27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

KILA UPANDE UJIANGALIE UPYA TANZANIA YA VIWANDA


MASUALA mengi yalijidhihirisha kwenye mkutano kati ya Rais Dk. John Magufuli na wafanyabiashara nchini kwenye mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara, uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam juzi.

Kubwa ni kwamba bado kuna mambo ambayo yanatakiwa kufanywa na vyombo vya serikali kuweka mazingira wezeshi zaidi na rafiki kwa wafanyabiashara/wawekezaji kuliwezesha taifa kuwa la viwanda.

Vilevile wafanyabiashara nao bado wana safari ndefu ya kushiriki inavyotakiwa katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa.

Kama michango ya wafanyabiashara mbalimbali ilivyoonyesha, baadhi ya vyombo vya serikali vyenye mamlaka havijajiweka sawa katika utendaji kazi wao.

Bado vinafanya kazi kwa mazoea na haviendi sambamba na mabadiliko duniani ambayo yanakwenda haraka, ni ya ushindani mkubwa na yanayohitaji mbinu za kisasa zaidi.

Malalamiko hayo yalielekweza kwa vyombo kadha wa kadha vya serikali  kama vile Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),   Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).

Hata hivyo, taasisi iliyokabiliwa na malalamiko mengi na makubwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo ina uuhimu wa pekee katika maendeleo ya viwanda nchini.

TRA ililalamikiwa hasa kuhusu njia na utaratibu wake wa kutoza kodi, viwango vya kodi na aina ya kodi – vyote hivyo vikielezwa kuwa siyo rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji, ambao ndiyo wanatakiwa watoe mchango mkubwa katika azma ya Tanzania ya Viwanda.

Hiyo ni kwa kuzingatia kwamba kodi ndiyo msingi wa maendeleo.

Wafanyabiashara hao walilalamikia ukadiriaji wa kodi ambao unaweka viwango vya juu mno, hali ambayo inaweza kuwa inachangia ukwepaji kulipa kodi.

Tatizo jingine lililoelezwa ni aina nyingi za kodi, jambo ambalo pia linakatisha tamaa ulipaji kodi inavyotakiwa.

Lakini, wafanyabiashara na wawekezaji nao walikosolewa kwa kutokuwa na uwazi unaotakiwa, kwa maneno mengine kwa udanganyifu.

Rais Magufuli, alitoa mfano wa kiwanda kimoja ambacho kimeagiza sukari wakati hakijakamilika, yaani kiwanda hewa!

Mjadala huo wa juzi unadhihirisha wazi kwamba kila upande unatakiwa kuchukua hatua za makusudi kuleta uelewano unaotakiwa katika ujenzi wa nchi.

Ni muhimu kwa kila upande – vyombo vya serikali kwa upande mmoja na wafanyabiashara na wawekezaji kwa upande mwingine – kuangalia upungufu na udhaifu wake na kutafuta njia ya kufanya marekebisho muhimu kwa ajili ya kufikia malengo yanayotarajiwa ya Tanzania ya Viwanda.

Matumaini yetu ni kwamba yaliyozungumzwa kwenye kikao hicho yatafanyiwa kazi na kutekelezwa kwa utashi na umakini mkubwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho katika taifa hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles