Mohamed Kassara ~Dar es salaam
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’, Zuberi Katwila, ametamba kikosi chake kurejea nchini na kombe la michuano ya Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) itakayofanyika nchini Uganda.
Kikosi hicho kinaendelea na maandalizi yake ya mwisho katika viwanja wa JK Park, Dar es Salaam kwa ajili ya michuano hiyo itakayoanza kutimua vumbi kuanzia Septemba 21 hadi Oktoba 5, mwaka huu, jijini Kampala.
Akizungumza na BINGWA jana, Katwila alisema kikosi chake kimefanya maandalizi makini, lengo likiwa ni kwenda kushindana katika michuano hiyo na kupata mafanikio, si kushiriki tu.
Alisema timu hiyo imezidi kuimarika kutokana na michezo mbalimbali ya kirafiki wanayoendelea kucheza ambayo imewapa utayari vijana wake wa kupambania ubingwa wa michuano hiyo.
“Tunashukuru maandilizi yetu yanaendelea kama yalivyopangwa, kila mchezaji ana morali ya hali ya juu.
“Tulipata michezo ya kirafiki ambayo imetujenga katika ngazi ya kiushindani na tumepania kuhakikisha tunarudi na ubingwa wa michuano hiyo,” alisema.
Alisema kinachompa hamasa zaidi ni namna wachezaji wake wanavyoyapokea mafunzo anayowapa na kuyafanyia kazi kwa umakini mkubwa, huku akitumia michezo hiyo ya kirafiki kurekebisha baadhi ya makosa anayoyaona kwenye kikosi chake hicho.