NA GLORY MLAY
KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake Tanzania Bara (Kilimanjaro Queens), Bakari Shime, amesema kikosi chake kipo fiti kushiriki michuano ya Cecafa Challenge itakayofanyika Mei 19, mwaka huu, nchini Rwanda.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Shime, alisema wamejipanga kuhakikisha hawafungwi kirahisi ili kutolewa katika michuano hiyo, kwani wachezaji wote wana morali ya kutosha ya kupata matokeo mazuri.
“Hatutakubali kupoteza michezo hiyo kirahisi, kwani ni muhimu kwetu kushinda, tumejiandaa kuhakikisha timu inapata ushindi ili iweze kupiga hatua inayofuata,” alisema Shime.
Shime alisema ameangalia baadhi ya mechi za wapinzani wao, hivyo watayatumia mapungufu aliyoyaona kwa baadhi ya timu na kuibuka na ushindi.
Kikosi cha Kilimanjaro Queens kimeundwa na wachezaji 25, kinaendelea na mazoezi katika Uwanja wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, kujiandaa na michuano hiyo ya wanawake.