24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Kinana abadili gia angani

Abdulrahaman Kinana
Abdulrahaman Kinana

Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana, amesema yupo tayari kuendelea kukitumikia chama hicho kama ataombwa na Rais John Magufuli.

Kinana aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma baada ya kukagua ukumbi utakaofanyika mkutano mkuu maalum wa CCM keshokutwa.

Mkutano mkuu huo unatarajiwa kumpitisha Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho baada ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kumaliza muda wake.

Kinana ameyasema hayo wakati mwaka 2012 alitangaza rasmi kung’atuka kwenye nafasi hiyo baada ya uchaguzi mkuu 2015.

Pamoja na kutangaza nia ya kutaka kuendelea na wadhifa huo, mwanzoni mwa wiki hii alikaririwa na gazeti moja la kila siku (siyo Mtanzania) akisema hatarajii kuendelea kuwa madarakani kwa sababu anahitaji muda wa kupumzika.

Katika maelezo yake hayo, alisema aliamua kushika wadhifa huo miaka michache iliyopita baada ya kuombwa na viongozi wakuu wastaafu na kwamba aliamua kuwakubalia kwa ahadi kwamba, atastaafu siasa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Pamoja na hayo, alisema mwanasiasa unapoingia madarakani, unatakiwa uandae mlango wa kuingia na mlango wa kutokea kama alivyokuwa akitarajia kufanya yeye.

Pamoja na kutoa kauli hiyo, jana alionekana kubadili ‘gia angani’ mbele ya waandishi wa habari kwa kusema yuko tayari kuendelea na nafasi hiyo kama ataombwa kufanya hivyo.

“Ni kweli nilikwishasema nitang’atuka baada ya muda wangu kumalizika, lakini kama nitaombwa, basi tutafanya mazungumzo upya kama tulivyofanya awali wakati nilipotaka kung’atuka mwaka 2012,’’ alisema Kinana.

Kuhusu mazingira ya chama chake, Kinana alisema baada ya kumaliza mkutano huo wa keshokutwa, CCM kitaanza kuwachukulia hatua waliokisaliti chama wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana.

Alisema wanachama hao wote watapata adhabu kulingana na makosa yao kwani tathimini imeshaanza kufanywa na tayari baadhi yao wameshapata adhabu zao.

Aliongeza kuwa, kila mwanachama atakayegundulika amefanya makosa wakati wa uchaguzi mwaka jana, ataambiwa makosa yake na kupewa nafasi ya kujitetea kabla ya kupewa adhabu.

Kuhusu mkutano huo, alisema maandalizi yote yamekamilika na mkutano huo utafanyika kama ulivyopangwa.

Alisema mabalozi 23 wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wanatarajia kuhudhuria na kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wajumbe wa mkutano huo, wamethibitisha kuhudhuria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles