NAIROBI, KENYA
KENYA itakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kukusanya takwimu za watu wenye jinsia mbili katika sensa yake ya kitaifa inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Katika sensa hiyo inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti itachukua idadi ya raia wake ambao hawajitambulishi kama ni wanaume au wanawake.
Watu wenye jinsia mbili mara kadhaa wanakabiliwa na unyanyasaji na kutengwa na jamii.
Nchini Kenya, inakadiriwa kuna watu zaidi ya 700,000 wenye jinsia mbili kati ya milioni 49.
“Kupata taarifa juu ya watu wenye jinsia mbili kwenye sensa itasaidia watu kufahamu changamoto tunazopitia,” alisema Ryan Muiruri, ambaye ni mwanzilishi wa taasisi ya Intersex Persons Society of Kenya (IPSK).
“Kujumuishwa kwenye sensa ni mafanikio makubwa kwetu,” aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC.
Afrika Kusini ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kuweka wazi muingiliano wa watu wenye jinsia mbili kwenye sheria ya kupinga ubaguzi.
Hatua hiyo ya Kenya imekuja wakati ikiwa imepita takribani miaka kumi tangu mwanamke mmoja nchini humo kuamua kwenda mahakamani mwaka 2009 baada ya daktari kuweka kiulizo sehemu ya kujaza jinsia kwenye cheti cha kuzaliwa mtoto wake.
Mwanamke huyo alitaka vitu vitatu: nyaraka ya utambulisho ya mtoto wake kuwa na uwezo wa kwenda shule, sheria kuzuia upasuaji kwa watoto waliozaliwa na jinsia mbili vinginevyo iwe muhimu kitabibu, na taarifa sahihi ikiwamo msaada wa kisaikolojia kwa wazazi.
Katika hukumu yake mwaka 2014 Mahakama Kuu iliagiza serikali itoe cheti cha kuzaliwa cha mtoto huyo ambaye wakati huo alikuwa na miaka mitano.
Zaidi mahakama ilimwagiza Mwanasheria Mkuu kuunda kikosi kazi ambacho kitaangalia njia za kutoa msaada sahihi kwa watoto wenye jinsia mbili.
Kikosi kazi hicho kilikabidhi mapendekezo yake kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwezi Aprili.
Kilipendekeza upasuaji kutofanywa haraka hadi pale watoto wenyewe watakapojiamulia kuchagua wao wenyewe kubaki na jinsia wanayoitaka na zaidi kupendekeza kufanyika kwa utafiti kubaini idadi yao.
Pia ilipendekezwa alama I itumike kama kitambulisho cha jinsia mbili, na itumike kwenye nyaraka za umma.
Alama hiyo inatumika kuelezea watu ambao wamezaliwa na tofauti za kibaolojia katika viungo vyao vya uzazi na ambao hawaeleweki kama ni wanaume au wanawake.
Kuna tofauti nyingi, zinazohusisha viungo vya uzazi, ovari na mifumo ya homoni.
Umoja wa Mataifa unasema kwa mujibu wa wataalamu, kati ya asilimia 0.05 na 1.7 ya watu wanazaliwa wakiwa na sifa ya jinsia mbili.
KISA CHA RYAN MUIRURI
Mwanzilishi huyo wa taasisi ya IPSK, Ryan anasema yeye binafsi alizaliwa akiwa na jinsia mbili, lakini alipewa utambulisho wa kike na akaitwa jina Ruth.
Ryan anasema wazazi wake hawakumkubali na walikwenda kwa mganga wa kienyeji kwa sababu walitaka kuweka sawasawa kile ambacho watu wengi waliona kama ni mkosi.
“Watu walimcheka mama yangu kwa sababu ya mwonekano wangu, na kuna nyakati nilimwona akilia,” anasema .
Anasema aligundua yupo tofauti alipokuwa na umri wa miaka mitano.
“Siku moja nilikuwa nacheza na watoto wengine, mmoja wao aliniita mimi msichana na mwingine akasema: “nani kakwambia Ruth ni msichana?.”
Anasema walimsogelea na kumvua nguo.
Ryan anasema shuleni kila alipokuwa anakwenda chooni watoto wenzake walikuwa wanamfuata kumwangalia kama anasimama au ana chuchumaa.
“Ilikuwa inaniumiza sana na nilikosa raha, kitu kilichokuwa kinaniuma zaidi ni kuitwa mkosi na wazee wa kijiji walinishutumu kuleta ukame ulioikumba eneo letu.
Anasema alitaka kujiondoa uhai mara tano kwa sababu alijiona mpweke na mtu anayekataliwa.
“Siku moja nilipokuwa benki nachukua fedha, mtu anayehudumia dirishani aliita polisi akinituhumu nimedanganya jinsia. Nilijaribu kuelezea hali yangu lakini hakuna aliyenielewa.
Anasema baadae aliamua kuanzisha taasisi anayoisimamia sasa ili kusaidia watu wenye matatizo kama yake.
Anasema kuwekwa kwenye sensa jambo hilo ni mafanikio makubwa kwao.
