Na Mwandishi Wetu, Kilwa
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imepata hati inayoridhisha katika ukaguzi unaofanywa na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016.
Taarifa za ukaguzi zimeonesha kuwa utunzaji wa kumbukukumbu, ukusanyaji wa mapato na matumizi umekidhi sifa za kikaguzi.
Hayo yalielezwa na Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Mkoa wa Lindi, Deogratius Mtenga wakati wa kikao cha baraza maalumu la madiwani wa halmashauri hiyo ambacho pia kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack na Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge.
Akiwasilisha taarifa ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2019/2020 Mtenga amesema hoja 61 zilikaguliwa na zote zilijibiwa.
Amesema hoja zilizofungwa ni 32 huku hoja 29 zikiwa bado hazijafungwa na hivyo kulitaka baraza la madiwani kuendelea kuzitafutia majibu ili nazo ziweze kufungwa.
Mkaguzi huyo Mkuu wa nje wa Mkoa wa Lindi amezitaja baadhi ya hoja zilizokaguliwa kuwa ni pamoja na halmashauri kuchelewa kuuza mali chakavu, kutoteketezwa kwa dawa zilizoisha muda wake, baadhi ya magari ya halmashauri kuwa na namba binafsi pamoja na watumishi kukaimu kwa muda mrefu katika nafasi za ukuu wa idara na vitengo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Renatus Mchau, amesema hatua mbalimbali zimeshachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuiandikia Wizara ya Fedha na Mipango kuomba kibali cha uteketezaji ambacho kimeshapatikana tangu Juni 15, 2021.
Kuhusu hoja ya watumishi kukaimu muda mrefu Mkurugenzi huyo amesema baadhi ya watumishi walikosa sifa za nafasi wanazozikaimu na hivyo utaratibu unafanyika wa ama kuwaombea vibali vya kuendelea kukaimu au kujaza nafasi endapo watu wenye sifa zinazohitajika watapatikana.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, amewapongeza kwa kupata hati hiyo huku akiwataka kuchukua hatua za haraka katika hoja ziliobaki ili ziweze kufungwa.
Aidha amewataka madiwani kufanya kazi kwa pamoja na wataalam ili kuweza kutatua changamoto kwa haraka.
“Waheshimiwa madiwani nyie ndiyo wasimamizi wa halmashauri kwa mujibu wa sheria lakini usimamizi wenu utafanikiwa tu endapo mtafanya kazi kwa kushirikiana, kukiwa na mvutano kati yenu mtakwama na mkikwama mtakuwa mmemkwamisha Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye anaamini nyie kwa nafasi zenu mna uwezo wa kuwaletea wananchi wenu maendeleo,’’ amesema Telack.
Akifunga baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri, Farida Kikoleka, amewataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku akimhakikishia mkuu wa mkoa kuwa halmashauri hiyo ina ushirikiano mkubwa na watumishi hivyo asiwe na wasiwasi.