JOSEPH NA MASHIRIKA YA HABARI,
MWANAMUME mmoja mburudishaji amewashangaza wengi kwa uwezo wake wa kugongelea misumari kwenye mbao akitumia kichwa chake mithiri ya nyundo.
Video na picha zilizowekwa kwenye tovuti ya asasi ya rekodi za dunia cha Guinness, zilionyesha umati ukishangazwa na jamaa huyo mkazi wa Boston nchini Marekani, John Ferraro.
Maelezo ya wataalamu wa afya yanasema fuvu lake la kichwa ni karibu mara tatu kwa uzito ikilinganishwa na binadamu wa kawaida.
Katika moja ya matukio alishuhudiwa akigongelea misumari 38 ya inchi tisa katika mbao kwa dakika mbili tu, akilenga kuvunja rekodi ya dunia kuhusu misumari mingi zaidi iliyogongelewa kwa kutumia kichwa kwa dakika chache zaidi.
Inasemekana mbali na kipaji hicho kisicho cha kawaida, jamaa huyu ni mwanamieleka.
Ferraro si tu ana uwezo wa kupigilia misumari kwa kichwa bali pia anaweza kustahimili tofali zito kuvunjwa kichwani mwake kwa kutumia mipira mizito ya mchezo wa kuviringisha tufe (bowling).
Kana kwamba hiyo haitoshi, Ferraro huruhusu watu kuvunja matofali katika kichwa chake.
Ferraro ambaye ni mkazi wa Boston mara ya kwanza alijigundua kuwa na kipaji akiwa mvulana wakati alipojigonga kichwa kwa kishindo kikubwa katika mlango wao mzito uliotokana na mwaloni wakati akimkimbiza kaka yake.
Mwenyewe anasema: “Nikiwa bado mdogo wakati namkimbiza kaka yangu ulipotokea ugomvi, alifunga mlango kwa nyuma ili kunikwepa. Kwa bahati mbaya sikuwa na hili wala lile nilijikuta nikiugonga kwa kishindo kwa kichwa kwa bahati mbaya na kusababisha ulegee bawaba zake na fremu zake.
“Wakati nilipokuwa mkubwa nilitumia kila aina ya mbinu kukuza kipaji changu kupitia usomaji wa vitabu vya zamani na makala kisha kufanyia mazoezi niliyojifunza pamoja na mbinu za mafunzo.
“Maandalizi, mafunzo na dhamira ya kufikia lengo viliniwezesha kujiamini juu ya uwezo wangu. Wakati muda wa kufanya onesho huwa nafanya kweli na kutoa burudani itakiwayo.
“Wakati wa maonesho haya ya kugongelea misumari, kupasua tofali kichwani kwa kutumia mpira mzito, 'maumivu huwa si kitu hata kidogo, nguvu ya akili na moyo ndivyo vinavyoniongoza. Inapobidi kutoka damu kwa ajili ya sanaa niioneshayo, hutoka damu. Ni kitu cha kukufanya uweze kujiamini mwenyewe,” anasema.
Anasema kuwa unachotakiwa ni kujiamini kwamba una nguvu na kitu kitapinda, kuharibika au kuvunjika.
Kitabibu, fuu la mburudishaji huyo ni karibu mara tatu ya wastani wa kawaida wa binadamu, likipimika kwa unene wa milimita 16 kulinganisha na wastani wa milimita 6.5 wa kawaida.
Ferraro alifanyiwa vipimo vya scan ya MRI katika shule ya Utabibu Harvard mjini Boston na wataalamu wa nyolojia na maradhi ya ubongo.
Ilifichua kwamba hana tatizo lolote la kiafya katika fuu lake na kumfanya Ferraro aamini ni zawadi toka kwa Muumba.
Kupitia uchunguzi wa kina wa x-ray, wataalamu wa afya walibainisha kuwa ubongo wa mburudishaji huyo uko vizuri licha ya kukumbana na vipondo karibu kila siku wakati akifanya maonesho.
Anasema: “Kamwe sijawahi kuumia au kupata athari kichwani au ubongoni kutokana na nguvu kubwa ya vipondo kichwani. Madaktari wanashangazwa kwamba niko vile vile kiafya bila kuumia kutokana na shughuli pevu ya gongagonga inayokabili kichwa.
Farraro kwa sasa ameshaweka rekodi mbili katika Kitabu cha Rekodi za Dunia, Guinness World Records moja ikihusu kuvunjwa kwa tofali kwa kutumia mpira mzito wa bowling wenye uzito wa lb 16 sawa na kilo saba kutokea umbali wa futi 10 juu ya kichwa chake. Nyingine ya kupigilia msumari katika mbao kwa kutumia kichwa.