27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Kili MediAir yaendeleza huduma za uokozi na utalii wa anga kwa watalii nchini Tanzania

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Kampuni ya Kili MediAir, inayotoa huduma za uokozi kwa njia ya anga nchini Tanzania, imeendelea kuboresha huduma zake na kujikita katika utalii wa anga ili kuwapa fursa Watanzania na watalii wa kimataifa kufurahia mandhari za kipekee nchini.

Akizungumza Oktoba 12, 2024, katika maonyesho ya nane ya S!TE yanayoendelea katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Daktari wa Uokozi wa Kili MediAir, Dk. Jimmy Daniel, alisema kampuni hiyo imetimiza miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake. Alieleza kuwa, kampuni hiyo imejikita zaidi kaskazini mwa nchi, huku ikipanga kufikia vivutio vyote vya utalii nchini.

“Mbali na uokozi, tumepanua wigo wetu ili kutoa huduma ya utalii wa anga. Tunakutana na watu wanaotamani kutembelea vivutio kama Mlima Kilimanjaro, lakini kutokana na umri au maradhi wanashindwa. Kwa hiyo, tunawapa fursa hiyo kwa kutumia helikopta,” alisema Dk. Jimmy.

Hata hivyo, alibainisha changamoto zinazowakabili, ikiwemo uelewa mdogo wa watu kuhusu huduma za ziada wanazotoa. “Wengi wanadhani sisi tunatoa tu huduma za uokozi, lakini sasa tunatoa elimu kwa umma kwamba tunahusisha pia huduma za utalii wa anga,” alieleza.

Changamoto nyingine alizozitaja ni upatikanaji wa bima kwa watalii wanaopata changamoto za kiafya wakati wa safari zao, pamoja na kuwasaidia watu wenye changamoto za kifedha, kama wapandaji milima na wabeba mizigo. “Kwa kuwa ni Watanzania, tunaona fahari kusaidia bila kuzingatia gharama, na tunajitahidi kadiri ya uwezo wetu kuhakikisha usalama wao,” alisema.

Dk. Jimmy alimalizia kwa kusema kuwa Kili MediAir inatoa huduma za uokozi kwa njia ya anga kwa kutumia helikopta na pia kwa njia ya ardhini, ili kuhakikisha kwamba wote wanaopata changamoto wanahudumiwa ipasavyo.

Kampuni hiyo inaendelea kujenga jina lake katika sekta ya uokozi na utalii, huku ikionyesha dhamira ya kuimarisha usalama wa watalii na kukuza sekta ya utalii nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles