25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kina Mbowe wasomewa upya mashtaka

KULWA MZEE

-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake wanane wanaokabiliwa na mashtaka 13 yakiwamo ya uchochezi, wamesomewa upya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliyepangiwa kusikiliza kesi yao.

Hakimu Simba alitoa maelekezo ya washtakiwa kusomewa upya mashtaka jana baada ya kupata taarifa kwamba kesi hiyo iko mbele yake.

Kesi hiyo iliyokuwa ikitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina, imepangwa rasmi kusikilizwa mbele ya Hakimu Simba baada ya hakimu aliyekuwa akiisikiliza, Wibard Mashauri kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

“Nimepata taarifa asubuhi jalada hili litasikilizwa mbele yangu, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inaelekeza washtakiwa wasomewe mashtaka upya, tusije tukafanya makosa, tukasikiliza mashahidi hata kumi mbele huko tukaambiwa limerudi kwa makosa,” alisema Hakimu Simba.

Baada ya kutoa maelekezo hayo, Wakili wa Serikali, Simon Wankyo aliwasomea upya washtakiwa mashtaka yanayowakabili.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kufanya maandamano isivyo halali na kuhamasisha chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali.

Inadaiwa Februari 16 mwaka jana katika Viwanja vya Buibui, Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwa pamoja na ujumla wao walikula njama ya kutenda makosa ya kufanya mkusanyiko usio halali, mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko la kutawanyika.

Mbowe na wenzake pia wanadaiwa Februari 16, mwaka jana, katika viwanja vya Buibui na barabara ya Mwananyamala na Kawawa, Kinondoni, walikusanyika kwa nia ya kutekeleza azma ya pamoja ya kuandamana hivyo kuwatia hofu wananchi kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani. 

Pia wanadaiwa wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani siku hiyo walikaidi agizo la SSP Gerald Thomas lililowakataza kufanya maandamano na waliandamana isivyo halali wakiwa na lengo la kuvamia ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kutokana na mkusanyiko huo wa ghasia walisababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeraha kwa  askari H. 7856PC Fikiri na E6976 CPL Rahim Msangi.

Washtakiwa wote walikana mashtaka na Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 28 na 29 kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.

 Mbali ya Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles