32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kenya yagonga mwamba ujenzi bomba la mafuta

Kenyan-President-Uhuru-Kenyatta-Mwandishi Wetu na Mashirika ya Habari

UJENZI wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda, umeziingiza Tanzania na Kenya katika vita kali ya kuwania mradi huo, ambao utaifanya nchi moja wapo kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Siku chache tu baada ya Uganda na Tanzania kuafikiana kuhusu ujenzi wa bomba hilo kutoka Bandari ya Tanga hadi Uganda, Jumatatu wiki hii Rais Uhuru Kenyatta alimwalika Rais wa Uganda, Yoweri Museveni Ikulu mjini Nairobi.

Kampuni zinazozalisha mafuta nchini Uganda, ni Tullow Oil plc kutoka Ireland, China National Offshore Oil Company (CNOOC) kutoka China na  Total ya Ufaransa ambazo pia zilialikwa kuhudhuria mkutano huo.

Hata hivyo, katika mkutano huo Rais Kenyatta alilenga kushawishi  uwezo wa Kenya katika kutatua changamoto, ambazo zilipelekea kile ilichoona kuzidiwa ujanja na Tanzania, ambapo Uganda ilisita kutoa uamuzi wa mwisho.

Badala yake uamuzi wa wapi mradi huo utapitishwa utatolewa wakati wa mkutano mwingine baina ya pande hizo mbili utakaofanyika mjini Kampala wiki mbili zijazo.

Mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Kenya ni miongoni mwa miradi iliyo kwenye mpango mkubwa wa ujenzi wa miradi ya miundombinu ya kanda ya kaskazini.

Bomba hilo la mafuta linakusudia kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Lamu, kupitia eneo lenye mafuta Kenya la Lokichar.

Awali viongozi hao wawili walikutana nchini Uganda Agosti mwaka jana na kuafikiana kuwa ujenzi huo ulipaswa kuharakishwa.

Lakini Tanzania iliipiku Kenya baada ya Museveni kukutana na Rais John Magufuli mapema mwezi huu .

Tanzania inataka ujenzi huo uanze haraka na wiki iliyopita Makamu wa Rais wa kampuni ya Total Afrika Mashariki, Javier Rielo alimhakikishia Rais Magufuli, kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi huo haraka kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.

Bomba hilo la kutoka Tanga hadi Uganda litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi kutoka Ziwa Albert hadi Bandari ya Tanga na litazalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na zisizo za moja kwa moja 20,000.

Wakati Tanzania ikiipiku Kenya, hilo lilielezwa pamoja na mambo mengine ni kutokana na unafuu, uzoefu kama vile bomba la mafuta Tanzania na Zambia (TAZAMA) na usalama zaidi kulinganisha na Lamu, ambako kimeshuhudiwa mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi.

Aidha ilielezwa kuwa wakati  Kampuni ya Tullow na CNOC ambazo pia zimewekeza nchini Kenya zikipendelea mradi huo upitie Kenya, Total ilikuwa ikipendelea Tanzania.

Hata hivyo, ripoti iliyowasilishwa wakati wa mkutano huo wa Nairobi, iliyotumiwa na Uganda kuhalalisha uamuzi wake wa kuuhamisha mradi huo Tanzania ilitokana na mapendekezo ya Tullow na CNOOC.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vilivyoshiriki mazungumzo ya Jumatatu, utafiti wa kampuni hizo mbili uliionya Uganda kutoendelea na mpango wake wa kuitumia njia ya Lamu.

Imefahamika kuwa kampuni hizo mbili zinazofanya kazi na Total, zilionya mpango ya Uganda kuanza kuvuna mafuta ghafi kwa ajili ya usafirishaji mwaka 2018 haitatimia iwapo itaendelea na mkataba na Kenya.

Rais Museveni na ujumbe wake uliwasilisha utafiti huo kwa timu ya Kenya iliyoongozwa na Rais Kenyatta kuonesha kwanini waliamua kuichagua njia ya Tanzania, ambayo ni ndefu zaidi ya ile ya Kenya.

Kwa mujibu wa utafiti huo, Kenya ina historia ndefu ya kuingia katika migogoro ya ulipaji fidia katika maeneo ya miradi, kitu ambacho kitachelewesha bomba kutoka Lokichar hadi Lamu.

“Wasiwasi wa Uganda ni utafiti uliofanywa na  Tullow na CNOOC ulioonesha kuwa fidia ya ardhi inaweza kuwa sababu kuu ya ucheleweshaji wa ujenzi wa bomba hilo,” chanzo cha habari kilichohudhuria mkutano huo kilisema.

Utafiti huo pia uligusia kuwa migogoro inayohusisha upatikanaji wa ardhi kwa miundombinu ya Bandari ya Lamu Port, Sudan Kusini na Ethiopia kupitia  (Lapsset) na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Ripoti ilisema wamiliki ardhi wa Kenya wana kawaida ya kupaisha mno thamani ya ardhi yao iwapo maeneo yao yanataka kuchukuliwa kwa ajili ya uwekezaji  mkubwa.

Katika uwasilishaji wake wa taarifa hiyo, Uganda pia ilionesha matokeo ya utafiti ukionesha eneo lililopangwa bomba hilo la mafuta halina barabara nzuri na hilo linaweza kukwamisha ujenzi huo.

Utafiti pia ulieleza  Bandari ya Lamu bado haijajengwa na hivyo inaweza isikamilike kufikia mwaa 2018 wakati Uganda itakapokuwa tayari kusafirisha mafuta ghafi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles