32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

KINANA BADO ANA NAFASI KUSIMAMIA AHADI YA KATIBA MPYA

Na Charles Mullinda


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alipata kuwaahidi Watanzania kuwa Katiba Mpya lazima itapatikana.

Katika ahadi yake hiyo aliyoitoa akiwa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, kwa maneno yake mwenyewe alisema: ‘Katiba Mpya tunaitaka lakini isiwe ya mazingaombwe ya kukoroga vichwa vya watu, ndugu kutoana macho au kung'oana meno kwa sababu hata itakapopatikana haiwezi kugeuza chai ya rangi kuwa ya maziwa.’

Ni mtazamo wangu kuwa tamko lake hilo lilimaanisha hata itakapopatikana Katiba Mpya Watanzania tutalazimika kuifuata na kuitii bila kujali inampendeza nani na inamchukiza yupi. Hata hivyo, kila mmoja anaweza kuwa na tafasili yake kuhusu kauli hiyo ya Kinana.

Ahadi hii ya Kinana ilifurahisha wengi kwa sababu ilidhihirisha kuwa CCM ambayo yeye ni Katibu Mkuu wake ilikuwa na shauku ile ile waliyonayo wananchi wengi ya kupata Katiba Mpya na inayoendana na mazingira ya sasa badala ya ile tuliyodumu nayo kwa zaidi ya miaka 50 sasa huku ikiwa imewekewa viraka vingi.

Leo ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja, Kinana anaonekana kutoikumbuka ahadi yake, yuko kimya licha ya kelele nyingi zinazopigwa na makundi mbalimbali ya jamii kuhusu umuhimu wa kukamilisha mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya.

Sina hakika kama ukimya wa Kinana kuhusu umuhimu wa kuwa na Katiba mpya umesababishwa na kutofurahishwa na mwenendo wa kuitunga kulingana na mwenendo tulioushuhudia kuanzia kwenye ukusanyaji wa maoni ya wananchi hadi wakati wa Bunge la Katiba.

Inawezekana kama ilivyokuwa kwa baadhi ya Watanzania kuwa mwenendo wa kutungwa kwa Katiba hiyo haukumfurahisha Kinana na hiyo ndiyo sababu iliyomsukuma kukaa kimya.

Lakini binafsi ninaamini kuwa Kinana hata kama hakufurahishwa na mwenendo huo, bado anayo nafasi ya kupiga chapuo kwa wenzake ndani ya chama chake ambao ndio wanaounda Serikali ili kasoro zilizojitokeza ziweze kurekebishwa na mchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya uweze kukamilishwa.

Kinana, mwanasiasa anayeheshimika ndani na nje ya chama chake kama kiongozi mwenye maono, busara na hekima ana kila sababu ya kupigia chapuo upatikanaji wa Katiba Mpya kwa sababu kwa sifa hizo alizonazo, ninaamini anajua Katiba Mpya ndiyo itakayorejesha amani, upendo na maridhiano ya kisiasa baina ya wanasiasa wanaohasimiana kwa miaka mingi huko visiwani Zanzibar.

Kinana anajua kuwa Katiba Mpya itakuwa na suluhisho la changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa pande mbili za Muungano za Tanzania Bara na Tanzania visiwani kuhusu mgawanyo wa mapato yanayotokana na rasilimali ambazo taifa letu linazo na pia hata mgawanyo wa madarakani kitaifa.

Pamoja na mengi ambayo yamejitokeza yakionyesha umuhimu wa kupatikana kwa Katiba Mpya, lakini mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar yaliyopitishwa wakati wa kipindi cha urais ambayo yalisababisha ufa mkubwa wa kiutawala baina ya pande mbili za muungano, CCM  ina kila sababu ya kuziziba ili kuulinda muungano wetu.

CCM ambayo Kinana ni Katibu Mkuu wake, ndiyo mwasisi wa Muungano, ina kila sababu ya kuhakikisha nyufa hizo zinazibwa badala ya kuziacha ziendelee kupasua ukuta wa Muungano.

Kinana anapaswa kuiishi kauli ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa taifa letu kuwa kila mara, Watanzania waitangulize Tanzania mbele halafu mengine yote yafuate nyuma.

Iwapo atakubaliana na kauli hiyo, haina shaka kuwa kwa sababu aliuona umuhimu wa taifa letu kupata Katiba Mpya mapema, popote atakapokuwa katika ziara zake za kichama au utekelezaji wa majukumu yake kama mtendaji mkuu wa CCM aitangulize Tanzania mbele kwa kupigania upatikanaji wa Katiba Mpya ambayo itaondoa Tanzania kwenye ulimwengu wa miaka 50 nyuma na kuipeleka kwenye ulimwengu wa sasa wa karne ya 21.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles