25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

KIGOGO ALIYEUZA AIRTEL HUYU HAPA


Na AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM -

SAKATA la uuzwaji wa Kampuni ya Simu ya Airtel iliyokuwa ikiendeshwa kwa ubia na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) limezidi kuchukua sura mpya, huku kigogo aliyeuza kampuni hiyo akiwekwa hadharani.

Kutokana na hali hiyo TTCL imetoa msimamo ikiwataka waliouza kampuni hiyo kwa ‘dili’ kuirejesha mikononi mwao kwa hiari badala ya kusubiri nguvu itumike.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL,  Omary Nundu ameitaka Airtel kukabidhi mali za kampuni hiyo kwa TTCL ambayo ndiyo wamiliki halali kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Nundu ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya awamu ya nne, ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kumtaka Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango, kufuatilia kwa karibu umiliki wa kampuni hiyo kabla ya mwaka huu kuisha kwa kuwa taarifa alizonazo kampuni hiyo ni mali ya TTCL.

Alisema Kampuni hiyo ya Airtel ambayo ilisajiliwa Novemba 3, 1998 na uongozi wa TTCL kwa mtaji wa Sh bilioni 200 kwa jina la Cellnet iliuzwa kijanja na waliokuwa viongozi wa bodi ya TTCL.

Alisema kupatikana kwa kampuni hiyo ambayo ilikuwa chini ya TTCL kulitokana na kuvunjwa na kugawanywa Shirika la Posta na TTCL  Desemba 1993.

Alisema baada ya mgawanyiko huo TTCL ikawa kampuni ya Serikali ikiwa na mtaji wa Sh bilioni 200.

“Julai 21,1999 baada ya miaka sita thamani ya hisa za TTCL zikapanda kutoka bilioni 200 mpaka bilioni 600, baadae Februari 23, 2001 likaja wazo la kubinafsishwa TTCL akajitokeza mtu anaitwa MSI Cellular Investment ,” alisema Nundu.

Alisema mwekezaji huyo alikuja kwa ajili ya kuwekeza katika kampuni ya TTCL katika upande wa simu za mkononi.

Alisema katika uwekezaji huo walikubali kutoa  fedha kwa ajili ya  kununulia  hisa ambazo zilikuwa Dola za Marekani milioni 120 ambazo ni sawa na hisa 1,028,665 kati ya  6,000,000.

“Kwa  hesabu hii hawa watu hisa zao ni sawa na  asilimia 17.14 si asilimia 35 kama inavyoelezwa, lakini kote wanataja kampuni ina hisa asilimia 35, hili peke yake ni tatizo,” alisema Nundu.

Alisema pamoja na hayo katika mchakato huo ulifanyika ujanjaujanja ambapo mwekezaji huyo  hakulipa fedha ambazo aliahidi zipatazo Dola milioni 120, badala yake walilipa Dola milioni 65, huku wakiendelea kuhesabu idadi sawa ya hisa na zile za awali.

Alisema siku hiyo hiyo Serikali ikachukua hisa  20,600,650 sawa na asilimia 25 na mwingine akapewa 14,050,000.

“Hapo sasa Serikali ndo alikuwa na hisa kubwa kwenye Celtel, watu hao wakachukua hisa nyingine 10,250,000 wakampa mwekezaji ambaye hakujulikana hiyo ndio ikapindua vitabu vya mahesabu, ikawa mwekezaji anahisa 24,626,000,” alisema.

Nundu alisema baada ya hapo Celtel ikawa na asilimia 60 na serikali asilimia arobaini na kusababisha bodi ya wadhamini iwe na watu wengi kutoka katika kampuni ya Celtel.

Alisema awali kabla ya yote kampuni hiyo ilianza kumilikiwa na mtu asiyejulikana ambaye alikuwa na hisa moja wakati hisa 999 zikiwa za TTCL.

Alisema baada ya muda  hisa hiyo moja akapewa mzungu aliyejulikana kwa jina la David Banfod ambaye alizishika kwa niaba ya mtu kabla ya kuzikabidhi kwa Mtanzania (jina linahifadhiwa kutokana na maadili).

“Baadae hisa hizo alikabidhiwa Mtanzania kwa bahati nzuri ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya Kampuni za Airtel na TTCL (jina tunalo),” alisema Nundu.

Alisema baada ya kukabidhiwa hisa hizo mwenyekiti huyo aliitisha kikao cha wajumbe wa bodi ambapo kati ya wajumbe tisa walihudhuria watano Watanzania wakiwa wanne na raia mmoja wa kigeni.

Alisema pamoja na kwamba bodi hiyo ilikuwa na wajumbe tisa lakini kikao hicho cha kuiuza kampuni ya Cellnet kilichokutana Agosti 5, 2005  kilikaliwa na wajumbe watano kikiongozwa na mwenyekiti ambaye alibariki kugawanywa kwa hisa zote na kuipatia  TTCL hisa moja na hisa 99  wakapewa Celtel.

Alisema kupitia kikao hicho wajumbe hao walibadilisha mawazo  na kuinyang’anya TTCL hisa ambayo iliwapa hivyo kuifanya Celtel kumiliki kampuni hiyo kwa asilimia mia moja kwa gharama ya Sh milioni 50.

Alisema badaaye kikao hicho pia kiliamua kuipa Serikali  hisa asilimia 65 huku TTCL ikiwa haijapewa kitu  na Celtel ikapewa asilimia 35.

“Kutokana na mgwanyo huo  gharama za hisa za serikali zikawa Sh milioni 26.6  na wengine wakawa wamechukua hisa za Sh milioni 14.3. Baada ya muda mwenyekiti kwa nafasi yake akachukua hisa nyingine za Sh milioni 10 na kumpatia mwekezaji,” alisema.

Alisema pamoja na mlolongo huo wote Juni 23 mwaka huu kampuni ya TTCL iliwataka Kampuni ya Bhart Airtel wajitoe kutoka TTCL, hivyo iliwalipa hisa milioni 14 kama wamiliki wa Airtel ambazo ni sawa na Sh bilioni 40.

“Katika hisa hizo walichukua Dola milioni 40 kuongeza mtaji wa Celtel wa kuwanyang’anya fedha zote TTCL na baadae kuamua kuwakopesha tena tena dola milioni 28 nje ya bilioni  40, hizo fedha ziliwekewa riba ya asilimia nane, mpaka leo deni limefika Sh bilioni 76.6,”alisema Nundu.

Alisema  mambo hayo yote wameyapata baada ya kuifanyia uchunguzi wa usajili na ubinafsishwaji wa kampuni hiyo wakati wakiwa wanatafuta mtu wakufanya naye kazi.

“Sisi tulitafuta tufanye biashara vizuri na wenzetu tukaanza kuchimba ndo tukayaona yote haya tukasema hapa lazima twende tujue mbivu na mbichi kama kuna kulipana tutalipana vipi na tunataka kwenda kistaarabu tu.

“Kwa sababu kila ukichimba unakuta mambo mazito zaidi, tumeomba Serikali ilichukue jambo hili sisi interest ikiwezekana ile kampuni ya Celtel turudishiwe,”alisema Nundu.

Alisema kampuni ilipata mlolongo wa hasara pale ilipolipwa Dola Milioni 65 ya hisa badala ya Dola milioni 120.

“Kampuni hii ilisajiliwa na TTCL, masafa ni ya TTTCL mali zilizotumika kuanzishia kampuni  ni za TTCL hivyo hawawezi kusema ni kampuni yao isipokuwa kipindi hicho kulikuwa na viongozi wasio waaminifu ambao siwezi kuwataja kwakuwa wanajijua wakashiriki kuipora kampuni na kuwapa wageni sasa ni vema wakairudisha kistaraabu,” alisema Nundu.

Alisema mchakato uliotumikwa kuipata ni Celtel ni haramu na mpaka sasa ipo kiharamu hivyo ni lazima irudishwe na si kuwapa hisa.

Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo kwa Msajili wa Makampuni, inaonyesha kuwa umekuwa ukibalidika tajngu ilipoanzishwa Kampuni ya Celtel Tanzania mwaka 2001 hadi Mei 2005.

Kwa wakati huo kampuni hiyo ilikuwa na wakurugenzi wazawa watatu ambapo hadi kufikia Novemba mwaka 2005 aliongezwa mzawa mwingine ambaye kwa sasa ni mbunge mstaafu.

Hata hivyo kati ya wakurugenzi hao pia yupo Mtanzania mmoja (jina tunalo) ambaye alipata kufanya kazi  katika taasisi nyeti serikalini.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, alisema  menejimenti na wafanyakazi wa kampuni hiyo wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na bodi hiyo  ili kuhakikisha haki ya Watanzania inapatikana baada ya kudhulumiwa na wajanja wachache.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles