27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Katika hili la elimu kama Nigeria tena 

Profesa-Joyce-Ndalichako1MAENDELEO ya sekta ya elimu katika miaka ya hivi karibuni yameonesha kuporomoka  hasa pale ilipotokea asilimia 65.5 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012 kupata daraja la sifuri kwa maneno mengine walishindwa au walifeli.

Baadaye ikaundwa tume ambayo ilifanya marekebisho na kuondoa mfumo wa kupanga kwa madaraja kwa kuingia katika mfumo wa wastani wa alama GPA ambao pia ulilalamikiwa na hata hivyo mwaka huu  ulifutwa.

Kwa hali ya sasa ilivyo kinachofanyika ni jitihada za kutaka kurudi kwenye mkondo na kuifufua elimu kutokana na kasoro ambazo zimeshajitokeza. Kitendo cha kubainika  kwamba katika udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu kwamba miongoni mwa waliodahiliwa ni pamoja na wale waliopata daraja la sifuri hilo ni jambo la ajabu.

Mazingira hayo yanaonesha kujaa harufu ya udanganyifu ambayo inachanganyika na harufu ya rushwa kitakachozalishwa hapo ni kundi la watu waliojaa udanganyifu na moja kwa moja kuja kuwa na tabaka la viongozi wadanganyifu.

Inakuwa hivyo kwa sababu wanaofanya au kufanyiwa udanganyifu kamwe ni vigumu kuacha kwani tabia hiyo inakuwa endelevu na inaendelea hadi kutinga katika sehemu za kazi au nyadhifa mbalimbali watakazokuwa nazo. Hivyo jamii inakuwa tayari inaongozwa na viongozi wadanganyifu.

Wapo wengi na kama ikifanyika tathimini bila upendeleo Tanzania inaweza kushangaza dunia jinsi inavyoongozwa na baadhi ya watu ambao kwa hakika leo hii wangestahili kuwa gerezani kutokana na uvunjaji wa sheria waliofanya.

Taswira inayoonekana hapa ni kwamba tunaingizana mkenge katika elimu kwa sababu kinachotafutwa siku hizi na wasomi  ni “bora elimu” na si “elimu bora”. Wasomi wanajivunia vyeti vya kuhitimu vyuo vikuu hata kama hawana maarifa yoyote ya kuboresha maisha ya binadamu.

Wanafunzi wanajitahidi sana kujijengea kitu kinachoitwa kwa Kiingereza CV (Curriculum Vitae) hata kwa njia za udanganyifu. (CV ni mtiririko wa maelezo muhimu binafsi ya mtu ya kihistoria kuhusu msomi kuanzia katika elimu, ajira, masuala ya kijamii, kidini, utamaduni, michezo na kadhalika).

Lakini habari za udanganyifu, kuiba mitihani, kughushi vyeti, rushwa za ngono na pesa katika ajira si ngeni barani Afrika na anayetaka kuwa bingwa wa uhalifu wa aina hiyo basi anaweza kujifunza maarifa hayo Nigeria.

Hivi sasa homa ya wanasiasa chipukizi kusaka shahada duni na vyeti bandia imeingia Tanzania kama ilivyoingia Nigeria miaka 38 iliyopita. Matokeo yake ni kwamba licha ya Nigeria kuwa na vyuo vikuu kamili 73 na shirikishi zaidi ya 20, majenerali wasio na shahada wametawala taifa hilo muda mrefu!

Utafiti uliofanywa Nigeria mwaka 2005/06 na Benki ya Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) ulibainisha kwamba mfumo wa elimu unadorora kwa kasi kutokana na rushwa.

“Nigeria ilikuwa ni taifa lililokuwa linazalisha wahitimu wa vyuo vikuu wenye hadhi ya kimataifa ambao waliweza kushindana na wahitimu wengine duniani. Leo hii, tunazalisha wahitimu wa ovyo wasioweza hata kuumba sentensi rahisi,” anasema Dk. Roy Chikwem, Mnigeria msomi anayeishi Marekani.

Rushwa na udanganyifu katika elimu huko Nigeria vilipaa hadi spika wa zamani wa Bunge la Wawakilishi alipogundulika kuwa amegushi cheti kuonesha kuwa ni mhitimu wa shahada  ya Chuo Kikuu cha Toronto, Canada.

Hatimaye alilazimika kujiuzulu baada ya kashfa hiyo kufumuliwa na vyombo vya habari. Hata hivyo bado spika huyo aliendelea kuwa mwajiriwa wa serikali. “Aibu gani,” anahoji Dk. Chikwem.

Jambo la kusikitisha zaidi, anasema Dk. Chikwem ni ukweli kwamba wazazi wengi huamua kuwanunulia watoto wao nafasi za kujiunga vyuoni badala ya kuwahimiza ili wajitahidi kufaulu mitihani.

“Na kwa wazazi wanaokwepa kujiingiza katika uvunjaji huu wa maadili na sheria, matokeo yake ni kuwa waathirika kwani watoto wao hukosa kuendelea na masomo na kubaki nyumbani hadi wazazi wao wajue jinsi ya kulaghai mfumo uliopo”. Dk. Chikwem anasema hatimaye wazazi hao huishia kutumia ule usemi maarufu wa Kiingereza: “If you can’t beat them, then join them”. Tafsiri yake: “Kama huwezi kuwashinda jiunge nao”.

Kwa mujibu wa Dk. Chikwem hivi sasa mashirika makubwa ya Nigeria kama Shell, Mobil, Chevron, Texaco, Citibank, Accenture, Nestle, Cadbury, Guinness yanapendelea kuajiri wahitimu wa vyuo vya nje ya Nigeria.

Mashirika haya hayana imani tena na mfumo wa elimu pamoja na wahitimu wa Nigeria. Mashirika hayo yanatetea uamuzi huo kwa kusema kwamba hulazimika kutumia gharama kubwa kutoa mafunzo ya ziada kwa wahitimu wa Nigeria ili wafikie kiwango cha utendaji kazi wanachohitaji. Wanasema wahitimu wa nje wana maarifa zaidi, uadilifu na hidhamu katika ajira.

Hivi sasa Tanzania inafuata mkondo wa Nigeria kwani inaweza kuelezwa kuwa ina viongozi na wataalamu wa aina mbalimbali katika sekta zote za uchumi na huduma za kijamii ambao elimu yao inaweza kuelezwa kuwa imepatikana kwa udanganyifu kuanzia katika fursa za kujiunga na shule, vyuo, kughushi vyeti, kuiba mitihani na rushwa za ngono au pesa katika kupata ajira kama si kujuana kwamba unamfahamu nani na si unafahamu nini, wanaotumia lugha ya Kiingereza wanasema ‘Technical know-who, not  technical know-how’.

Baadhi ya mambo yanayofanyika kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kisiasa ndiyo hayo yanayosababisha kuporomoka kwa baadhi ya sekta na sasa inalazimu kutumia nguvu nyingi  katika mapambano ya kutaka kurudi kwenye mstari.

Kwa uhalisia ni kwamba matukio kama hayo yanadidimiza matamanio ya wavuja jasho pamoja na hali ya baadaye ya nchi. Katika uhalisia wa mambo ili ahadi  njema inayosema “Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote” ilishatupwa jalalani  na hakuna mvunajasho ambaye leo hii anaweza kutoka kifua mbele  kwamba anaitekeleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles