30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kiongozi CNDD-FDD asakwa Burundi

Hussein Radjabu (burundi beat) copieMwandishi Wetu na Mashirika ya Habari
SERIKALI ya Burundi imetangaza msako dhidi ya mwenyekiti wa zamani wa chama tawala cha CNDD-FDD nchini Burundi, Hussein Rajabu, kwa kutoweka jela pamoja na mkuu wa gereza la Mpimba.
Msemaji wa Serikali, Liboire Bakundukize, alisema jana kuwa msako dhidi ya watu hao umeanza.
“Serikali inamsaka Hussein na wale wote waliomsaidia kutoroka gerezani waweze kufunguliwa mashtaka mara moja,” alisema Bakundukize katika taarifa yake.
Pamoja na kutolewa taarifa hiyo ya Serikali, Mwanasheria Hussein ametangaza kufungua mashtaka dhidi ya Serikali ya Burundi.
Mwanasheria huyo, Prosper Niyoyankana a alisema mebaini kwamba mteja wake alikua akifanyiwa madhila na vitisho vya kuuawa alipokua jela.
Alisema anahisi Rajabu huenda ametekwa nyara au ameuawa.
Rajabu alitoweka jela usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii, ambako alikuwa akizuiliwa tangu mwaka 2007.
Juzi, msemaji wa polisi, Liboire Bakundukize, alithibitisha kwamba Hussein Rajabu alitoroka jela akiwa na wafungwa wengine watatu pamoja na askari magereza wanne ambao waliondoka na vifaa vya jeshi zikiwamo silaha na redio ya mawasiliano ya jeshi.
Hata kiongozi wa jela kuu la Mpimba mjini Bujumbura, ambako Rajabu amekuwa akizuiliwa amethibitisha taarifa ya kutoroka kwa kiongozi huyo wa zamani wa chama tawala aliyefarakana na Rais Pierre Nkurunziza.
Baada ya kuondolewa uenyekiti wa chama hicho Februari 2007, miezi miwili baadaye, Rajabu alikamatwa kwa tuhuma za kula njama za kuendesha uasi wa jeshi na kumtukana Rais Nkurunziza kwa kumwita ‘chupa tupu’.
Mwaka mmoja baadaye, Aprili 2008, Rajabu alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 13 jela na wadadisi wa mambo wanasema iwapo kweli Rajabu ametoroka litakuwa pigo kubwa kwa utawala wa Rais Nkurunziza.
Hata hivyo, wafuasi wengi wa kinara huyo wa zamani wa chama hicho tawala wanahisi huenda ameondolewa jela na kwenda kuuawa.
Mwanasheria wake, Prosper Niyoyankana, ameiomba Serikali ya Burundi kufanya kila linalowezekana ifahamike mteja wake amepelekwa wapi akihisi huenda ameuawa.
Hayo yanatokea wakati kukiwa na ripoti ya mpasuko ndani ya chama tawala, baada ya baadhi ya wafuasi vigogo wa chama hicho kutoa misimamo tofauti kuhusu uamuzi wa Rais Nkurunziza kutaka kugombea urais kwa muhula wa tatu kinyume na katiba.
Ingawa Rais Nkurunziza anasisitiza kuwa muhula wake wa kwanza madarakani alichaguliwa na Bunge na hivyo haupaswi kuhesabiwa kwa mujibu wa Katiba, anakabiliwa na upinzani mkubwa ndani na nje ya chama chake.
Vyama vya upinzani, mashirika ya raia na Kanisa la Katoliki nchini Burundi vinapinga hatua yake hiyo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita serikali ya Burundi iliandaa maandamano ya amani ambayo yaliitikiwa na halaiki ya watu, wengi wao wakiwa wanafunzi na wafanyakazi wa serikali.
Upinzani ulidai maandamano hayo yaliandaliwa na chama tawala kuonyesha kuwa kina wafuasi wengi.
Baadhi ya mashirika ya raia yalikosoa maneno yaliyotumiwa na waandamanaji, wakisema ni kama vitisho kwa baadhi ya viongozi wa mashirika hayo ya raia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles