NEW YORK, MAREKANI
BAADA ya kufanya vizuri kwa muda wa miaka 14, kipindi maarufu cha familia ya mwanamitindo, Kim Kardashian, Keeping Up With The Kardashians, kinatarajiwa kufika mwisho mwaka 2021.
Keeping Up With The Kardashians ni miongoni mwa shoo chache za runinga zilizojizolea umaarufu ulimwenguni kote kwa maudhui yake kuonyesha uhalisia wa maisha ya Kim Kardashian na familia yake kwa misimu 20 kupitia televisheni E.
Kupitia mitandao ya kijamii familia ya Kardashian ikiongozwa na Kim mwenyewe walitoa ujumbe wa kusitisha kipindi hicho bila kuweka wazi sababu hivyo kusababisha taharuki kwa mamilioni ya mashabiki wa pindi hilo.
“Kwa mashabiki zetu wapenzi, kwa huzuni tumeamua kuchukua maamuzi magumu kama familia na kuisitisha shoo yetu ya Keeping Up With The Kardashians, baada ya miaka 14 ya misimu 20 na mamia ya vipindi , tunasema asante kwa wote mliotutazama kwenye nyakati za furaha na huzuni ndani ya miaka yote hiyo,” ulisema ujumbe huo.
Itakumbukwa kuwa kipindi cha Keeping Up With The Kardashians, kimefanikiwa kuwapa umaarufu memba wa familia ya Kim kama vile Kylie Jenner aliyeanza kuonekana akiwa mtoto wa miaka 10, Khloe, Kourtney, Kendall na kaka yao Rob Kardashian.