24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Kilio hiki cha Kanisa Katoliki ni cha wengi

JUZI Baraza la Maaskofu wa Kanisa  Katoliki Tanzania(TEC) lilisema kanisa hilo limetikiswa kiuchumi kutokana na taasisi zake nyingi zinazotoa huduma kusimama katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Covid 19.

Kutokana na hilo Katibu Mkuu TEC, Charles Kitima aliyezungumza na waandishi wa habari  aliiomba Serikali kufanya mazungumzo na wamiliki wa taasisi zisizotengeneza faida.

Alisema kutokana na hali ya ugonjwa huo kuna baadhi ya nchi zimewasaidia watu wake katika masuala ya kodi.

Alitolea mfano  Kenya akisema wamefuta kodi kwa watu wao lakini wao  kwa kuwa wamewekeana mkataba na Serikali inawalazimu kulipa kodi.

Katika hilo Kitima aliiomba Serikali kuboresha mazungumzo na taasisi  zao 

Alisema kanisa hilo lina taasisi nyingi za afya, elimu na za huduma za kiroho ambazo zinatoa huduma bila kutengeneza fedha za ziada ambazo wangeweza kuziweka pembeni ili kusaidia panapokuwa na shida.

Kwa mujibu wa Kitima, kanisa hilo hutegemea anayepokea huduma zao alipe na wao waweze kuwalipa wafanyakazi ambao ni wahudumu wa afya na walimu. 

Alisema kwa upande wa taasisi za afya hawajaathirika sana kwa kuwa waliendelea kupokea wagonjwa tofauti na upande wa elimu ambako athari imeonekana kubwa kuanzia shule za chekechea, msingi na sekondari na vyuo vikuu kwa kuwa wanategemea wanafunzi walipe ada ndipo nao waweze kuwalipa wafanyakazi wao.

Alisema kadiri uwezo wa wazazi kulipa ada unavyopungua ndio uwezo wao wa kuwalipa watumishi nao unapungua.

Kauli hiyo ya Katibu Mkuu huyo wa TEC haina tofauti na kile tulichokiandika mara kadhaa tukisisitiza hatua za kukabili hali ngumu ya uchumi.

Kwa bahati nzuri Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua hatua katika eneo la fedha, ingawa tulisisitiza hatua kama hizo pengine zingechukuliwa katika maeneo mengine kama yale yanayohusu kodi kwa kuwa si tu Kanisa Katoliki bali wengi biashara na huduma zao zimeyumba katika kipindi hiki.

BoT kwa upande wake ilitangaza kuchukua hatua sita za kisera kukabiliana na athari za corona kwenye benki ikiwa ni pamoja na kupunguza riba, amana, hati fungani na dhamana.

Lengo la hatua hizo ni kudumisha uthabiti wa sekta ya fedha na upatikanaji wa huduma za fedha nchini.

Hatua zilizochukuliwa ni kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa BoT kutoka asilimia saba hadi sita, kuanzia Juni 8, mwaka huu.

Wakati BoT wakichukua hatua hiyo tuliandika huko nyuma kwamba tayari baadhi ya watu biashara au kazi zao zimeathirika kutokana na ama kufunga au kushuka hasa kwa wakati huu.

Upo ushahidi mwingi wa biashara kuporomoka  kutoka kwa wenye vituo vya mafuta, wauza nguo, wakulima wakubwa , wafanyakazi wa sekta binafsi, likiwamo kundi kubwa la walimu na wengine.

Miongoni mwa hao  wapo ambao walichukua mikopo mikubwa na sasa hali imekuwa tofauti.

Watu hao hao na wengine ndio wanaokabiliwa na madeni makubwa ya mapango, mahitaji yao ya kila siku na mengine.

Tuliona Serikali ya Kenya ikitangaza kuchukua hatua ili kuwanusuru raia wake ambao wameyumba kiuchumi katika wakati huu.

Miongoni mwa hatua ambazo Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ilichukua mapema kabisa ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya kaya zisizojiweza ikiwamo  familia zisizojiweza.

Huko nyuma pia tuliona Marekani ikiongeza tena dola nusu bilioni mbali na zile dola trilioni mbili kwa ajili ya raia wake waliopoteza ajira katika wakati huu wa janga la corona.

Tuliandika kwamba hatuwezi kamwe kujilinganisha na Marekani kwa uwezo na kila kitu, lakini tunachotaka kusema pamoja na hatua zilizochukuliwa na BoT, mamlaka nyingine za Serikali nazo zifikirie namna ya kuwapunguzia mzigo wananchi wake hususani kwenye suala zima la kodi.

Tunasema hivyo kwa sababu tunaamini bila kufanya hivyo, wengi watalazimika kufunga biashara na huko mbele Serikali  ikajikuta imepoteza walipa kodi wengi zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles