26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

KAULI YA JPM NZITO

JPMSITABADILIKA

Kadama Malunde, Shinyanga na Evans Magege- Dar es Salaam

SAA chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kusema kuna magazeti mawili siku zake zinahesabika kutokana na kuandika habari za uchochezi, mjadala mkubwa umeibuka huku wadau wa habari wakitoa maoni yao kutokana na kauli hiyo.

Mjadala huo ulioibuka katika mitandao ya kijamii ulibebwa na maswali kadhaa ikiwamo majina ya magazeti na habari zipi yaliyoandika ambazo ni za uchochezi.

Akizungumza mjini Shinyanga jana alipofungua viwanda vya Jambo Food Products Co. Ltd kinachojihusisha na uzalishaji wa vinywaji na Fresho Investment Co. Ltd kinachojihusisha na uzalishaji wa vifungashio vya mazao, alisema Serikali yake haitasita kuyafuta magazeti mawili ambayo hakutaja majina kwa sababu ya habari hizo zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

“Navipongeza vyombo vyote vya habari kwa kazi nzuri ya kuhabarisha Watanzania isipokuwa magazeti mawili tu ambayo yenyewe kila siku ni kuandika habari za uchochezi tu, bahati nzuri Watanzania wanayajua na wamekuwa wakipuuza habari zao, wao ukizungumza neno wanageuza neno hili, ukizungumza habari hii wao wanageuza hivi.

“Magazeti haya mawili siku zao zinahesabika, huo ndio ujumbe, wasifikiri wanafanya tunawaangalia, Serikali ya kutumbua majipu haiwezi kuacha kutumbua magazeti yanayofanya kazi ya kuchochea, kama wanasikia wasikie, kama hawasikii wasisikie,” alisema.

Magufuli alisema kamwe hatakubali amani ya nchi ivurugwe na vyombo hivyo vya habari ambavyo vimekuwa vikitumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa.

Pia alisema hata mauaji ya Kimbari yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 yalisababishwa na baadhi ya vyombo vya habari baada ya kuandika taarifa za uchochezi.

“Tanzania ni kimbilio la nchi nyingine, kamwe sitakubali nchi ivurugwe na vyombo vya habari vichache ambavyo kazi yao kila kukicha ni kuandika habari za uchochezi, amani ni kitu kikubwa, wanaomwamini Yesu Kristo kuna maneno alisema amani nawaachieni, amani ni kitu muhimu sana.

“Magazeti mengine yanafanya kazi vizuri sana, isipokuwa haya mawili tu, naombeni tufanye kazi uchaguzi umeisha, mimi kama rais wenu nitaendelea kulinda amani ya nchi hii, wanaochochea hawataki tuwe na amani, hawataki tuwe na viwanda,” alisema.

Baada ya Magufuli kuzungumza hivyo, wadau wa tasnia ya habari walizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu jana na kutoa maoni tofauti.

PROFESA BANA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana, aliichambua kauli hiyo kwa kusema Magufuli ashauriwe kuhusu habari ili awe mvumilivu wa baadhi ya mambo.

Alisema kwa mtazamo wake hatarajii magazeti yote yaandike akitakacho Magufuli kwa sababu magazeti mengine yanapima mauzo ya habari na sera zao.

“Nadhani hili suala linahitaji uvumilivu zaidi wa mawazo na fikra tofauti. Ndiyo uhuru wa watu kuandika wakitakacho, kusema wakitakacho ili mradi wasivunje sheria. Kuna magazeti ambayo yapo upande wa Serikali na mengine yanakosoa Serikali, hayo ndiyo mambo ya kuvumiliana.

“Nadhani Rais ashauriwe vizuri kwamba aweze kuwa mvumilivu kwa baadhi ya mambo kwa sababu huo ndio uhuru wa habari kama rais anaona magazeti yanakwenda kinyume sheria zipo,” alisema.

Pia alisema tangu wakati wa uchaguzi uliopita magazeti mengi yamekuwa na misimamo yake kutokana na mazingira yaliyokuwapo.

“Nadhani unajua unakuta misimamo fulani kwa maana ya gazeti fulani, habari fulani ya mtu fulani ikapewa uzito hata kama alivyosema vinastahili kuhojiwa kiuandishi, lakini vikapewa uzito ndiyo habari yenyewe.

“Sasa hiyo rais na Serikali yake hawawezi kuingilia haraka haraka labda kama kuna gazeti limekiuka maadili, sheria za nchi hapo sawa. Lakini hii ya kuchukua misimamo na kuandika wanachofikiri ni sahihi na hilo nadhani ni gumu kwa rais kuliweka wazi isipokuwa ni kuelimishana tu kwamba unaandika kwa faida gani na unaandika kwa faida ya nani na kwanini uchukue msimamo,” alisema.

TEF

Naye Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, alisema Magufuli amekwenda mbali kwa kutoa kauli hiyo kwa sababu yeye kama mkuu wa nchi magazeti mawili si saizi yake.

Alisema rais anatumia nguvu kubwa pasipo uhitaji: “Ukiwa mkuu wa nchi ukaanza kushugulika na gazeti moja au mawili haileti maana kwa sababu rais unaweza kuzungumza kwa ujumla kuhusu vyombo vya habari vya nchi, lakini hatari yake kwa sasa hivi mambo yanaweza kutokea kwa maana ya watu wanaweza kutokea wenye nia mbaya wakashughulikia vyombo vya habari kwa kutumia kigezo cha kwamba kauli ya rais ni amri.

“Lakini pia chombo hicho cha habari kitakachoguswa sasa hivi kitajua kwamba rais ndiye kaelekeza kishughulikiwe,” alisema.

Aliongeza kwamba, nchi inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na sheria za habari zipo na zimewekwa kwa mtu yeyote akiwamo rais mwenyewe.

“Sasa kwa kauli kama hiyo rais ameshavihukumu vyombo vya habari hata kabla ya kusikilizwa, hivyo chochote kitakachotokea ni kwamba sijui itakuwaje, lakini inawezekana rais ameshatoa maelekezo ya kwamba washughulikie hivyo vyombo ambavyo hajavitaja,” alisema.

KIJO BISIMBA

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema kauli ya Rais Magufuli inatishia Watanzania.

Alisema kama kuna magazeti hayafanyi vizuri kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa vyombo husika vifuatiliwe na kuchukua hatua inavyostahili.

Bisimba alisema rais kutoa kauli hiyo yenye fumbo ni kiashiria cha kutisha mawazo ya wananchi kwa sababu taarifa za wananchi ndizo huzaa habari katika magazeti.

“Kwa mfano gazeti ukiachia tahariri, mambo mengine ni sauti ya watu kwamba watu wanasema watu wanaandika, hivyo ukitoa vitisho hivyo maana yake ni kuwatisha wananchi wasiuseme ukweli, hata huo ukweli anaopenda kuutoa rais basi usiwafikie wananchi kwa sababu waandishi watakuwa na hofu ya kuandika.

“Ifahamike vyombo vya habari haviwezi kufanya vitu vyake pasipo kupewa taarifa kutoka kwa wananchi kwa mfano kama hivi unavyoniuliza ni kwa sababu rais kasema, lakini kama asingesema usingeniuliza,”  alisema.

MCT

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mkajanga, alisema hawezi kutoa tamko rasmi kuhusiana na kauli hiyo kwa sababu walikuwa katika kikao cha ndani kuongelea mustakabali wa vyombo vya habari na hata kauli ya Magufuli ni sehemu ya mjadala.

“Hilo tunalijadili kwa hiyo siwezi kulitolea taarifa kwa sasa, lakini ninachotaka tu kusema ni vigumu kutaka mimi kusema kitu cha moja kwa moja kwa sababu magazeti yenyewe hayakutajwa wala habari hizo zinazosemekana ni za uchochezi hazikubainishwa ni habari gani. Lakini kwa ujumla tamko hili lazima litajenga hofu kwa waandishi na kwa wahariri kwa sababu mkuu wa dola akitamka ina asili ya kujenga hofu,” alisema.

PROFESA SHIVJI

Mhadhiri Mstaafu wa UDSM, Profesa Issa Shivji, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu maoni yake juu ya kauli hiyo alijibu kwa kifupi hana cha kusema.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Tusubirie kusoma habari zenye vichwa kama vile NYUMBU NA NYATI WAPAMBANA, NDOVU AAMUA UGOMVI WA SIMBA NA NYATI, BATA WANUNULIWA VIATU, NGURUWE AZAA WATOTO SITA, RAIS AANGALIA MECHI YA SIMBA NA YANGA! Tusitarajie tena habari za kipelezi na zenye kuikosoa serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles