Waziri awataka watumishi wa umma kupambana na rushwa

0
896
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) leo Mei 24, wengine pichani ni viongozi wa TUGHE na RAAWU.

Awamu ya Tatu ya Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa (2017-2022) ina mtazamo mpya unaolenga kuhakikisha rushwa inaondolewa nchini kwa kutumia mbinu mpya na zinazotekelezeka kwa kuweka mkazo katika sekta zenye mazingira shawishi ya rushwa.

Utekelezaji wa mkakati huo unalenga kupunguza na kudhibiti rushwa katika sekta muhimu ambazo ni pamoja na manunuzi ya umma, ukusanyaji wa mapato, utoaji wa haki, maliasili na utalii, madini, nishati, mafuta na gesi, afya, elimu na ardhi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, leo Mei 24, amekemea na kuwataka watumishi kupambana na rushwa katika sehemu zao za kazi.

 “Wizara inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake, kutoa huduma kwa umma ikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha na rasilimali watu, hali hii inasababisha kutofikiwa kwa malengo.

“Niwahakikishie kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto hizi na yeyote atakayejihusisha na kubainika kupokea au kutoa rushwa hatua stahiki  zitachukuliwa dhidi yake, ni matumaini yangu kuwa mkiwa kama wataalamu mtatumia uwezo wenu katika kuibua mikakati itayosaidia kuwezesha kilimo kuwa chenye tija na cha kibiashara” amesema Japhet.

Aidha Waziri Japhet amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano ina dhamira ya dhati ya kuondoa uzembe na ubadhirifu miongoni mwa watumishi wa umma na hivyo mtumishi anaruhusiwa kudai haki zake za msingi kwa kuzingatia Kanuni, Sheria  na Taratibu za utumishi wa umma.

Ameweka bayana kuwa serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya mwajiri na mtumishi kwani pasipokuwa na ushirikiano wa pande hizo mbili, ni vigumu taasisi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Ili kuweza kutafsiri dhana hiI ni muhimu pande zote mbili kutambua haki na wajibu katika utekelezaji wa majukumu ya kazi, kumekuwa na utamaduni wa baadhi ya watumishi kudai haki bila kutimiza wajibu wao kwa mwajiri,” amesema Waziri huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here