Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
BENKI ya CRDB ilianzishwa Juni mwaka 1996, kufuatia marekebisho makubwa ya kiutawala, kimuundo na kifedha yaliyofanywa kuanzia mwaka 1991 ambayo yaliiweka Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini (CRDB) kwenye hali ya kuweza kubinafsishwa.
Benki hiyo ilianzishwa ikiwa na mizania ndogo iliyojumuisha amana zenye thamani za Sh bilioni 40 na rasilimali za Sh bilioni 54, ikiwa imeshikilia asilimia 5 tu ya jumla la rasilimali za mabenki yaliyokuwepo nchini kwa wakati huo. Ukiona ilivyo sasa unaweza kujua kazi kubwa iliyofanywa na hivyo kuwapongeza wahusika.
Wakati inaanzishwa ilikuwa na matawi 19 tu na mfumo duni wa Tehama, ambapo kila tawi lilikuwa linajitegemea kiuendeshaji, likiwa na mfumo wake wa kutunza hesabu zilizotokana na mfumo duni (uncomputerized system) wa kutolea huduma kwa wateja.
Kutokana na mwanzo huo mgumu, katika mwaka wa pili (1997) benki hiyo ilipata hasara ya Sh bilioni 1.8.
MWAKA 1998
Uongozi bora wa wazawa na ubunifu kwenye bidhaa na huduma uliifanya benki hiyo kutambulika, kuthaminiwa na kuzawadiwa tuzo mbalimbali na taasisi za kitaifa na kimataifa.
Dk. Charles Kimei alianza kuiongoza benki hiyo mwaka 1998 na tangu wakati huo, mambo mengi yamefanyika yaliyoiwezesha benki kupata faida mwaka hadi mwaka na kuendelea kustawi.
“Toka ilipoanzishwa, uendeshaji wa Benki ya CRDB uliongozwa na azma ya kutumia ubunifu na teknolojia ili kuwahudumia wateja vizuri na kujijengea uwezo wa kuunda bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja kwa kasi inayostahili.
“Lengo la misingi hii lilikuwa ni kujenga benki imara inayoongoza Tanzania kwa kuwafikishia wananchi wengi huduma muhimu za kifedha,” anasema Dk. Kimei.
Hadi sasa benki hiyo inajivunia mafanikio mbalimbali ikiwemo kukua kwa faida kutoka Sh bilioni 2 mwaka 1998 hadi kufikia Sh bilioni 108 mwaka 2016.
Rasilimali za benki hiyo zimekuwa kutoka Sh bilioni 54 hadi kufikia Sh trilioni 5.3 mwaka 2016.
Pia mtandao wa matawi umekua kutoka matawi 19 mwaka 1998 hadi matawi 262 mwaka 2017.
“Tulikuwa wa kwanza kuunganisha matawi yetu ili kufanya kazi kama tawi moja na hivyo kuwezesha uhamishaji wa fedha kutoka tawi moja kwenda jingine papo kwa papo tangu mwaka 1999.
“Tulikuwa wa kwanza kuanzisha mfumo wa kutoa huduma kwa wateja wetu kwa kutumia kadi za ATM mwaka 2002.
“Tulikuwa wa kwanza kubuni bidhaa inayokidhi mahitaji ya watoto (Junior Jumbo Account) na wanafunzi (Scholar Account) ambazo leo hii mabenki yote yameiga na bahati mbaya wengine wakachukua majina hayo hayo bila kujali sheria zinazolinda chapa.
“Tumekuwa wa kwanza kuingiza bidhaa mahsusi ya uwekezaji inayolenga Wanawake (Malkia Account).
“Tumekuwa wa kwanza kuona fursa katika kuwapelekea huduma za kibenki Watanzania wanaoishi nchi za nje, akaunti yenye chapa ya Tanzanite,” anasema Dk. Kimei.
Anasema sasa hivi benki imeimarika sana kwani wamekuwa kinara katika ubunifu wa bidhaa na huduma katika soko na kuwa chaguo nambari moja kwa Watanzania.
“Benki yetu ina mengi ya kujivunia, lakini nisisitize uwepo wa wafanyakazi wazuri wenye kutii masharti yanayoendana na utamaduni wa biashara tuliojiwekea na hivyo kuwa wabunifu… hii ndio siri ya mafanikio yetu,” anasema Dk. Kimei.
HUDUMA BUNIFU
Dk. Kimei anazitaja baadhi ya huduma ambazo ni bunifu kuwa ni huduma kupitia simu za mikononi (Simbanking na SimAccount), huduma kupitia mtandao (Internet Banking), huduma kupitia matawi yanayotembea yaani (mobile branches) na huduma kupitia mawakala wa FahariHuduma.
Huduma zingine ni kupitia ATM, madawati ya kimataifa ya China na India huduma kupitia kadi za kimataifa za TemboCardVisa, TemboCard MasterCard na TemboCard China Union Pay.
Benki hiyo pi imefungua kampuni tanzu nchini Burundi, Kampuni tanzu za CRDB Bank Microfinance Ltd na CRDB Bank Insurance Ltd.
Kampuni tanzu ya ‘CRDB Bank Microfinance’ inajihusisha na biashara na mikopo kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo, wakati kampuni tanzu ya CRDB Bank-Burundi imefunguliwa ili kujenga daraja la kibiashara kati ya nchi hizi mbili.
MIKOPO, AJIRA
Benki hiyo inajivunia kutoa mchango mkubwa wa maendeleo ya T1aifa kupitia utoaji wa mikopo mbalimbali ya kilimo, biashara, ujenzi na elimu.
Zaidi ya asilimia 30 ya mikopo yote inayotolewa huingia katika sekta ya kilimo, ambapo licha ya kukumbwa na misukosuko ya biashara katika soko la dunia, mikopo kwenye sekta hiyo imekua kutoka Sh bilioni 229 mwaka 2008 hadi kufika Sh bilioni 632 mwaka 2015.
Benki hiyo pia imejiwekea sera maalumu ya kuchangia kwenye mahitaji ya jamii ambapo kila mwaka hutenga asilimia moja ya faida yake ili itumike kusaidia maeneo ya elimu, afya na mazingira.
Kwa upande wa nafasi za ajira, asilimia 99.99 ni ajira za wazawa.
Benki hiyo pia ina utaratibu maalumu wa kutoa nafasi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kupata mafunzo ya kazi kwa vipindi vya kati ya miezi mitatu mpaka mwaka mmoja ili kujifunza.
Benki ya CRDB pia imeendelea kuwa kinara wa ulipaji kodi (Corporate tax) kati ya mabenki na makampuni mengine nchini.
Agosti mwaka jana, benki hiyo ilitoa gawio la Sh bilioni 19.5 zinazotokana na asilimia 21 za hisa za Serikali zilizowekezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Denmark kwenye benki hiyo.
TUZO
Umahiri wa Dk. Kimei katika masuala ya uongozi umemwezesha kupata tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi ikiwemo tuzo ya umahiri wa nyakati zote (Life Time Achievement Award) kutoka jarida la Bankers Africa mwaka 2016.
Pia alipata tuzo ya kiongozi bora wa mwaka kutoka African Business Leadership Awards na kupendekezwa zaidi ya mara tatu katika kinyang’anyiro cha African Banker of the Year.
Aidha, chini ya uongozi wake benki ilifanikiwa kupata tuzo mbalimbali kama vile tuzo ya ubora wa huduma ya ‘Euro Money’ iliyotolewa na Jumuiya ya Mabenki barani Ulaya mwaka 2004, tuzo ya umahiri wa chapa yaani ‘Superbrand’ kwa miaka mitano mfululizo toka mwaka 2010 na tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka inayotolewa na Umoja wa Waajiri Tanzania (ATE) kwa zaidi ya miaka sita mfululizo.
KUSTAAFU
Dk. Kimei anatarajia kustaafu Mei 31, 2019 ili kuwapa nafasi watu wengine kuongoza.
Anasema kuondoka kwake hakutakuwa na tatizo lolote katika benki hiyo.
“Kunaweza kuwa na hisia mbalimbali lakini mimi mwenyewe nimeamua kutoongeza muda wa mkataba. Hadi nitakapoondoka nitakuwa nimekaa miaka 21 na ninamshukuru Mungu sana kwa sababu miaka hii ni mingi na huwezi kukaa miaka yote hiyo bila kukabiliana na changamoto mbalimbali.
“Ni vizuri kuwaachia wengine ili waweze kuendeleza…nitabaki kuwa mwanahisa na mteja wa benki,” anasema Dk. Kimei.
Dk. Kimei ni Mchumi Mbobezi mwenye Shahada ya Uzamivu (Phd) kutoka Chuo Kikuu cha Uppsala nchini Sweden.
Amefanya kazi katika sekta ya fedha nchini kwa zaidi ya miongo mitatu.
Kabla ya kujiunga na CRDB, aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Sera na Ukaguzi wa mabenki ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki nchini (TBA) na kwa nyakati tofauti amekuwa akihudumu kama mwenyekiti au mjumbe wa bodi kwenye taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi.
Mchakato wa kumpata mkurugenzi mpya wa benki hiyo utaanza mwaka huu na utachukua miezi 18 hadi kukamilika kwake..