Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wenzake wanane wa chama hicho, imetua kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Kesi hiyo iliyokuwa ikitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina leo imepangwa rasmi kusikilizwa mbele ya Hakimu Simba baada ya hakimu aliyekuwa akiisikiliza kuanzia mwanzo, Wibard Mashauri kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uchochezi ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.
Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka jana jijini Dar es Salaam.