27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Kikwete, Kagame ana kwa ana

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Rwanda, Paul Kagame wamekutana ana kwa ana nchini Kenya.
Hatua hiyo imekuja huku ikiwa imepita miaka miwili tangu Tanzania na Rwanda ziingie katika vita ya maneno hasa baada ya Rais Kikwete kumshauri Kagame kukaa meza moja na kikundi cha waasi cha FDLR cha nchini humo.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa Rwanda wakati akizungumza katika kikao cha Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, ambao ulikuwa ukijadili suala la amani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na ukanda wa Maziwa Makuu.
Ushauri huo pia uliwagusa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), ambao aliwataka kufanya mazungumzo na waasi wanaopingana na serikali zao.
Hata hivyo hali ilionekana kuwa tofauti kwa viongozi hapo juzi katika mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika Jijini Nairobi nchini Kenya, ambapo Rais Kikwete alikabidhi uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika mkutano huo ambao ulikuwa ukiongozwa na Rais Kikwete, muda wote Kagame alikuwa ni mwenye tabasamu dhidi ya kiongozi huyo wa Tanzania.
Wakati mkutano huo wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukiwa unaendelea Rais Kagame alinyanyuka katika kiti chake na kwenda kumwomba udhuru Mwenyekiti wa EAC, Rais Jakaya Kikwete ili aweze kuondoka kabla ya kumalizika kwa mkutano wa 16 wa kawaida wa wakuu wa nchi za jumuiya hiyo.
Wakati viongozi hao wakiteta meza kuu, hali hiyo iliamsha minong’ono miongoni mwa wajumbe wa mkutano huo ambao walikuwa wakijadiliana na hata kuona tukio hilo ni la kihistoria kwa viongozi hao.
Kwa muda wa miaka miwili sasa uhusiano wa Tanzania na Rwanda umekuwa ukipita katika wakati mgumu na mtikisiko hasa baada ya Rais Kikwete kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao na kwamba hilo lilidhihirika katika kauli zilizokuwa zinatolewa na viongozi wa Serikali ya Rwanda.
Katika kile kilinachoelezwa kutafuta suluhu ya mgogoro huo Septemba 5, mwaka 2013, Rais Kikwete na Paul Kaganme wa Rwanda walikutanishwa na kukaa chumba kimoja kuzungumza kwa saa nzima huko kando mwa mkutano wa maziwa makuu uliofanyika Kampala nchini Uganda lakini hakuna waandishi walioruhusiwa kuingia katika mkutano huo.
Pamoja na kukutana kwa viongozi hao haikujulikana nini kilichozungumzwa kati ya viongozi hao, jambao ambalo lilitishia kusambaratika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hali hiyo iliibuka hasa baada ya viongozi wa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda kukutana kila mara kwa kile kilichokuwa kinaelezwa kuwa ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo kwa kutuimia Bandari ya Mombasa, Kenya.
Akizungumza katika hotuba yake ya Agosti 3, mwaka jana ambayo hutoa kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema ushauri aliutoa kwa Rwanda ulikuwa na nia njema.
“Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa, kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike,”
“Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali ya Congo , Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais Kagame hakusema chochote pale mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.
Rais Kikwete alisisitiza. “Kwa upande wangu sijasema lolote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu.
“Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha, sijafanya hivyo kwa sababu sioni faida yake,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kagame alitoa lugha zisizostahili dhidi ya Rais Kikwete katika sherehe ya kuhitimu mafunzo ya kijeshi ya maofisa 45 wa jeshi lake Julai mwaka huu, ambapo alisema ushauri wa kufanya mazungumzo na waasi wa FDLR ni ujinga na haupo katika historia ya Wanyarwanda.
“Nilinyamaza kimya kwa sababu sikupenda kusikiliza ushauri kuhusu FDLR, kwa sababu nafikiri ni upuuzi ulioambatana na ujinga. Hatuwezi kuacha maisha yetu kama Wanyarwanda tunavyoishi sasa. Ushauri wa Kikwete ni sawa na kucheza na makaburi ya watu wengi ambao ni ndugu zetu,” alisema Kagame.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles