26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Kero 22 kati ya 25 za Muungano zapatiwa ufumbuzi

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

OFISI ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imesema inaendelea kutafuta ufumbuzi wa kutatua kero tatu za Muungano zilizobaki huku hadi sasa kero 22 zikiwa tayari zimepatiwa ufumbuzi kati ya 25 zilizoibuliwa.

Kero hizo ambazo hazijapatiwa ufumbuzi ni Sekta ya Fedha, Mgawanyo wa Fedha kutoka Benki Kuu (BoT), Usafiri wa vyombo vya moto na uletaji wa sukari kutoka katika kiwanda cha Kihonda Zanzibar kuja Tanzania Bara.

Hayo yameelezwa leo Jumanne, Marchi 26,2024 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Seleman Jafo wakati akielezea mafanikio ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Waziri Jafo amesema Serikali zote mbili zimeweka mwongozo rasmi wa vikao vya Kamati ya pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano ambavyo hushirikisha wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano.

Amesema vikao hivyo hufanyika katika ngazi tatu za Makatibu Wakuu, Mawaziri na kikao cha Kamati ya Pamoja ambacho Mwenyekiti wake ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya pamoja mwaka 2006 hadi sasa, kasi ya utatuzi wa changamoto imeongezeka ambapo hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 25 zilizoibuliwa.

“Changamoto nyingi ambazo zilikuwa hazijapatiwa ufumbuzi zimejadiliwa na pande zote mbili za Muungano na kupatiwa ufumbuzi ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 pekee hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo kwa kipindi hicho.

“Naomba niwahakikishie watanzania jambo linaenda vizuri,hoja zilizobakia zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi,” amesema Waziri Jafo.

Waziri Jafo amesema katika kipindi chote cha miaka 60 ya Muungano Serikali zetu mbili zimeendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wananchi wa pande zote mbili kufanya kazi kwa uhuru na amani.

“Hali hii imewezesha nchi yetu kuendelea kujitosheleza kwa chakula ambapo hali ya utoshelezi wa chakula imeongezeka kutoka asilimia 90 mwaka 2000 hadi asilimia 124 mwaka 2022.

Vile vile, udugu na uhusiano wa wananchi umeendelea kuimarika ambapo wananchi wa pande zote mbili wameungana katika misingi ya ndoa na kujenga urafiki katika uendeshaji wa shughuli za kibiashara na kijamii.

“Hali hii inawezesha Watanzania kuwa na uhuru wa kuishi katika eneo lolote la upande wa Muungano, kupunguza migawanyiko ya kijamii na kuondoa hisia za ukabila na ubaguzi miongoni mwao,” amesema Waziri Jafo.

Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema kupitia mikutano hiyo ya kuelekea miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Mawaziri ambao wanasimamia wizara zenye taasisi za Muungano wanapata fursa kuzungumza na watanzania kuelezea tulipotoka, tulipo na tunapokwenda.

“Katika kipindi hiki cha shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano, wataalam kutoka taasisi za Muungano watapata fursa ya kupita katika vyombo mbalimbali vya habari kuelezea masuala mbalimbali ya Muungano yanayofanywa na Serikali,” amesema Matinyi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles