Tunu Nassor, Dar es Salaam
Jumla ya kaya 40,000 za eneo la Salasala, jijini Dar es Salaam zinatarajiwa kupatiwa huduma ya maji safi katika operesheni maalum ya kuwaunganisha inayofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa).
Akizungumza katika eneo hilo Mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa Dawasa, Ritamary Lwabulinda amesema operesheni hiyo imeanza rasmi leo katika eneo hilo na wanatarajia kuunganisha wateja 600 kwa siku.
“Tumeanza na wananchi wa Salasala kwani tayari kuna mtandao wenye maji ya kutosha na baadaye maeneo mengine yatafuata,” amesema Ritamary.
Aidha, ametoa wito kwa wakazi wa Salasala na maeneo jirani kujitokeza katika serikali zao za mitaa kuchukua fomu ili wapatiwe maji.
Kwa upande wake mmoja wa wateja waliopata huduma hiyo jana Vitalis Ephraim alisema wanaishukuru Dawasa kwani awali mlolongo wa kuunganishwa ulikuwa unachukua muda mrefu.
“Tumekuwa tukinunua maji katika magari ambayo walitulazimisha kununua gari zima hivyo tulikuwa tunachanga ndipo tunapata maji,” amesema Ephraimu.