24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kaya 19, 000 nchini kupima VVU, homa ya ini

*Ni kupitia utafiti wa THIS, watakaobainika kuunganishwa na vituo
*Ni vile watakavyochagua kwa ajili ya matibabu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Takribani kaya 19,000 nchi nzima zitapata fursa ya kupima Virusi Vya UKIMWI(VVU) kupitia Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya VVU/UKIMWI(THIS) wa Mwaka 2022-2023.

Pamoja na hilo pia kaya hizo zipatapa fursa kwa wanakaya wake kufanyiwa kipimo cha ugonjwa wa homa ya ini ‘B’ na homa ya ini ‘C’.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene (wa tano kutoka kulia),viongozi mbalimbali wa serikali,wizara na taasisi pamoja na baadhi ya wadau wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuzinduliwa kwa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania.

Hayo yamebainishwa jijini Mwanza Septemba 29, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene, wakati akizindua Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya VVU/UKIMWI wa Mwaka 2022-2023 kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

“Utafiti huu wa mwaka 2022-2023 utatoa fursa kwa kaya takriban 19,000 nchi nzima kupimwa VVU majumbani kwao na kujua hali zao siku hiyo hiyo.

“Kwa wale watakaokutwa na maambukizi ya VVU kwenye utafiti huu wataunganishwa na vituo vya afya watakavyochagua ili kuanza matibabu.

Amesema kuwa huduma za dawa za kufubaza makali ya Virusi Vya Ukimwi (ARV) zinapatikana bure katika vituo vya afya nchini nakwamba matibabu yanasaidia watu wanaoishi na VVU kuishi maisha marefu na yenye afyaikiwamo kupunguza hatari ya kuambukiza watu wengine.

“Nimejulishwa kuwa zaidi ya kupima VVU, washiriki watapata pia fursa ya kufanyiwa kipimo cha ugonjwa wa homa ya ini ‘B’ na homa ya ini ‘C’.

“Hii ni habari njema na itasaidia wale waliokutwa na maambukizi kuweza kupata huduma stahiki za afya,” amesema Simbachawene.

Amesema utafiti huo ambao unatarajiwa kuanza mwaka huu kwa kuratibiwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tazania (TACAIDS), Ofisi ya Takwimu (NBS), Wizara ya Afya na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI uumetanguliwa na ule wa mwaka 2003/2004 na 2016/2017.

“Utafiti uliopita wa mwaka 2016/2017 ulitoa mwanga juu ya namna ambavyo tumeelekeza nguvu zetu kufikia malengo yaliyokusudiwa katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na ugonjwa wa UKIMWI.

“Aidha, utafiti huu ulionesha kiwango cha maambukizi nchini, kushuka na kufikia asilimia 4.7. Pia, utafiti huu ulionyesha idadi ya wanaoishi na virusi vya Ukimwi waliojitambua ilikuwa asilimia 61, waliokuwa katika tiba ilikuwa asilimia 92 na waliofikia ufubazaji VVU walikuwa asilimia 87.

“Matokeo hayo yalikuwa muhimu sana katika kuunda mkakati wa Kitaifa wa mwitikio wa VVU na UKIMWI. Tangu mwaka 2018, nchi imekuwa inatekeleza kwa kasi afua zinazolenga kutambua Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi na kuwaunganisha kwenye tiba za ARV ili pia wafikie ufubazaji wa VVU,” amesema Simbachawene.

Ameongeza kuwa katika kufanikisha hilo, serikali ina jukumu la kuwahakiki wanaoishi na virusi vya Ukimwi kupitia tafiti kama hizo kwenye ngazi ya jamii na taifa kwa ujumla.

“Ni imani yetu kama serikali kuwa, utafiti huu kama ulivyokuwa wa mwaka 2016/2017 utatoa takwimu za VVU ambazo zitatupa uelewa zaidi wa kukabiliana na janga la UKIMWI na pia takwimu ambazo zinapaswa kutuongoza katika kuboresha mipango ya afya na mgawanyo wa rasilimali fedha katika program mbalimbali za VVU.

“Tunafahamu kuwa si kila mtu anayeishi na VVU nchini Tanzania anafahamu hali yake,” amesema Simbachawene.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kufadhili UKIMWI (PEPFAR) ambayo iligharamia utafiti wa mwaka 2016/2017 na itaendelea kugharamia utafiti wa mwaka 2022/2023.

“Huu ni mfano mzuri sana wa ushirikiano uliopo kati ya serikali ya Tanzania kupitia Wizara na Mashirika yake na serikali ya Marekani kupitia Mfuko wa Rais wa Dharura wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) na ICAP iliyo kwenye Chuo Kikuu cha Columbia na wadau wengine wanaoshirikiana kufanikisha utafiti huu,” amesema Simbachawene.

Pia ametoa wito kwa watafiti watakaokwenda kukusanya taarifa, kuhakikisha wanakusanya takwimu bora na sahihi zenye kuleta tija kwa nchi.

Utafiti wa viashiria vya VVU/UKIMWI unalenga kupima asilimia ya watu wanaoishi na VVU nchini, kupima kiwango cha maambukizi mapya, huduma za upimaji, tiba na ufubazaji wa VVU na kiwango cha uelewa kuhusu VVU na UKIMWI miongoni mwa Watanzania.

Aidha, utafiti huo utawezesha kufahamu tabia mbalimbali hatarishi zinazochangia kuenea kwa VVU nchini ambapo viashiria vinavyotoa taarifa hizi vitazingatia umri, jinsia, maeneo na nchi kwa ujumla wake.

Mkurugenzi Mkazi wa ICAP,Haruka Mayaruma, akiwaeleza wadau (hawapo pichani) Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania (THIS 2022-2023) utakavyofanyika.

Awali, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la ICAP, Haruka Mayaruma alisema jitihada hizo za kihistoria zisingefanikiwa bila msaada wa serikali ya Tanzania, PEPFAR, CDC na wadau wengine wa utafiti huo.

“Jitihada endelevu za programu za kinga, tiba na matunzo, zimeweka alama katika kudhibiti janga la VVU duniani kwa kupunguza idadi ya maambukizi mapya ya VVU, athari za ugonjwa wa UKIMWI na kupunguza vifo.

“Utafiti wa THIS ni sehemu ya Mradi wa Tathmini ya Athari za VVU unaosimamiwa na ICAP, ambao ni juhudi za nchi nyingi kukusanya taarifa muhimu zinazohitajika kuongoza mwitikio wa kimataifa dhidi ya janga la VVU.

“Katika kila utafiti, hufanyika ushauri nasaha na upimaji wa VVU katika kaya, unaofanywa na watafiti waliopewa mafunzo na matokeo ya vipimo vya VVU hurudishwa papo kwa papo. Tafiti hizi pia huambatana na maswali kuhusu upatikanaji wa huduma za kinga, tiba na matunzo,” amesema Mayaruma na kuongeza kuwa:

“Kwa ufadhili wa PEPFAR na msaada wa CDC, ICAP ilitekeleza tafiti za awali za PHIA katika nchi 15, kwa malengo ya kupima kiwango cha maambukizi mapya, ushamiri wa VVU kitaifa na kimkoa na kiwango cha wenye VVU vilivyo fubaa,” amesema.

Amesema kwa siku za karibuni, ICAP imekuwa ikitekeleza tafiti za aina hii katika nchi tano ikiwemo Tanzania kupitia THIS 2022-2023.

“Takwimu kutoka kwenye tafiti hizi zitaendelea kuchangia katika uelewa wetu wa programu ya VVU na maendeleo kuelekea malengo mapya ya UNAIDS 95-95-95 tunapoelekea kufikia kizazi huru cha UKIMWI duniani,” amesema.

Balozi wa Marekani nchini, Dk. Donald Right amesema jitihada zinazofanywa na serikali ya Tanzania zitasaidia mapambano dhidi ya UKIMWI ingawa eneo la mambukizi ya mtoto kutoka kwa mama hatufanya vizuri na kusistiza tujifunze kwa matokeo ya nyuma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kifua Kikuu na UKIMWI, Fatuma Towafiq alisema Bunge litaendelea kuishauri na kuisimamia serikali itenge bajeti ya VVU na anaamini utafiti huo ukifanyika kwa weledi na umakini utatoa matokeo sahihi yenye tija na kuwawezesha Watanzania kuwa an afya bora.

Nae, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Seif Shekilaghe, kwa niaba ya Waziri, Ummy Mwalimu, amesema utafiti huo utaonyesha namna ya kutekeleza mapambano ya VVU na utangalia magonjwa mengine ikiwemo homa ya ini ili kufikia malengo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko amesema utafiti wa mwaka 2016/2017 ulionyesha kuwa watu milioni 1.4 walikuwa na maambukizi mapya na mwaka 2021 watu milioni 1.7 walikadiriwa kuwa na maambukizi ya VVU.

“Asilimia 84 wanafahamu hali zao, asilimia 73 wanafikiwa na huduma za afya na asilimia 66 wanatumia dawa za kufubaza virusi (ARV), hivyo takwimu za THIS 2022-2023 zitasaidia kutupima na kuwa na ujuzi wa masuala ya VVU,” amesema Dk. Maboko.

Upande wake, Henry Karugendo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) amesema watashirikiana na Wiara ya Afya kupanga mipango ya afya kwa kutumia takwimu bora za VVU ambazo ni nyenzo muhimu ya kuiwezesha serikali na wadau kuandaa sera, mipango na takwimu rasmi za mapambano ya VVU kuhakikisha watu wanapata huduma za matibabu.

“Takwimu za utafiti wa THIS 2022-2023 zitaonyesha kiwango cha maambukizi mapya ya VVU, kiwango cha watumiaji dawa, kiwango cha homa ya ini B na C na uelewa wa wananchi na kuisaidia serikali kuboresha huduma za afya,VVU na ustawi wa wananchi,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles