Nyemo Malecela -Kagera
KATIBU wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Katoke, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Jaspar Jasson ‘Korot’ (41), ameuawa kwa kunyongwa na kamba shingoni na mwili wake kutelekezwa kando ya barabara kuu ya Muleba- Biharamulo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi, alisema mwili wa marehemu ambaye pia ni mkulima na mkazi wa Bushamba, uligundulika Februari 17 saa 1.30 asubuhi katika eneo la Kakindo, Kitongoji cha Kishenge, Kijiji cha Bisore, Kata ya Muhutwe wilayani Muleba ukiwa kando ya barabara hiyo.
Baada ya uchunguzi wa eneo la tukio na mwili wa marehemu uliofanywa na daktari aliyefuatana na polisi, ilibainika sababu ya kifo ni kukosa hewa baada ya kukabwa shingo.
Pili mwili wa marehemu ulikutwa na dalili za kunyongwa, umekutwa na alama ya michubuko ya kamba shingoni, lakini pia ukiwa na haja kubwa na ndogo katika nguo alizokuwa amevaa.
Kamanda Malimi alisema hata mazingira ya mwili ulipokutwa kulikuwa hakuna mti na ulikuwa kando mwa barabara na hakuna alama zinazoonyesha tukio lililosababisha kifo chake kama vile vurugu katika majani, bali kilichoonekana ni tukio hilo lilifanyika eneo jingine ambalo halijulikani na mwili kupelekwa kando mwa barabara kwa lengo la kupoteza ushahidi.
“Mpaka sasa hakuna ushahidi wa kuonyesha kama marehemu kabla ya kufikwa na umauti alikuwa na ugomvi na mtu yeyote.
“Hata hivyo imeelezwa kwamba hadi anafariki marehemu alikuwa ametengana na mke wake wa ndoa kwa kipindi kisichopungua miaka minne na akamtelekeza na watoto kisha akahamia na kuishi na mwanamke mwingine, Beatrice Zacharia – ‘hawara’ mwenye mji na watoto wake katika Kitongoji cha Mushonde, Kijiji cha Bisore, Wilaya ya Muleba.
“Kabla ya umauti kumfika Feburuari 16 mwaka huu, alionekana katika Kijiji cha Bisore alikokuwa amehamia akiwa peke yake saa 11 jioni,” alisema Kamanda Malimi.
Alisema juhudi za upelelezi zinaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho na nani aliyehusika kuuweka mwili huo kando mwa barabara na hadi sasa hakuna ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi.