25.9 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kaya 413 zazingirwa na maji Lamadi mkoani Simiyu

Na Samwel Mwanga,Busega

KAYA 413 zilizoko katika Kata ya Lamadi Wilaya ya Busega mkoani Simiyu zimekosa makazi baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na hivyo kusababisha kuongezeka kwa kina cha maji kwenye Ziwa Victoria.

Nyumba hizo ziko mwambao mwa Ziwa Viktoaria katika kitongoji cha Lamadi, Itongo na Makanisani.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed (wa kwanza kushoto)akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Faidha Salum (wa kwanza kulia) wakiwa kwenye mtumbwi wakikagua makazi ya watu yaliyozingirwa na Maji katika Mji wa Lamadi ulioko wilayani humo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed ametembelea eneo hilo leo Mei 6, 2024 akimbatana na Mkuu wa wilaya ya Busega, Faidha Salum, kwa ajili ya kujionea athari hiyo ambapo ameiagiza serikali ya wilaya hiyo kuhakikisha inachukua hatua za haraka ili kuwasaidia wananchi hao.

Amesema amejionea hali halisi ya maafa yaliyowakuta wananchi hao, hivyo ni vizuri serikali ikaelekeza nguvu zake katika kuwasaidia wananchi hao waliopatwa na janga hilo na kuhakikisha kuwa misaada ya kibinadamu inatolewa haraka.

“Kwanza nichukua fursa hii kuwapa pole,nikiwa katika ziara yangu ya kutembelea Tarafa 16 za mkoa wa Simiyu kusikiliza kero za wananchi, jana nikiwa katika mkutano wangu katika tarafa ya Kivukoni nilipata taarifa hizi za maafa haya kupitia kwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Lamadi.

“Leo nimeona nisitishe mkutano wa asubuhi ili niweze kufika hapa Lamadi kujionea hali halisi jinsi maji yalivyozingira nyumba zenu,kweli nimeona wananchi wanateseka hivyo na hii inatokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha ziwa Victoria kuongezeka maji na kuzingira makazi yenu,” amesema Shemsa na kuongeza kuwa:

Maji yakiwa yamezingira baadhi ya nyumba katika mji wa Lamadi wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu.

“Nikuelekeze Mheshimiwa DC kuna mipango ambayo mlikuwa mmeipanga lakini sasa kutokana na adha hii tuliyoiona mimi na wewe baada ya kutembelea eneo hili na Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan hataki wananchi wake wateseke hivyo hatua za haraka zichukuliwe za kuzihamisha hizi kaya na kuwapatia misaada ya kibinadamu na misaada hiyo ifike kwa walengwa haya majanga maji si yapo hapa Simiyu tu bali kwa sasa yako maeneo mengi hii inatokana na kuwa na mvua nyingi sana kwa kipindi hiki,”amesema.

Amewataka viongozi wa CCM katika eneo hilo wahakikishe misaada itakayoletwa kwa wananchi hao inawafikia walengwa kwani wao wanajukumu la kuisimamia serikali.

Kulwa Cheyo Mkazi wa Lamadi wilaya ya Busega akielezea jinsi maji yalivyoathiri nyumba yake na kumlazimu kuhama.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Busega, Faidha Salum, amesema tangu kutokea kwa janga hilo Aprili 26, mwaka huu serikali ya wilaya hiyo imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kuwahamisha wananchi katika eneo hilo na sasa watawaweka wananchi hao katika makambi na kuwahudumia kwa chakula pamoja na vyandarua.

“Tutaendelea kuwaondoa watu wote ambao kaya zao zimezingirwa na maji na kuwaweka katika makambi mbalimbali kwa kutoa chakula na vyandarua na tayari Mganga Mkuu wa wilaya ameanza kugawa vyandarua tangu jana na pia ni kazi ngumu kuyatibu maji haya hata kama tukinunua mapipa ya dawa maana haya maji yanaingia na kutoka katika ziwa Victoria.

“Nikuhakikishie Mwenyekiti maelekezo yako yatatekelezwa na mimi nitoe wito na niwaombe wananchi tuchukue tahadhari kuacha kutumbukia kwenye maji haya ili kuepukana na uchafu ambao umekusanywa na maji haya hivyo tusiwaruhusu watoto wadogo kuchezea maji haya kama mtu hana ulazima wa kupita kwenye maji haya asifanye hivyo maana hatuwezi kuyatibu maji haya yote,” amesema Faidha.

Awali, Diwani wa Kata ya Lamadi, Laurent Bija, kuwa eneo hilo limekuwa likikimbwa na mafuriko ya maji mara kwa matra hasa katika kipindi cha mvua za masika na kusababisha nyumba zilizoko mwambao mwa ziwa Viktoria kuzingirwa na maji na nyingine maji na kusababisha watu kukosa makazi ya kuishi.

Mkuu wa Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Faudhia Salum(aliyeko mbele) akiwaeleza Waandishi wa habari athari ya nyumba zilizozingirwa na Maji katika Mji wa Lamadi.

Amesema ni vizuri kwa sasa serikali kusaidia kusafisha Mto Lamadi ili uweze kumwaga maji yake katika Ziwa Viktoria na siyo kurudi kwenye makazi ya wananchi pia Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) katika wilaya hiyo kusaidia kusanifu barabara za mita ili ziweze kumwaga maji katika ziwa hilo.

Diwani huyo amesema kuwa katika kitongoji cha Lamadi kaya zilizoathirika ni 222, Kitongoji cha Itongo kaya 55 na kitongoji cha Makanisani kaya 136 na baadhi kukosa kabisa makazi ya kuishi.

Kulwa Cheyo mkazi wa Lamadi amesema kuwa ameamua kuhama katika nyumba yake kutokana na maji kujaa ndani na hivyo inatokana na mto Lamadi kujaa uchafu na hivyo kutoruhusu maji kupelekwa katika ziwa Victoria na hivyo kusababisha maji hao kuzingira makazi yao hivyo ni vizuri serikali ikasikia kilio chao.

Diwani wa Kata ya Lamadi, Laurent Bija(aliyeko mbele)iliyoko wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu akiwaeleza Waandishi wa habari athari ya nyumba zilizozingirwa na Maji katika Mji wa Lamadi.

Mmoja wa wananchi walioathirika na mvua hizo, Monica Mhege amesema kuwa maji yamejaa na vyoo vimebomolewa na hivyo uchafu wote vikiwemo vinyesi vinaelea kwenye maji hivyo kuna athari ya kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles