30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Dawa za mitishamba chanzo ugonjwa wa figo

COSTANSIA MUTAHABA (DSJ) Na TUNU NASSOR

-DAR ES SALAAAM

DAKTARI Bingwa wa Figo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Jonathan Mngumi, ameishauri jamii kuacha kutumia dawa za miti shamba ambazo hazijathibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA)  kwa kuwa huchangia kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa figo.

Sambamba na hilo ameitaka jamii kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya dawa za kupunguza maumivu za diclofenac kwa muda mrefu kwa kuwa pia husababisha ugonjwa huo ambao unashika nafasi ya sita kwa magonjwa yanayosababisha vifo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk. Mngumi alisema matumizi ya dawa hizo huathiri figo na kusababisha kushindwa kufanya kazi.

Alisema sababu nyingine inayosababisha ugonjwa huo ni kuwa na magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu.

“Niwashauri Watanzania kuacha matumizi holela ya dawa za miti shamba na diclofenac bila kushauriwa na madaktari kwani husababisha uharibifu wa figo,” alisema Dk Mngumi.

Aidha Dk Mngumi ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Madaktari wa Figo Tanzania (NESOT), Kanda ya Pwani alisema kwa sasa asilimia saba ya Watanzania wanaugua ugonjwa huo.

 “Niwashauri Watanzania kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya ya figo ili kuepuka kufika hospitali ikiwa katika hali mbaya,” alisema Dk Mngumi huku akisisitiza Watanzania kujiunga na bima za afya ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu kwa kuwa ni ghari sana.

Naye daktari bingwa wa ugonjwa huo wa kutoka Chuo Shirikishi cha Tiba (MUHAS), Dk Frida Mowo alishauri Watanzania kufanya mazoezi mara kwa mara na kula mlo kamili ili kuepukana na ugonjwa wa figo.

“Kuna aina mbili za ugonjwa wa figo ambazo zipo za mshituko wa papo kwa papo ambao unatibika ambao husababishwa na kupungukiwa damu hasa kwa wanawake wanaojifungua pamoja na wale wanaopata ajali,” alisema Dk Frida.

Dk Frida aliitaja aina ya pili ya ugonjwa wa figo sugu kwamba ni figo kushindwa kufanyakazi na haliwezi kutibika na kurudi katika hali yake ya kawaida.

“Aina hii ya pili hutibiwa kwa njia ya kusafisha damu ama kupandikiziwa figo kutoka kwa mtu mwingine,” alisema Dk Frida.

Daktari mwingine Bingwa wa Figo, kutoka MUHAS, Dk Ladius Rudovick alisema MNH imefanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa 38 tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo hospitalini hapo.

 “Ugonjwa huu hauchagui rika japokuwa umri asilimia kubwa ni kati ya miaka 35 na 45 ndio huathirika zaidi,” alisema Dk Rudovick. Hayo yamejiri wakati Tanzania ikiungana na dunia nzima kuadhimisha siku ya figo duniani inayoadhimishwa kila Alhamisi ya pili ya mwezi Machi kila mwaka

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles