24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

KILIMO CHAWATIA HOFU WABUNGE

 

 

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

BAADHI ya wabunge wameonyesha hofu juu ya ukuaji wa sekta ya kilimo nchini.

Hofu hiyo waliionyesha jana wakati walipochangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliyowasilishwa juzi na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Charles Tizeba.

Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Kigoma Mjini, (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, alisema kutokana na Serikali kutowekeza katika sekta hiyo, idadi ya masikini nchini imekuwa ikiongezeka ingawa takwimu zinaonyesha pato la taifa limekuwa likikua.

 “Mwaka 2009, Pato la Taifa lilikua kwa Dola bilioni 21.4 za Marekani na mwaka 2016 pato hilo lilikua kwa Dola bilioni 52 za Marekani.

“Pamoja na kwamba Pato la Taifa linakua, idadi ya masikini nchini inazidi kuongezeka. Tatizo hapa ni nini, tatizo ni Serikali kutowekeza katika sekta ya kilimo ambayo tunaambiwa inahusisha asilimia 65.5 ya Watanzania.

“Kwa hiyo, ili kuondokana na hali hiyo, lazima sasa Serikali iwekeze katika kilimo kwa sababu ndicho chenye idadi kubwa ya watu,” alisema Zitto.

Mbunge wa Kigoma Mjini, (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe
Kwa upande wake, Mbunge wa Mufindi Mjini, Mahmoud Mgimwa (CCM), alisema kama Serikali haitawekeza zaidi katika kilimo kama ilivyo sasa, uwezekano wa maisha ya Watanzania kuimarika utakuwa mdogo kwa kuwa kilimo ndicho chenye idadi kubwa ya Watanzania.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba (Chadema), pamoja na kutoridhishwa na utaratibu wa Serikali kuagiza ng’ombe wapigwe mihuri wakati inaharibu ngozi za wanyama hao, alisisitiza umuhimu wa Serikali kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutenga fedha nyingi ili kiweze kuleta mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

Wakati hao wakisema hayo, Mbunge wa Pangani, Jumaa Aweso (CCM), alizungumzia kilimo cha umwagiliaji na kusema kuna haja ya kukiimarisha kwa kuwa kilimo cha kutegemea mvua hakiamini zaidi.

“Jimboni kwangu Pangani kuna Mto Pangani, lakini jambo la ajabu ni kwamba mto huo unamwaga maji baharini na sisi hatuyatumii katika umwagiliaji.

“Kwa hiyo, naona sasa kuna haja kwa Serikali kuanza kuimarisha kilimo hicho kwa sababu bila kufanya hivyo, sekta ya kilimo haitachangia kikamilifu katika Pato la Taifa,” alisema.

Naye Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), alihimiza kilimo cha umwagiliaji nchini na kushangaa ni kwa nini hakifanyiki mkoani Morogoro ambako alisema kuna mito zaidi ya 1,000.

Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige (CCM), alisema kama kilimo cha umwagiliaji hakitaimarishwa nchini, ikiwamo Shinyanga ambako kuna bonde linalofaa kwa kilimo hicho, Watanzania hawataepuka upungufu wa chakula ambao umekuwa ukiwakabili kila mara kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles