29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

KIKWETE AONGOZA MAZISHI MKE WA KINGUNGE

Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ameongoza waombelezaji katika mazishi ya mke wa mwanasiasa mkongwe nchini, Peras Kingunge Ngombale Mwiru.

Kikwete aliwaongoza viongozi mbalimbali wa wakiwemo wa CCM na upinzani katika mazishiyaliyofanyika jana katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Rais huyo mstaafu alipangwa kwenye ratiba ya kuwa moja ya wazungumzaji kwenye msiba huo nyumbani, lakini hakuonekana na baadaye aliungana na waombolezaji wengine makaburini.

Hata hivyo juzi alifika nyumbani kwa Kingunge kuomboleza  msiba huo.

Awali mzee Kingunge alilazimika kuaga mwili wa mkewe Peras akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.

Akizungumza kabla ya kuaga mwili wa mama yao mtoto wa mwanasiasa huyo, Kinje Ngombale Mwiru, alisema familia yao ipo katika wakati mgumu na baba yake atarudishwe tena hospitali ya Taifa Muhimbili leo kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

Viongozi wengine waliohudhuria msiba huo ni Spika Mstaafu Anne Makinda, Mawaziri Wakuu wastaafu Edward Lowassa, Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye.

Wengine ni Mbunge wa Kuteuliwa, Abdallah Bulembo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wabunge mbalimbali ambao walijitokeza kuaga mwili wa mke wa Kingunge.

Kinje alisema mama yake alifariki dunia Januari 4, mwaka huu  katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na ugonjwa wa kupooza mwili.

Aliwashukuru viongozi wote akiwamo Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Benjamin Mkapa  kutokana na ukaribu wao katika kipindi chote cha msiba.

“Familia tuna kipindi kigumu kuliko na haijawahi kutokea msiba wa mama umetukuta baba akiwa na hali mbaya na ameletwa kwa uangalizi wa madaktari na atarudishwa hospitalini Muhimbili kesho (leo) siwezi kuongea mengi naomba kipindi hiki kigumu kipite,” alisema Kinje.

Kwa upande wake mwakilishi wa wananchi kutoka Kilwa mkoani Lindi, Said Manolo alisema marehemu Peras alikuwa ni mwanamke shujaa aliyeacha alama.

“Kukaa na mume maskini wa kujitakia si jambo rahisi Kingunge amekuwa akiishi maisha ya kimaskini kwa ajili ya uzalendo wa nchi kuwa na mwanamke wa kuishi naye kwa upendo inahitaji uvumilivu,” alisema Manolo.

Alisema pamoja na kuwa mama wa familia Peras alihakikisha anatumia muda wake kuwezesha wananchi wa Kilwa na kuwa kichocheo cha maendeleo hususani katika elimu na alifanikisha ujenzi wa shule.

Naye mwakilishi wa kituo cha kulea watoto wanaoishi katika  mazingira hatarishi Kigamboni New hope Famili Group, Omary Kombe alisema mama huyo alikuwa ni mlezi na alifanikisha makazi ya watoto hao na kupata huduma zote muhimu ikiwemo elimu.

“Alianza kwa kuwasaidia kutafuta eneo la kupanga na baadaye makazi ya kudumu Kigamboni na wapo baadhi yao wamefanikiwa hadi kufikia elimu ya juu,” alisema.

Alisema muda wote wa malezi kwa watoto hao alihakikisha anakaa nao na kuwasisitiza elimu huku akiwataka walezi kubeba silaha ya upendo katika kufanikisha ndoto za watoto hao waliotolewa mitaani na kutelekezwa hali iliyosababidha kukosa malezi bora.

Marehemu Peras aliagwa nyumbani kwake Vicktoria, alisaliwa katika kanisa la St. Peter na kuzikwa makaburi ya Kinondoni jijini Dare es Salaam, alizaliwa Machi 1941 ameacha mume, mtoto mmoja na wajukuu wanne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles