Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla amesema kuwa biashara ya usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi haitafanyika kwenye uongozi wake.
Akizungumza bungeni leo Mei 24, wakati akihitimisha hotuba ya bajeti yake katika mwaka wa fedha 2019/20 na kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge ikiwemo suala la usafirishaji wanyamapori hai amesema biashara hiyo ilishafungwa tangu alipochaguliwa kuwa waziri wa wizara hiyo.
”Biashara ya wanyamapori hai haitafanyika nikiwa kama Waziri wa Maliasili na Utalii kwakuwa suala hilo lilishafungwa.
“Wizara imeamua kufunga mlango wa biashara hii, hata awe chawa au kunguni, atakayetaka kufuga afuge ili watanzania waende kwenye Zoo yake kuwatazama wanyama hao,” amesema Kingwangalla.
Ameongeza kuwa kuhusu suala la vipepeo kusafirishwa kwenda nje ya nchi wananchi ambao walikuwa wamechukuliwa vipepeo vyao ili viakuzwe watarudishiwa fedha zao na serikali.
Wakati huo huo Waziri huyo amesema kuwa Rais John Magufuli ameridhia hifadhi tatu mpya kuingizwa katika orodha ya Hifadhi za Taifa.
“Hapa nina hati kutoka kwa Rais, ameridhia hifadhi mpya tatu kuingia katika orodha ya hifadhi za taifa,” amesema Kigwangalla
Amezitaja hifadhi hizo mpya kuwa ni hifadhi ya Burigi, Chato, hifadhi ya Rumanyika, Karagwe na Ibanda, Kyerwa.