kiongozi wa kijeshi, Seare Mekonnen alitumikia nafasi hiyo kwa mwaka mmoja baada ya kuteuliwa na waziri Abiy, ambaye alifanya mabadiliko kwenye idara ya usalama alipoingia madarakani mwezi Aprili mwaka jana.
Ni wazi kuwa waziri mkuu anakabiliwa na upinzani kutoka ndani ya jeshi ambao wanapinga mtindo wake wa utawala.
Kuuawa kwa gavana wa Amhara ambaye alikuwa mshirika muhimu kwenye mji huo pia ni pigo kubwa kwa waziri mkuu Abiy, mji ambao wenyewe unakabiliwa na changamoto za kiusalama na vurugu za baadhi ya makundi.
Uchaguzi wa kwanza tangu bwana Abiy aingie madarakani unapaswa kufanyika mwakani lakini ni vigumu kuona namna gani hili jambo linafanikiwa kwenye nchi ambayo usalama wake ni mdogo. Hali ya kisiasa ni mbaya sana.
Ardhi ya jamii ya Amhara ni mji wa pili wenye watu wengi na umeipa Ethiopia lugha ya taifa hilo, Amharic.
Mapigano kati ya jamii ya Amhara na Gumuz iligharimu maisha ya watu mwezi uliopita mjini Amhara na mji jirani wa Benishangul Gumuz.
Mapigano kati ya jamii hizo yalisababishwa na migogoro ya ardhi, takribani watu milioni tatu walikimbia makazi yao.
Suala jingine ambalo waziri mkuu anapaswa kukabiliana nalo ni kutokuwepo kwa hali ya utulivu ndani ya jeshi.