24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

MAMBO MAWILI YALIYO MREJESHA LULU URAIANI

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM


IKIWA ni siku ya nne ya msanii Elizabeth Michael (Lulu), kuwa uraiani baada ya kutoka Gereza la Segerea Jumamosi Mei 12, Magereza imeeleza sababu zilizofanya abadilishiwe kifungo.

Akizungumza na Mtanzania jana, Naibu Kamishna wa Magereza, Augustino Msanii alisema moja ya sababu iliyofanya Lulu kuwa nje ni msamaha wa Rais John Magufuli, alioutoa kwa wafungwa Aprili 26.

Alisema katika msamaha huo, Lulu ni mmoja wa wafungwa ambao robo ya vifungo vyao ilipunguzwa na  Rais.

Sababu ya pili alisema ni amri ya Mahakama Kuu ambayo imeamua Lulu kutoka gerezani na atumikie kifungo cha nje akiwa anafanya kazi za kijamii Wizara ya Mambo ya Ndani mpaka Novemba 12, ambapo atakuwa huru.

“Ieleweke bado ni mfungwa wetu na angeendelea kukaa gerezani hadi Novemba 12, ila hiki kifungo kimepunguzwa kwa msamaha wa Rais, bila msamaha wa Rais ilikuwa atoke Machi 12, mwaka 2019.

“Kwa hiyo bado ni mfungwa kwa mujibu wa Sheria ya Community Service Namba 6 ya 2002 ambayo inaruhusu mtu kutoka akawa na kifungo cha nje, yaani kifungo cha huduma za jamii. Hii ina maana atapangiwa kazi wilayani, sijui wilaya gani na atapangiwa kazi kwa masaa fulani kwa siku tano. Hatakuwa chini yetu kwa masharti ya sheria hiyo,” amesema.

Uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam uliamuru msanii huyo amalizie kufungo chake akiwa nje ya gereza.

Sehemu ya uamuzi huo ambao MTANZANIA limeuona ulisomeka hivi; “Lulu alihukumiwa Novemba mwaka jana baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua Steven Kanumba bila kukusudia na kuhukumiwa kwenda jela miaka miwili.

“Alitakiwa kumaliza kifungo Novemba mwaka huu baada ya kifungo chake kupungua kutokana na msamaha wa Rais.

“Lulu alikuwa miongoni mwa wafungwa waliopata msamaha,  kifungo kilipungua hivyo akaomba amalizie akiwa nje kwa kufanya kazi za jamii.”

Jaji Ama-Isario Munisi, aliyetoa uamuzi huo aliamuru awe chini ya Ustawi wa Jamii na awe anafanya kazi za huduma za jamii katika Wizara ya Mambo ya Ndani. .

Novemba 13 mwaka jana, Jaji Sam Rumanyika baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa Jamhuri na utetezi wa mshtakiwa alimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka miwili.

Lulu alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili, 2012 akishtakiwa kwa kosa la kumuua Steven Kanumba Aprili 7, mwaka huo, tukio lililotokea Sinza Vartican.

“Katika mazingira hayo ya mshtakiwa kuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu, sheria inamtaka kutoa maelezo ya kina kuhusu kifo cha marehemu na akishindwa yeye ndiye anakuwa muuaji.

“Ushahidi wa mazingira unaweza kumtia hatiani pale ambapo ushahidi wote unamnyooshea kidole mshtakiwa peke yake mwanzo mwisho…ushahidi wa shahidi wa kwanza ni kwamba kulikuwa na mzozo, ushahidi huo mshtakiwa alikubali kwamba kweli kulikuwa na mzozo akapigwa na marehemu.

“Mwingine anaweza kusema kapigwa au kulikuwa na ugomvi, tafsiri ya ugomvi ni ile kurushiana maneno ya kejeli, dharau, kizembe, kwa aliyeanzisha alikuwa na nia ya kumuudhi mwenzake…hilo si la msingi sana, kwa maoni yangu kutokana na tafsiri hiyo basi kuanguka ni miongoni mwa matukio yanayotazamiwa kutokea katika ugomvi,”alisema Jaji Rumanyika.

Jaji Rumanyika alisema mshtakiwa katika utetezi wake alisema marehemu alikuwa kalewa na kwa msingi huo mlevi kati ya mambo anayofanya ni kuanguka ovyo.

“Kuhusu hili mshtakiwa alijikanganya, anasema marehemu alimfukuza akamudu kumkamata na kumrudisha chumbani kwa kumburuza lakini hakusema wakati akimfukuza na kumburuza kama alikuwa akianguka.

Alisema mshtakiwa alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu hivyo alitakiwa kuelezea nini kilitokea.

“Tunabakia na watu wawili wa kusema kwa kina kuhusiana na tukio hili ambao ni mshtakiwa na marehemu…marehemu hata akifufuka kwa muujiza …mahakama haitasikiliza muujiza.

“Pengine anaweza akatokea mtu mwingine akasema Aprili 7, 2012 wakati tukio likitokea mshtakiwa alikuwa na umri wa miaka 17, hakuwa mtu mzima..kwa umri huo anaweza kusema asingeweza kujua mabaya.

“Hili lina mazingira yake makuu matatu, moja…alikuwa mtoto aliyefikia hatua fulani akiitwa mke alikubali, pili, mtoto wa aina yake mshtakiwa alithubutu na kuamua ndivyo sivyo kwa matakwa yake… anajiamulia wapi aende na tatu, mtoto wa aina yake mshtakiwa anaamua kwenda matembezini usiku wa manane, akamtembelea mpenzi wake na kisha akaendelea na matembezi yake.

“Mshtakiwa huyu si wale watoto waliolengwa kulindwa katika sheria ya mtoto…kama mtoto anaweza kufanya ya watu wazima na akajiamini kuyafanya ni mkomavu.

“Sitaki kuwa wa kwanza kuonyesha kushindwa …kifo cha marehemu Kanumba kimetokana na mshtakiwa kifo kinachotokana na ugomvi hupelekea aina hii ya mashauri,”alisema Jaji Rumanyika.

Alisema sheria ya kuua bila kukusudia ina lengo la kudhibiti vitendo hivyo na kwamba katika mashauri mengi muuaji si lazima ithibitike.

“Kwa kuwa mshtakiwa kasema marehemu alikuwa na wivu usio na msingi, wivu huo ndio ulisababisha kupigwa ….hakuna mchezo usio na kanuni…mapenzi ni mchezo basi wivu ndio kanuni zake.

“Kama aliamua kuingia katika mchezo basi afuate kanuni, wivu wa maendeleo huzaa maendeleo lakini wivu wa mapenzi huzaa maangamizi. Mshtakiwa alijua marehemu ana wivu basi alipoanza kushukiwa kuhusu simu alitakiwa kwa kanuni ya mapenzi aache simu lakini yeye aliamua kama noma na iwe noma.

“Kutokana na ushahidi huo mahakama inamtia hatiani mshtakiwa chini ya kifungu namba 195 ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu,”alisema Jaji Rumanyika na kuwataka mawakili wa pande zote kusema lolote dhidi ya mshtakiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,853FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles