KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
UPANDE wa mashtaka katika kesi ya kukaidi amri ya kutawanyika eneo la gezani inayowamkabili wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Halima Mdee, inatarajia kuanza kusikilizwa Agosti 28 mwaka huu.
Hayo yalibainika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipoletwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, kwa ajili ya kusomwa hoja za awali lakini haikuweza kuendelea.
Wakili wa Serikali Faraja Nguka, alidai hataweza kusoma hoja za awali kwa kuwa hajalipitia jalada la kesi hiyo hivyo ameiomba mahakama impe muda alipitie kwanza.
Hakimu alikubali ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 28 mwaka huu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda mjini, Ester Bulaya pamoja na Mbunge wa viti maalum mkoa wa Singida Jesca Kishoa.
Wengine ni Meya wa Ubungo Boniface Jacob, Diwani wa Tabata Patrick Assenga, Mshewa Karua, Khadija Mwago, Pendo Mwasomola, Cesilia Michael, Happy Abdallah, Stephen Kitomali na Paulo Makali.
Wengine ni Ahumani Hassan, Omary Milodo, Emmanuel Ignastemu, Stephen Kitomali, Hamis Yusuph, Juma Juma, Mustafa Lada, Emmanuel Zakaria na Steven Ezekiel.
Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Machi 13, 2020 katika gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Mashtaka mengine ni kufanya mkusanyiko usio halali, kuharibu mali, kutoa lugha ya kuudhi na kifanya shambulio kwa askari magereza.