30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

KILIO CHA WANAWAKE KUMILIKI ARDHI BADO KITENDAWILI

Na JOHNAES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM


KILA baada ya miaka miwili taasisi, asasi na mashirika mbalimbali yanayojishugulisha na utetezi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia hufanya tamasha la kijinsi linalowaunganisha wanawake kutoka ndani na nje ya nchi.

Tamasha la mwaka huu lilifanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 5 hadi 8, likiratibiwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) katika viwanja vya ofisi hiyo Mabibo jijini Dar es Salaam. Mada kuu ilikuwa ni ‘Mageuzi ya Mifumo Kandamizi kwa Usawa wa Jinsia na Maendeleo Endelevu.’

Wanawake zaidi ya 1,500 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaungana kujadili changamoto na mafanikio yaliyopatikana kutokana na harakati walizozifanya katika kipindi cha miaka miwili katoka michakato ya kuleta usawa wa jinsia na maendeleo.

Wanawake ambao walitoa mchango mkubwa katika kuleta ukombozi wa wanawake kimapunduzi na kupigania usawa wa kijinsia wakapata nafasi ya kutambuliwa mchango wake kwa kupewa tuzo. Miongoni mwa waliopata tuzo hizo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda, Mbunge wa Bunda Mjini Chadema, Ester Bulaya na wengine.

Washiriki wakapata fursa ya kujadili mada mbalimbali ili kuangalia ni wapi wamefikia na changamoto gani bado inawakabili.

 

Umiliki wa ardhi

Dk. Vicencia Shule ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TGNP, anasema mwanamke hawezi kuinuliwa kiuchumi kama hatakuwa na haki ya kumiliki ardhi.

Anasema umiliki wa ardhi kwa wanawake  bado ni changamoto ambapo hadi sasa ni asilimia 20 tu ya wanawake ndio wanaomiliki ardhi.

“Hatuwezi kuwa na maendeleo kiuchumi kama mwanamke hatakuwa na haki ya kumiliki, kutumia na kuamua matumizi ya ardhi kwani ili nchi iweze kuendelea haipaswi kumwacha mtu nyuma.

Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya Ardhi kutoka Shirika la Kimataifa la Care, Mary Ndaro anasema ili kufikia uchumi wa kati na wa viwanda serikali haipaswi kuwaacha wanawake nyuma hasa ukizingatia kuwa ndio kundi kubwa la Watazania wote kwa asilimia zaidi ya 51.

Anasema nchi yoyote ili iweze kuendelea inatakiwa iende na wananchi wake wote na si idadi fulani ya watu. Hivyo, kwa Tanzania ambayo ina wanawake zaidi ya asilimia 51 ili iweze kuendelea lazima isiwaache nyuma.

“Sina maana kuwa wanaume waachwe nyuma, lakini ni muhimu kama nchi inataka kuendelea lazima isiwaache wanawake kwa kuhakikisha wanamiliki ardhi, kutumia na kufanya uamuzi kwenye vyote vitokanavyo na ardhi.

“Hapo ndipo tutapata nafasi ya kuzungumzia maendeleo, Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati, lakini tukiacha hawa wananchi ambao ni wengi tutakuwa tunapoteza muda,” anasema Mary.

Anaongeza: “Tuna jukumu la kuhakikisha sera na sheria zetu hazimfanyi mwanamke kuwa ili aweze kumiliki fursa za kiuchumi lazima aungane na mwanamume kwa sababu si wanawake wote wenye wanaume pembeni wa kuwashikilia.

“Imetosha kusema kuwa kidogo kidogo wanawake watasogea, wakati wa kusogea ni sasa kwani karibu asilimia 70 ya wanawake Tanzania ardhi inawahusu haijalishi wa kijijini au mjini. Tunapozungumzia ukombozi wa kiuchumi lazima ardhi ihusike kwa mlengo wa kijinsia,” anasema Mary.

 

Mifumo kandamizi

Suala la mifumo kandamizi ambayo imekuwa moja ya changamoto ya kufikia usawa wa kijinsia linajitokeza, ambapo mwakilishi wa Ekama Development Foundation Tanzania, Lucia Akaro anasema jitihada za haraka zinahitajika kuiondoa mifumo hiyo inayomkandamiza mwanamke.

“Kundi la wanawake ndilo linaloathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi na hata  kupambana na  ukatili  wa  kijinsia.  Kuna haja  ya  kuanzisha  majukwaa ya kuelimisha jamii ili kuondokana na unyanyasaji  wa  familia kupitia  ardhi ama mavuno,” anasema.

Anazitaja athari zitokanazo na ukatili kuwa ni kupungua kwa nguvu kazi hivyo wanawake kukosa kipato na kuwasababishia umaskini.

Anasema kuwapo kwa mifumo kandamizi kumeongeza mimba za utotoni kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi asilimia 27 mwaka 2016/17.

 

Elimu kwa watu wenye ulemavu

Tamasha hilo liliwashirikisha watu kutoka makundi mbalimbali wakiwamo wenye ulemavu ambao kilio chao kiko kwenye utekelezaji wa sera ya elimu bure.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu ya Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Doris Kulanga anasema licha ya kuwapo kwa sera ya elimu bure, watu wenye ulemavu wanalazimika kutumia gharama kubwa kuitafuta.

Anasema watoto wengi wenye ulemavu wanatoka kwenye familia duni hivyo wanashindwa kupata fursa hiyo kwa kuwa  shule zipo mbali hivyo hulazimika kugharimia usafiri.

Nasiria Ally ni mlemavu wa kusikia, anasema kundi hilo limeachwa nyuma kielimu ukilinganisha na makundi mengine, kwamba shule nyingi za walemavu wa kusikia  hazina vifaa vya kutosha na hata kwenye vyombo vya uamuzi hawashirikishwi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi anaishauri serikali na wadau wa  maendeleo kuangalia usawa wa elimu katika nyanja zote, kila mtu apate elimu bila vikwanzo.

“Ukosefu wa mabweni na shule kuwa mbali na makazi ya watu ni moja ya changamoto zinazowaathiri zaidi watoto wa kike jambo ambalo limechangia ongezeko la mimba za utotoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles