26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kilio cha Neymar Jr kina maana nyingi

BADI MCHOMOLO

ZILITUMIKA dakika 21 tu kwa nyota wa timu ya taifa ya Brazil, Neymar Jr kufuta ndoto zake za kuisaidia timu hiyo kubeba taji la Copa America kwenye ardhi ya nyumbani.

Ilikuwa katika mchezo wa kirafiki kati ya Brazil dhidi ya Qatar, huku Brazil wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani walifanikiwa kushinda mabao 2-0 kwenye uwanja wa Mané Garrincha, lakini Neymar alitolewa nje kutokana na kuumia enka ya mguu wa kulia.

Alitolewa uwanjani huku akilia, tena alikuwa anatembea kwa kusaidiwa na madaktari wa timu hiyo ya taifa, kulia kwake kulikuwa na maana nyingi sana.

Miongoni mwa vitu ambavyo Neymar vinamfanya alie akipata maumivu ni pamoja na kuhofia kuukosa ufalme ndani ya Brazil, kushuka kwa thamani yake pamoja na mengine.

Brazil ni sehemu ambayo inajulikana kwa kutoa wachezaji wengi wenye kutikisa dunia kwa miaka tofauti, kama ilivyofanywa na Edeson Pele, Ronaldo de Lima, Ronaldinho, Rivaldo, Roberto Carlos na wengine wengi.

Kwa miaka ya hivi karibuni Neymar amakuwa akitajwa kuja kuwa mfalme baada ya mastaa hao kutokana na uwezo wake wa kucheza soka, lakini inawezekana ikawa ndoto kwake kutokana na majeraha anayoyapata mara kwa mara.

Alikuwa katika kiwango cha hali ya juu akiwa ndani ya Barcelona, lakini baada ya kuondoka Agosti 13, mwaka 2017 na kujiunga na klabu ya PSG, bado hajaonesha kiwango cha zaidi ya Barcelona, kikubwa ni majeruhi ya mara kwa mara.

Tangu ajiunge na PSG mwaka 2017, ameumia mara 11 na kumfanya akose baadhi ya michezo, majeraha makubwa yalianza kumkuta Februari 26, mwaka jana ambapo alivunjika mifupa ya vidole vya mguu na kumfanya awe nje ya uwanja siku 90 (miezi mitatu), na kukosa michezo 16 ya PSG.

Januari 24 mwaka huu aliumia kifundo cha mguu na kumfanya awe nje ya uwanja kwa siku 85 na kukosa michezo 18 ya PSG.

Hadi kufikia hapo tayari PSG wameanza kuichoka huduma mchezaji huyo kwa kuwa hameshindwa kuiunganisha timu ili kufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kushirikiana na wachezaji wenzake.

Juni 5, wiki hii ameumia tena, amechanika enka ya mguu wa kulia ambapo ameripotiwa kwamba ataikosa michuano ya Kombe la Copa America inatarajiwa kuanza kufanyika Juni 14 mwaka huu huku Brazil wakiwa wenyeji kwenye ardhi ya nyumbani.

Amelia sana! Amelia kutokana na maumivi aliyokuwa anayapata, lakini amelia kwa kuwa anakwenda kuikosa Copa America kwenye ardhi ya nyumbani mbele ya idadi kubwa ya mashabiki, lakini amelia huku akiamini ufalme wake katika soka unaanza kupoteza na amelia kwa kuwa umri wake unazidi kusogea akihofia kushindwa kufanya makubwa kwa taifa lake kama walivyofanya waliopita.

Kitu kikubwa ambacho Neymar anajivunia kwa sasa ni kuipa Brazil ubingwa wa michuano ya Olimpic mwaka 2016 akiwa nahodha, lakini ana deni kubwa kwenye Kombe la Dunia au Copa America, anastahili kulia.

Mwaka 2014 kwenye Kombe la Dunia nchini humo, Neymar alilia sana kwa kuwa alivunjika pingili ya mgongo, lakini safari hiyo alilia na wengi kwa kuwa walishindwa kutamba kwenye ardhi ya nyumbani.

Kwa sasa tayari Wabrazil wameanza kuzoea maisha bila ya Neymar, wanaanza kuufuta ufalme wake na ndioa maana kwa sasa nahodha wa timu hiyo amepewa beki wa pembeni Dani Alves.

Mapema mwaka jana Neymar alitangazwa kuwa miongoni mwa wachezaji watatu duniani ambao wanaingiza kiasi kikubwa cha fedha kwa mwaka badala ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Huko ndiko alikobaki Neymar, lakini kwenye ushindani wa soka jina lake lipo chini sana, dalili tosha za kupoteza ufalme wake kwa kuwa anashika nafasi ya saba kwa wachezaji ambao wanatajwa sana kwenye ufalme wa tuzo mbalimbali.

Wachezaji wanaotamba kwa sasa ni Messi, Ronaldo, Eden Hazard, Mohamed Salah, Kylian Mbappe, Virgil van Dijk na anafuata Neymar. Kweli anastahili kulia kwa kuwa ushindani wa kulinda heshima yake ni mkubwa sana na anaweza hasiuweze.

Ni wazi kwamba, hana furaha ya soka ndani ya PSG kama ilivyo akiwa Barcelona, ikumbukwe kwamba aliondoka Barcelona huku akidai anatafuta ufalme mbali na Messi, kwa kuwa aliamini hawezi kufanya hivyo akiwa anacheza pamoja na bingwa huyo.

Japokuwa sababu nyingine ambayo ilimfanya aondoke Barcelona ni pamoja na ofa kubwa ambayo iliwekwa na PSG kwa ajili ya kumsajili mchezaji huyo Euro milioni 222 na kuwa mchezaji wa kwanza duniani kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha, lakini sasa amedai yupo tayari arudi Barcelona.

Naymar amekuwa mchezaji wa vituko kwa sasa, kule PSG amefungiwa michezo mitatu kwa kumpiga shabiki, lakini kesi kubwa aliyonayo sasa ni tuhuma za ubakaji zilizotokea Mei 15 kwenye moja ya hoteli nchini Ufaransa.

Soka lake linakwenda pabaya, sio mwisho mzuri alioutaka akiwa na umri mdogo katika ndoto zake za kucheza soka, labda alikuwa na ndoto za kufanya makubwa zaidi ya Ronaldinho, Ronaldo de Lima, Pele na wengine. Hii inamuumiza sana, lazima alie.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles