26 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 8, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Kifo cha Mkapa

ANDREW MSECHU– DAR ES SALAAM

HATIMAYE, familia ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa imetaja sababu zilizosababisha kifo cha rais huyo, aliyefariki dunia usiku wa Alhamisi Julai 23, 2020.

Sababu hizo zilitajwa na msemaji wa familia ya Mkapa, William Erio, alisema amelazimika kuzitaja hadharani, baada ya kuwepo kwa baadhi ya watu ambao wameanza kutoa sababu zisizo halisi za kifo chake.

Akizungumza jana katika Misa ya Kitaifa iliyoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Erio alisema sababu ya kifo cha Rais mstaafu Mkapa ni kupatwa na mshtuko wa moyo au kama inavyoitwa kitaalamu “Cardiac Arrest”.

“Ninadhani ni vizuri kulisema hivyo kwa sababu kumeanza kuwa na maneno maneno na maelezo mengine ya kila mtu akijifanya ni nabii na mwelewa katika mitandao ya kijamii na maeneo mengine, niwaombe na kuwasihi Watanzania wenzangu tumuenzi mzee wetu aliyetangulia mbele ya haki kwa kuhesimu ukweli huo, kuwa hicho ndicho kilichosababisha kifo chake,” alisema.

Akielezea zaidi mazingira ya kifo chake, Erio alisema Mkapa alipelekwa hospitali Jumatano ya wiki iliyopita, Julai 22 baada ya kusema kuwa hajisikii vizuri.

Msemaji huyo wa familia, alisema ameamua kutumia fursa ya Ibada kueleza kwamba Mkapa alikuwa hajisikii vizuri na baada ya kwenda hospitali alichukuliwa vipimo na kuonekana kuwa ana ugonjwa wa malaria. 

“Alianza matibabu na akalazwa siku ya Jumatano. Siku ya Alhamisi mchana aliendelea vizuri na mimi binafsi nilikuwa naye hadi kwenye saa mbili usiku, akanipa maagizo ya kumpelekea Baba Askofu Nzigilwa kwamba alimkubalia kushiriki katika shughuli yake ya kuagwa jana (Jumamosi) lakini hatoweza kuhudhuria.

“Aliniambia nimfikishie salamu zake na bahasha yake. Baada ya hapo aliendelea kufuatilia taarifa ya habari kwa sababu kwanza alikuwa anaangalia maonesho ya mubashara kuhusu chaguzi zilizokuwa zinaendelea kwa wanaogombea ubunge wa Viti Maalumu kwa wanawake katika Chama cha Mapinduzi.

“Alisikiliza taarifa ya habari tukaagana naye na nikaenda kutekeleza kile alichotuagiza tukiwa na wanafamilia wengine na baada ya hapo taarifa iliyopo ni kwamba, baada ya kusikiliza taarifa ya habari aliinuka akitaka kutoka lakini alivyoinuka, alikaa akainamisha kichwa na hadi walipokuja kumpima ikawa amethibitika kuwa ameshafariki,” alisema.

Erio alisema Mkapa amepigana vita vilivyo vizuri, mwendo ameumaliza, imani ameilinda hivyo ni vyema apumzike kwa amani.

Hata hivyo, msemaji huyo wa familia alisema wanatoa shukrani za dhati kwa Seriakli na viongozi wote kwa jinsi ambavyo wamekuwa karibu na familia na kwa namna walivyoshughulikia msiba huo tangu Mkapa, alipotwaliwa Alhamisi usiku.

Alisema wanashukuru hata kwa yale yanayoendelea hadi safari ya kumpumzisha inayoendelea hadi atakapopumzishwa siku ya Jumatano wiki hii.

Aliishukuru pia Serikali kwa uamuzi wa kuruhusu ibada maalumu na wananchi kuanza kumuaga jana, pia anashukuru kwa namna ambavyo imeamuliwa kwamba aanze kuagwa kwa njia hiyo ya Misa Takatifu jana na kuwashukuru maaskofu kwa kukubali kwa kuwa hakuna njia bora ambayo wangeweza kuifanya tofauti na hiyo.

NGALAREKUMTWA ATOA NENO

Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa ambaye aliongoza misa hiyo maalumu jana, Tarcisius Ngalalekumtwa alisema imefanyika wakati Neno la Siku lililoongoza likisema kuwa Omba Utakacho Nitakupa, ikiwa ni nafasi ambayo Mungu Mwenyezi anaongea katika lugha ambayo anapenda ieleweke.

Askofu Ngalalekumtwa ambaye aliongoza jopo la maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), alisema neno hilo, linakumbusha namna Suleiman mwana wa Mfalme Daudi, ambaye baada ya kuwa baba yake, Daudi amerudi kwa baba zake, yaani kufariki dunia, alikalia kiti cha kifalme, akitawala kipindi cha amani na utulivu pande zote katika ufalme. 

Alisema Mwenyezi Mungu alimuuliza iwapo anatamani apewe kitu chochote akipendacho kama zawadi? Naye akiangalia mahitaji ya utawala na uongozi aliokabidhiwa aliomba apewe moyo wa adili, hivyo Mungu akamjazia moyo wa hekima na wa akili zisizokuwa za kawaida.

Alisema kutokana na chaguo lake, Sulaiman alisikika hata na falme za mbali hadi huko Uhabeshi, yaani Ethiopia ya sasa na anaendelea kukumbukwa kuwa ndiye aliyemjengea Mungu Mwenye Enzi Hekalu linalosifika sana huko Yerusalemu.

Alisema Watanznaia ni wana wa Ufalme wa Mungu naye ndiye mwenye kauli juu ya maisha ya kila mmoja na anayetawala maisha ya watu wote, ili kila mmoja afike mwisho wenye Heri na wenye Baraka.

Askofu Ngalalekumtwa alisema hekima kama aliyoiomba Suleiman ni thamani na ni lulu kuliko zote na hivyo kuumbwa kwa ajili ya umilele pamoja naye ndiyo zawadi ya kipekee.

Alisema kama leo hii kwa nafasi hii neno hilo la Omba Utakalo Nikupe lingeelekezwa kwa kila mmoja, kwamba aombe apewe nini orodha ingekuwa ndefu ya kuchosha hata kwa maombo ambayo huenda yangekuwa mazuri tu kwa ajili binafsi na kwa ajili ya wengine.

Alisema swali ni kwamba hicho unachoomba kwa bwana kinakupeleka kwenye kwenye lengo la uumbaji? Na hapo ndipo ..

Alisema Sala Kuu ya Jumapili ya jana inaungama kwamba pasipo Mungu hakuna lililo thabiti wala Takatifu hivyo sala inaomba huruma ya Mungu ili waamini wajaliwe kutumia vyema mambo ya dunia huku wakiambatana nay a milele.

“Tukitumia vyema mambo ya dunia huku tukitazama ya milele, hapo ndipo akili ilipo, hiyo ndiyo hekima na ndiyo mpango kazi wenye tija kwamba umejaliwa maisha na kuyaishi kwa Utukufu wa Mungu, si kwa manufaa binafsi bali pia ya wengine

“Mzee wetu Mkapa alizoea kuhudhuria na kushiriki maadhimisho ya Dominika na leo anahudhurishwa kwa njia ya maombezi yetu, hivyo tupeleke maombi, dua na maombolezo yetu yaende kwa baba wa milele, kusudi mzee wetu huyu ambaye tuna imani na matumaini makubwa juu ya huruma ya mungu na upendo wake kuwa amjalie kukaribishwa kwenye mji wa wenye haki aweze kukumbatiwa kifuani pa Ibrahim baba yetu wa imani, kipenzi wa Mungu.

“Tuendelee kutafakari na kuadhimisha mafumbo ambayo lengo ni kutufukisha katika kiti cha enzi, cha huruma na cha upendo,” alisema askofu huyo.

Askofu Ngalarekumtwa aliyewakilisha TEC alishirikiana na Askofu Agapitus Ndorobo wa Jimbo la Mahenge, Askofu Anthony Banzi wa Jimbo la Tanga na Askofu Alfred Maruma wa Jimbo la Njombe

Akizungumza kwa niaba ya TEC, Askofu Ndorobo wa Jimbo la Mahenge, alisema msiba wa Mkapa ni wa taifa pamoja na Kanisa la Tanzania na la Ulimwengu kwa kuwa alikuwa Baba mwema na kwa ushahidi, ni yeye ambaye amekaa pamoja naye pamoja na familia.

Alisema ushahidi huo unakwenda pia kwa wengine waliowahi kuwa karibu naye, akiwemo Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli na wote walioshirikiana naye kwa nyakati zote hadi ilipofika habari kwamba hayupo tena, ambapo kila mmoja ana ushuhuda wake.

Alisema Mkapa alipewa haki ya kuwa na Kristo na kwamba wanatumaini watafufuka pamoja naye kwa kuwa ni Baba mwema aliyewapenda Watanzania wote na Afrika na ni Baba ambaye alijua kusikiliza shida ya kila mmoja na hicho ndicho kitakosekana kwa muda mrefu.

“Ni mtu aliyesikiliza shida ya kila mmoja na aliweza kuwasaidia kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake, na hivyo tunaona hilo litakuwa pungufu ambalo tutaendelea kulipata hadi Bwana atakapotujaziliza,” alisema Askofu Ndorobo.

 Alisema yeye binafsi alikutana naye kwa mara ya kwanza akiwa Padri akifanya kazi Kurasini wakati wa ujio wa Baba Mtakatifu John Paul II, ambapo aliona utendaji wake na juhudi yake katika kuwahimiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles