PYONGYANG, KOREA KASAKAZINIÂ
KOREA Kaskazini imefanya jaribio jingine ililoliita ‘muhimu’ katika kituo chake cha uzinduzi wa safari za Setilaiti ili kuinua kiwango chake cha udhibiti wa nyuklia, vimesema vyombo vya habari vya taifa hilo.
Msemaji ameliambia shirika la habari la KNCA kuwa jaribio hilo lilifanyika siku ya Ijumaa katika uwanja wa kituo cha uzinduzi wa Setilaite cha Sohae , lakini hakutoa maelezo zaidi.
Mazungumzo baina ya Marekani ni Korea Kaskazini juu ya mpango wake wa Nyuklia bado yamekwama.
Rais wa Marekani, Donald Trump amekataa kuondoa vikwazo hadi pale Korea Kaskazini itakapoacha mpango wake wa Nyuklia.
Lakini kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un badala yake amekuwa akitaka hakikisho jipya kutoka kwa Marekani kabla ya mwisho wa mwaka.
Korea Kaskazini imesema kuwa itachukua njia mpya kama hilo halitafanyika- ikisema kuwa Marekani itarajie “zawadi ya Krismasi ” kama haitaheshimu wito wake.
Trump ameshindwa kufikia mapatano muhimu ya kuifanya Korea Kaskazini iachane na mpango wake wa nyuklia, licha ya kufanya mikutano miwili na kiongozi Kim Jong-un na hata kufanya ziara Korea Kaskazini.
Haijawa wazi ni kitu gani hasa Korea Kaskazini ilikua inakifanyia majaribio kwenye eneo hilo.
Ankit Panda, mtaalamu wa Korea Kaskazini katika Shirikisho la Wanasayansi wa Marekani, ameiambia BBC, kuwa huenda lilikuwa ni jaribio la ardhini la injini ya makombora ya masafa.
Waziri wa ulinzi wa Korea Kusini alisema awali kuwa hilo ndilo lililokuwa lengo la jaribio mapema mwezi Disemba.
Korea Kaskazini imekuwa ikiimarisha majaribio yake ya silaha na kutoa maneno makali dhidi ya Marekani katika wiki za hivi karibuni.
Japan iliilaumu nchi hiyo kwa “marudio ya ufyatuaji wa makombora ” baada ya kufyatuliwa kwa makombora mawili mwezi wa Novemba.
Korea Kaskazini hata hivyo ilisema kuwa ilikuwa inafanyia majaribio mtambo wake mkubwa wa kufyatua roketi nyingi “, na ikatishia kuwa Japan huenda ikashuhudia makomborra halisi katika kipindi kijacho ambacho si kirefu.