Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Unapoingia katika karakana ya ufundi wa uungaji vyuma Chuo cha Ufundi Stadi Veta, Dar es Salaam, kama hutaangalia umri wa unaowakuta hapo ni vigumu kujua yupi ni mwanafunzi na yupi ni mwalimu. Hii inatokana na utani na ucheshi unaotawala hata wakati wa mafunzo kati ya mwalimu wao na wanafunzi wenye ulemavu wa viungo na wale wa akili.
Kitengo hicho kinaendeshwa na Mwalimu, Kintu Kilanga (58) ambaye anasema ili kuwafanya wanafunzi hao wenye ulemavu wa akili na wale wa viungo waweze kujifunza kwa kwa bidii ni muhimu kuwaweka karibu wayafurahie mafunzo yao na kujifunza kwa kujiamini.
“Paulo hebu mtembeze kidogo…unashangaa nini au nikupige konzi,” hivyo ndivyo alivyosema Mwalimu Kintu Kilanga wakati akimwambia mwanafunzi wake Paulo Ngunyari (31) mwenye ulemavu wa viungo ili kunionyesha sehemu mbalimbali za karakana hiyo.
Paulo alipokuwa akinitambulisha kwa wanafunzi wenzake aliwataja kwa majina yao halisi pamoja na majina yao maarufu akisema baadhi yao hupewa majina hayo na Mwalimu Kilanga kutokana na jinsi anavyowaona lakini yeye (Paulo) alijipa mwenyewe jina la ‘Mnyama’.
“Mimi niliamua tu kujiita mnyama lakini anapokuja mwenzetu hapa tunajaribu kumtoa unyonge unakuta anakuja mpole kabisa mtu mwingine tunaweza tukamuita mbabe lakini ukiamuangalia yeye ndiyo anaonewa lakini kumtoa unyonge tunamuita jina linalomwongezea sifa fulani ili apate kujiamini,” anasema.
Ni wanafunzi wacheshi na kila niliyemuona wakati natembezwa katika karakara hiyo alikuwa akiwajibika kwenye mashine mbalimbali huku wakimwona Kilanga siyo tu kama Mwalimu bali kama baba na rafiki yao wa karibu.
JINSI WANAVYOJIFUNZA
Mwalimu Kilanga anasema kazi ya ualimu ameifanya kwa miaka 41 lakini kufundisha wanafunzi wenye ulemavu huu ni mwaka wa 12.
“Mimi mafunzo niliyopata ni ya ualimu wa kawaida ila mafunzo zaidi hawa unaowaona (wanafunzi wenye ulemavu) ndiyo wanaonifundisha jinsi ya kuwafundisha wao. Kwa sababu mimi nakuwa rafiki yao halafu nafanya nao kazi pamoja kwahiyo mle ndiyo naanza kuona mapungufu na kuyatafutia tiba,” anasema Mwalimu Kilanga.
Anasema ili kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu wa akili kazi za ufundi ni muhimu kujifunza kutoka kwa kila mwanafunzi jinsi ya kumsaidia aweze kupata ujuzi unaotarajiwa. Na hii anasema unaenda hatua baada ya hatua.
Kwa mujibu wa Mwalimu Kilanga wanafunzi kwa wasio na ulemavu wa akili husoma kozi hiyo kwa miaka miwili lakini wanafunzi wenye ulemavu wa akili hawana muda rasmi kwa sababu wanatofautiana kuelewa kulingana na kiwango cha ulemavu walionao.
Anasema mara ya kwanza wanafunzi hao wakitengeneza vitu huvipeleka nyumbani kwenda kuwaonyesha wazazi na wanajamii wengine ili kubadili mtizamo hasi uliojengeka dhidi ya watu wenye ulemavu kwa kudhani kuwa hawawezi chochote.
“Mtihani wa kwanza ni lazima atengeneze jiko na likipelekwa nyumbani familia inaweza kushangaa hili jiko katengeneza Kimaro (mwanafunzi wake) kwahiyo nyumbani inakuwa ni heshima na kama walikuwa wanamuona hawezi watabadilisha mtazamo,” anasema.
WANAVYOFANYIWA USAILI
Tofauti na ufundishaji wa wanafunzi wengine, kwa wanafunzi wenye ulemavu Mwalimu Kilanga anasema anatumia akili zaidi kwa sababu kila siku inabidi awe anafanya ubunifu wa kutatua matatizo anayokutana nayo katika ufundishaji.
“Ndiyo maana unaona mashine hizi (huku akionyesha mashine) niligundua baada ya kuona mapungufu nikatafuta suluhisho, yaani hawa wanakuwa huru kunionyesha mapungufu yao na mimi najitahidi kutengeneza urafiki matokeo yake wao wananifundisha mimi jinsi ya kufundisha,” anasema.
Mwalimu Kilanga amebuni mashine maalumu kwa ajili ya kuwafanyia usaili wanafunzi wenye ulemavu wa akili pindi wanapotaka kujiunga na chuo hicho.
Anasema baadhi ya watoto wenye ulemavu wa akili hawawezi kuongea wala kuandika hivyo hufanyiwa usaili kwa vitendo ambavyo wamevigawa katika kanuni kuu mbili za ufundishaji. Kanuni ya kwanza kadiri mtoto anavyofanya ndivyo anavyojua na kanuni ya pili inatumia hisia.
“Kuna mtu mmoja bahati mbaya leo (siku ya mahojiano haya) sikuja na nyaraka, tulimpa afanye usaili akawa anachorachora tu, unaweza kumrudisha ukadhani hafai kumbe anafaa…hawa wote unaowaona (yaani wanafunzi wake) wamepita hapa,” anasema Mwalimu Kilanga huku akionyesha mashine ya usaili.
Akifafanua jinsi usaili unavyofanyika anasema mtoto husika hujaribiwa kwa namna mbili ambapo kwanza hutakiwa kugusa sehemu zinazotoa sauti katika mashine hiyo kisha hutakiwa kufuatisha mchoro mwingine kama ulivyo ambao nao hutoa sauti.
“Yeye anapochomeka kwenye mashine sisi tunajua kwa sababu anagusa sehemu inayotoa sauti kama king’ora, lakini sehemu nyingine haina kifaa kinachotoa sauti kwahiyo mimi namuangalia tu utamkuta mwingine anang’ang’ania unajua huyu kidogo namna gani.
“Lakini sehemu nyingine nimepunguza nafasi, sehemu nyingine nimeongeza ndivyo ninavyofanya. Halafu tunataka achore kwa kufuatisha mchoro huu (wenye alama ya S ambao unapofuatishwa pia unatoa mlio wa sauti), hatumfundishi atumie kasi gani au akandamize kwahiyo tunamuangalia anafanya makosa mangapi, na ana kasi gani.
“Hili ni eneo lingine tunataka achore mchoro kwa kasi mbili tofauti, anapochora kwa kufuata mlio tunaanza kumuona kihisia yuko vizuri kwahiyo tunamchukua tunamwambia mzazi mletee buti, ‘overall’ aanze mafunzo,” anasema Mwalimu Kilanga.
Mwalimu Kilanga anasema zamani walikuwa wanatumia vibao lakini hivi sasa wameboresha kwa kubuni mashine hiyo na kwamba mashine hizo ziko tatu.
“Wengi wao hawawezi kuongea vizuri, kama huyu (Mohamed Mussa) utampimaje, nitamuingiza kwenye mashine ya usaili. Pale kwa dakika tano tu naweza nikamgundua kama anaelewa haraka au taratibu.…Hatumpi sijui mbili mara mbili…hakuna hiyo, sisi tunampeleka pale halafu tunampima uwezo wa yeye kujifunza ujuzi na karibu wote wanaofaulu,” anasema.
Licha ya mashine hiyo Mwalimu Kilanga pia kwa kushirikiana na wanafunzi wake amebuni zana saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu wa viungo ambao hawawezi kushika baadhi ya vitu kwa mkono.
“Hawawezi kukata kwa mikono ndiyo maana tumebuni msumeno ambao wakitaka kukata mbao wanazungusha mashine inakata, kwahiyo akija mwingine mwenye ulemavu labda wa miguu tutaangalia miguu hiyo tutaisaidia vipi kwa sababu hatutaki asote chini. Tunataka asimame atoboe kama tunavyotoboa sisi akae juu. Kwahiyo itabidi atengenezewe kiti kimfikishe juu halafu aweze kurudi chini na aweze kutembea nacho kwenye karakana,” anasema.
MAFANIKIO
Mwalimu Kilanga anasema anaona fahari kufundisha watu wenye ulemavu kwa sababu kila siku amekuwa akijifunza vitu vipya kupitia wao na baadhi ya wanafunzi wake wamejiajiri na wengine wanajitegemea.
“Wapo walioajiriwa lakini wengine katika kundi hili wameshapanga wanajitegemea hayo ni mafanikio tayari. Mr Bin (Mohamed Seleman) huyu tayari anajitegemea, huyu naye anaishi mwenyewe (Mohamed Mussa).
“Mimi hapa siwatoi hawa kwa sababu ninawatengeneza wawe walimu kwahiyo nina miaka nao minne, wengine mitano, yule (Paulo Mweta) minne, hapa tayari ni walimu wasaidizi kwangu.
“Mr Bin (Mohamed Seleman) ana miaka saba tayari kashakuwa fundi hawezi kusema lakini anasikia, huyu ni mmojawapo ninaowaandaa kuwa walimu, ukinikimbia wewe nakuendea kwa babu,” anasema Mwalimu Kilanga huku mwanafunzi wake akitabasamu na kutikisa kichwa.
CHANGAMOTO
Mwalimu Kilanga anasema; “Changamoto ninazozipata kwanza lazima muda mwingi niwepo hasa kwa wale wenye ulemavu wa akili kwa sababu sitaki wakazusha kitu halafu akaja mtu mwingine kuamua ile kesi, atatoa tafsiri tofauti inaweza ikahatarisha hata uwepo wao…wataanza kusema watoto hawa hawafai, watoto hawa hatari sana lakini mimi naweza nikaitatua ile kesi kwa misingi ya kwamba mapungufu yao ndiyo yamenifundisha mimi jinsi ya kuwafundisha.
Changamoto nyingine anasema ni uhaba wa walimu kwa sababu walimu wengine huona ni kazi kubwa kuwafundisha watu wenye ulemavu wa akili.
“Ukiwa unafuata pesa zaidi malipo hayawezi kukulipa mimi nalipwa mshahara wangu wa kawaida tu lakini nafarijika kuwafundisha,” anasema.
WANAFUNZI WANAVYOMZUNGUMZIA
Akizungumza huku akisaidiwa na mwanafunzi mwenzake Paulo Mweta kutafsiri maswali ya mwandishi wa makala haya, Mohamed Seleman (28) mwenye ulemavu wa akili anasema Kilanga ni zaidi ya mwalimu.
“Huyu ni baba yetu nilikuja hapa nikiwa sijui kitu chochote lakini hili ‘katapila’ (anamnyooshea kidole mwalimu wake) achana nalo, ukija hapa lazima utajua kila kitu. Namimi nitakukimbia ubaki peke yako hapa,” anasema Seleman huku akimtania mwalimu wake.
Naye Mohamed Mussa mwenye ulemavu wa viungo anasema “Kama si kuja Veta sijui maisha yangu yangekuwaje, Mwalimu Kilanga amenisaidia sana mpaka sasa naweza kujitegemea mwenyewe.
Kwa upande wake Paulo Ngunyari anasema Mwalimu Kilanga amejitoa kuwasaadia watu wenye ulemavu na yeye anamuita profesa kwa sababu kutokana na kazi kubwa anayoifanya.
“Humu ndani wote tunamuita Profesa Kintu sababu hapa si mchezo, mtu mwingine anakuja hajui kitu hivyo ni mtu wa kipekee sana,” anasema Ngunyari.
Naye Dauson Kanyawawa (33) ambaye pia ni tunda la Mwalimu Kilanga anasema alihitimu chuoni hapo mwaka 2010 na baada ya kufanya kazi kadhaa mtaani aliamua kurudi chuoni hapo kujitolea kufundisha.
“Nimejitolea kufundisha kwa sababu Kintu ni mwalimu wangu kanifundisha, nilipomaliza nilikwenda mtaani nikapambana katika makampuni mengine mambo hayakwenda vizuri nikarudi tena hapa,” anasema Kanyawawa.
Anasema kwa kiasi kikubwa wanatumia utani kuwafundisha watoto hao ambao unasaidia kuondoa uoga na kurahisisha ufundishaji.
UFUNDISHAJI HATUA YA AWALI
Charity Chikolelo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko mwenye utaalam wa kufundisha watoto wenye ulemavu anasema kuna hatua za ufundishaji kwa watoto wenye ulemavu. Anasema wako wanaoweza kuandaliwa waingie kwenye vyuo vya ufundi au wajumuishwe kwenye madarasa ya kawaida.
Hivyo anasema kabla mtoto hajaandikishwa shule huwa anapimwa kulingana na aina ya ulemavu alionao na kwamba wanaweza wakaelekeza ni visaidizi gani avitumie wakati wa kujifunza.
“Mfano wako wanaoandaliwa waingie kwenye vyuo vya ufundi lakini wengine wanaandaliwa wajumuishwe kwenye madarasa ya kawaida, kwahiyo mtoto anaweza akaandaliwa akaenda darasa la kwanza, akaja darasa la pili na akamaliza…tunaye mtoto anayemaliza darasa la saba ambaye ni kiziwi asiyeona na anafanya vizuri.
“Mimi nawashauri wazazi wasiwafiche watoto watoe taarifa kwa serikali za mitaa kwamba nina mtoto ambaye ana changamoto fulani, na mjumbe atoe ushirikiano kwa ustawi wa jamii,” anasema Mwalimu Chikoleka.
USHAURI KWA WAZAZI
Mwalimu Kilanga anawashauri wazazi wenye watoto wenye ulemavu wasiwaache kwa kudhani hawawezi badala yake wawatoe na kuwapeleka shule au katika vyuo vya ufundi huku akiwataka walimu pia kutowaogopa kwani wanafundishika.
“Ingekuwa hawezi kufanya chochote asingeweza kula lakini kama anamega tonge anaweka mdomoni tayari akili anayo, ingekuwa hana akili angeweka jichoni au sikioni au anamega anatupa…tatizo liko katika kuelewa wengine wanachelewa wengine wanawahi,” anasema.
Mwalimu Kilanga anasema wengine walikuwa wanawaogopa sababu ya mtizamo wa kijamii wanaona labda atafanya haya na yale na kwamba hali hiyo ndiyo inachangia waonekane hawawezi kitu. Lakini ukimchukua hatua kwa hatua anafanya mambo makubwa na mazuri.