24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kilichomtumbua DCI Diwani

Diwani Athuman
Diwani Athuman

Na MWANDISHI WETU,

RAIS Dk. John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) Diwani Athuman.

Taarifa iliyosambazwa jana kwenye vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa ikimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, haikuweka bayana sababu za uamuzi huo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Diwani atapangiwa kazi nyingine na kwamba uteuzi wa DCI mpya utatangazwa baadaye.

Pamoja na kwamba taarifa ya Ikulu haikutaja sababu za kuondolewa kwa Diwani katika nafasi hiyo, taarifa ambazo hazijathibitishwa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinadai kuwa huenda uamuzi huo umechukuliwa kutokana na kiongozi huyo kushindwa kutimiza wajibu wake sawasawa.

Taarifa nyingine zinadai kuwa kuondolewa kwa Diwani kunatokana na Rais Dk. Magufuli kutaka kupanga safu yake mpya.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Diwani anadaiwa kushindwa kuendana na kasi anayoitaka Rais Magufuli ya mapambano dhidi ya uhalifu.

Diwani licha ya kuelezwa kuwa ni kiongozi mwadilifu, mchapakazi na asiye na haraka katika kutoa maamuzi, anadaiwa kushindwa kushiriki ipasavyo katika operesheni maalumu zinazofanywa kimya kimya dhidi ya watu waliotajwa kuwa ni wahujumu uchumi.

Taarifa zinadai kuwa tukio la hivi karibuni ambalo linahisiwa kuwa chanzo cha kuondolewa katika nafasi yake, ni la kumnusuru mmoja wa wahalifu aliyenaswa katika operesheni ya kimya kimya inayoendelea.

Inadaiwa mhalifu huyo alikamatwa hivi karibuni kwa madai ya kulihujumu taifa, lakini aliachiwa kimya kimya kwa maelekezo ya Diwani.

“Jamaa inadaiwa alipigiwa simu na mtu mmoja kuwa amekamatwa, hivyo akawa kama anajaribu kuzuia wasimtie matatani, sasa waliokuwa kwenye operesheni wakatoa taarifa kwa viongozi wa juu,” kilisema chanzo kingine na kuongeza;

“Huenda hii ndiyo sababu kubwa kwa sababu jamaa alikuwa mbali na operesheni hizo.”

Itakumbukwa kuwa Diwani ameondolewa katika nafasi hiyo akiwa amefanya kazi kwa takribani mwaka mmoja na miezi mitano, baada ya kuteuliwa Mei, mwaka jana na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Alipoteuliwa kushika wadhifa huo Mei 12, 2015, Diwani alieleza matarajio yake kuwa ni pamoja na kuona Tanzania inaendelea kuwa na amani, utulivu na usalama.

Uamuzi wa Rais Magufuli kumwondoa Diwani katika nafasi yake hiyo, licha ya hulka yake ya uadilifu na uchapakazi, umeonekana kuwashtua baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi na polisi kwa ujumla.

Wakati wa mchakato wa kumtafuta mrithi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Said Mwema, alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushika nafasi hiyo kutokana na uadilifu na utendaji wake ndani ya jeshi hilo.

Hata hivyo, nafasi hiyo ilichukuliwa na Ernest Mangu, huku yeye akiteuliwa kushika nafasi ya DCI iliyoachwa wazi na Robert Manumba ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya uteuzi huo, Diwani alikuwa Kaimu Kamishna wa Kamisheni ya Intelijensia ya Jinai na alipoteuliwa kuwa DCI, nafasi hiyo ilichukuliwa na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Valentino Mlowola ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Kabla ya hapo, mwaka 2012, Diwani alihamishiwa mkoani Mbeya kuchukua nafasi ya Kamanda Advocate Nyombi na kuwa kamanda wa polisi wa mkoa huo.

Diwani pia kabla hajawa RPC, aliwahi kushika nafasi nyingine za kiutendaji na kiutawala kama mlinzi (Bodyguard) wa IGP mstaafu Omari Mahita, Kaimu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles