27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kila wiki watoto 10 hulazwa MNH kwa ajali ya moto

Mtoto akiwa ameungua motoVeronica Romwald na Mwantumu Saadi, Dar es Salaam

MATUKIO ya watoto kuungua moto yamekuwa yakijitokeza na kuripotiwa mara kwa mara katika maeneo tofauti nchini.
Unaweza ukajiuliza na pengine kushangazwa kwamba inakuwaje mtoto wa mwezi mmoja anaungua ingawaje bado hajaanza hata kujongea (kusogea kutoka eneo moja kwenda jingine).
Sababu kuu inayochangia kutokea kwa hali hiyo inatajwa kuwa ni uzembe wa baadhi ya wazazi na walezi kwa kukosa umakini katika kuwalinda watoto dhidi ya hatari ya kuungua moto.
Ingawaje zipo sababu nyinginezo zinazochangia kama vile hitilafu za umeme lakini asilimia kubwa ya majeraha ya moto kwa watoto husababishwa na vitu vyenye maji maji kama vile chai, uji, maji ya moto, maziwa, vyakula, maharagwe na mafuta ya kupikia.
Uangalizi mdogo kwa watoto hasa wale wasio na ufahamu husababisha wengi wao kuungua na kufariki dunia, hali ambayo husitisha kabisa ndoto zao za baadae na wapo ambao huharibika mwonekano wao wa awali.
Daktari Bingwa wa Upasuaji na Mkuu wa Kitengo cha Majeraha ya Moto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Edwin Mrema anasema watoto nane hadi kumi wenye umri wa kati ya mwezi mmoja hadi miaka nane hufikishwa hospitalini hapo kila wiki kutibiwa majeraha yatokanayo na ajali mbalimbali za moto.
Anasema idadi hiyo imeongezeka ikilinganishwa na miaka minne iliyopita na kwamba hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na uzembe huo pamoja na ukosefu wa elimu juu ya namna ya kumkinga mtoto asikumbane na ajali hizo.
“Unakuta mzazi au mlezi anaishi ndani ya chumba kimoja na humo ndani ameweka kila kitu ikiwamo jiko, anaweza akatoka kwenda nje na labda akasahau kulizima, wakati mwingine kama ni lile linalotumia mafuta huweza kulipuka na kisha moto kuwaka na kusambaa katika vitu mbalimbali vilivyomo ndani mwishowe anakuta mtoto ameungua,” anatoa mfano.
Anasema wakati mwingine mzazi hujisahau kupooza maji aliyoyaandaa kwa ajili ya kumsafisha mtoto na hivyo hujikuta akimuunguza.
“Maji ya kumsafisha mtoto huwa yanatakiwa kuwa na joto la wastani, wakati mwingine baadhi ya wazazi hujisahau kupooza maji hayo na kwa sababu ngozi ya mtoto ni laini mno tofauti na mtu mzima hujikuta akimuunguza,” anasema.
Dk. Mrema anasema watoto wengi hasa wale ambao wameanza kuwa na fahamu kwa asilimia kubwa huungua na vitu vya majimaji na wachache kati yao huungua na moto unaotokana na hitilafu ya umeme na mengineyo.
Modester Dismas, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam ni mmoja kati ya wazazi waliolazwa katika wodi ya watoto walioungua na moto hospitalini hapo.
Alilazwa hapo baada ya mtoto wake Arial Masawe mwenye umri wa miaka sita kuunguzwa na mafuta ya moto Januari 3, mwaka huu.
Anasema siku hiyo, mtoto wake huyo alikuwa akicheza nje na wenzake, wakawa wanataka kumpiga ndipo akakimbilia jikoni kwenda kushtaki kwake ndipo akakumbwa na mkasa huo.
Anasema wakati Arial alipokimbilia jikoni yeye hakuwapo na kwa bahati mbaya alikumbana na mafuta hayo ambayo alikuwa ameyaepua muda mchache kutoka jikoni na kwamba yalikuwa bado ya moto, akatumbukia, yakamwagika na kumuunguza.
“Nilijisikia vibaya, sikutegemea kama mwanangu siku moja atakuja kuungua kwa sababu nilimlinda siku zote na mwaka huu nilitarajia ataingia darasa la kwanza,” anasema kwa huzuni.
Modester anawashukuru manesi na madaktari wa MNH kwa kumhudumia mtoto wake vizuri ambapo kwa sasa ameanza kupona majeraha yake.
Hata hivyo anaiomba Serikali kuongeza vitendea kazi pamoja na kurekebisha miundombinu ya wodi hiyo ikiwamo kuongezwa kwa vitanda kwani wakati mwingine hali huwa mbaya.
“Miundombinu si mizuri kwa sababu wakati mwingine unakuta wodi inajaa watoto wanalazwa wawili wawili kitandani na sisi wazazi tunalazimika kusimama,” anasema.
Arial kwa sasa anaendelea vizuri na anasema anatamani siku moja Mungu akimjalia awe Rais kama Jakaya Kikwete, mwanajeshi au daktari ili awasaidie watu wanaokumbwa na majanga hayo.
“Kwa kweli kumuhudumia mtoto aliyeungua inahitaji moyo wa ziada, madaktari wanajitahidi kuwasaidia pamoja na kutupa ushauri wa namna ya kuwalea hadi wapone,” anasema.
Dk. Mrema anasisitiza kwamba lazima wazazi wawe makini na kuchukua tahadhari kwa sababu idadi ya watoto wanaoungua na kufikishwa hospitalini hapo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku.
“Idadi inaongezeka na kwa mujibu wa takwimu tulizonazo hivi sasa tunahudumia kati ya majeruhi 384 hadi 480 kwa mwaka,” anasema.
Anasema kutokana na idadi hiyo kuongezeka wakati mwingine wodi maalumu ya kulaza watoto walioungua iliyopo katika jengo la watoto hospitalini hapo huwa haitoshelezi.
Anasema wodi hiyo ina uwezo wa kulaza watoto 23 pamoja na wazazi wao, lakini wakati mwingine hulazimika kulaza watoto 30 na wazazi wao.
“Tukilaza watoto 23 maana yake ni mtoto mmoja na mama yake hivyo tunakuwa na watu 46 lakini wakiwa 30 maana yake ni watu 60 kwa maana hiyo huwa tunalazimika kulaza watu wanne katika kitanda kimoja.
“Hali hii si nzuri hata kiafya lakini unakuta hatuna jinsi na tunahitaji kuwasaidia watoto wote kwa kuwapatia huduma stahiki, kwa maana hiyo tunahitaji ikibidi tuongezewe nafasi pamoja na idadi ya vitanda,” anasema.
Anasema gharama ya kumtibu mtoto mmoja aliyeungua kwa moto huwa ni kati ya Sh 30,000 hadi 50,000 na kwamba huwa wakihitaji chakula maalumu chenye lishe ya kutosha ili kumjengea kinga ya mwili itakayomsaidia kupona haraka.
Anasema Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha watoto hao wanapatiwa huduma ya matibabu bure hospitalini hapo lakini katika kipindi cha hivi karibuni wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya vitendea kazi.
“Kumhudumia mtoto mmoja ni ghali miili yao huhitaji lishe ya kutosha ili kuwajengea kinga ya mwili kwa sababu nyingi hupotea kupitia majeraha.
“Vile vile mzazi huhitajika kuwa na fedha kati ya Sh 30,000 hadi 50,000 kutokana na hali hiyo Serikali iliona ni vizuri igharimie matibabu yao lakini wakati mwingine huwa tunajikuta tukiishiwa kabisa vifaa, hivyo wazazi hulazimika kuchangia,” anasema.
Anasema Serikali pia imejitahidi kuwajengea jiko kwa ajili ya kuwaandalia chakula maalumu chenye lishe watoto hao.
“Watoto hawa huitaji chakula chenye protin nyingi pamoja na wanga… si wazazi wote wana uwezo wa kuleta chakula kile kinachotakiwa,” anasema.
Anasema hivyo wanahitaji Serikali iwawezeshe kupata vifaa, pamoja na vyakula kwa ajili ya kupika chakula hicho.
Vile vile anaiomba iwasaidie kutatua changamoto nyingine inayowakabili ya ufinyu wa nafasi ya kulaza watoto hao ili wahudumiwe.
“Lakini pia itakuwa vizuri iwapo kama watatuwezesha kupata angalau nafasi ya vipindi katika vyombo vya habari kwenye vituo vya redio na runinga ili tukaielimishe jamii namna ya kumkinga mtoto na ajali za moto kwa sababu hali si nzuri,” anasema.
Anasema pia wanahitaji vitendea kazi kwa ajili ya kuandaa chakula cha watoto hao pamoja na maziwa, unga na vinginevyo.
“Kama nilivyosema kwa sasa tunawaagiza wazazi walete chakula lakini pia tunatumia jiko kuu la hapa hospitalini kuandaa lakini ni vizuri kama tutapata la kwetu kabisa tukawahudumia vizuri watoto hawa,” anasema.
Daktari huyo anawaasa wazazi kuwa makini na ulezi wa watoto kwa sababu wakati mwingine mtoto anapoungua anaweza kuathirika ndani kwa ndani hivyo kupata madhara makubwa zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles