29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Kashfa ya Escrow, Jk kuzima au kuchochea moto

 

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete

FREDY AZZAH na SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
IKIWA leo ni siku ya 23, tangu Novemba 29,mwaka huu Bunge lilipopitisha maazimio nane juu ya kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 306 katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Rais Jakaya Kikwete anatazamiwa kuuzima ama kuchochea moto wa sakata hilo atakapozungumza na wazee wa Jiji la Dar es Saalam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais Kikwete leo atazungumza na wazee hao katika Ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza.
Itakumbukwa katika mkutano wa Bunge uliopita, wabunge wengi bila kujali itikadi za vyama vyao walitaka viongozi wote waliohusika katika kashfa hiyo wachukuliwe hatua ikiwa ni pamoja na kuwajibishwa.
Mbali na wabunge hao, viongozi wa juu wa Chama Cha (CCM) wakiwa katika mikutano ya hadhara sehemu mbalimbali nchini, walinukuliwa na vyombo vya habari wakisema kashfa hiyo isihusishwe na chama hicho na kuagiza kuwa wale wote waliohusika wachukuliwe hatua.
“Msimamo wa CCM kila aliyehusika na Escrow abebe msalaba wake bila kujali cheo wala chama atokacho, kujiuzulu pekee haitoshi kwani ni sawa na likizo tu ya kwenda kula vizuri pesa walizoiba,” alisema Nape akiwa katika moja ya ziara katika mikoa ya kusini.
Mbali na Nape, viongozi wengine wa chama hicho akiwamo Makamu Mwenyekiti-Bara, Philip Mangula walifika Dodoma kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuwashinikiza wale wote waliohusika na kashfa hiyo kuwajibika.
Hata hivyo, juhudi zao hazikuzaa matunda, mpaka hivi karibuni Ikulu ilipotoa taarifa ya kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Wakati umma ukisubiri hatima ya viongozi wengine ambao Bunge liliazimia wawajibishwe na mamlaka zao za uteuzi, hivi karibuni Waziri wa Aridhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliibuka na kusema hawezi kujiuzulu kwani akifanya hivyo hata Rais Kikwete.
Profesa Tibaijuka alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa yeye na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ni tegemeo la Rais Kikwete.
Kauli ya Profesa Tibaijuka, inakumbusha kauli hiyo iliyotolewa na Spika, Anne Makinda kuwa, mara zote kazi ya Bunge imekuwa rahisi pale watu wanapotakiwa kuwajibika kwa sababu huwa wanakubali kuwajibika.
Makinda, alitoa kauli hiyo baada ya baadhi ya wabunge kudai wapo mawaziri waliowajibika ili hali hawakufanya kosa moja kwa moja, lakini hawa wa sasa licha ya kuonekana dhahiri kufanya makosa, kiti cha Spika kinaonekana kuwabeba.
Mkutano wa Bunge na taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa tangu vyombo vya habari kuibua kashfa hiyo mwanzoni mwa mwaka huu, ni kitendawili amacho Rais Kikwete anatakiwa kukitegua leo.
Kuteguliwa kwa kitendawili hicho kwa kutekelezwa kwa maazimio ya Bunge na wahusika kuchukuliwa hatua, kutawapa Watanzania ahuweni kwani kutafungua madirisha ya fedha za maendeleo ambazo zimezuiliwa na wahisani.
Kutotekelezwa kwa maazimio hayo, kutasababisha Serikali na hasa Waziri Mkuu, Mizengo Pindaa ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni kupata wakati mgumu katika mkutano mwingine unaotarajiwa kuanza Januari 27, mwakani.
Hivi karibuni, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema baada ya muhimili huo kumaliza kazi yake, unasubiri ripoti ya Serikali kwenye Bunge lijalo juu ya namna ambavyo maadhimio yake yamefanyiwa kazi.
Alisema kwa viongozi ambao walitakiwa kuchuliwa hatua na Bunge, chombo hicho kitafanya hivyo kabla ya mkutano ujao.
Kwa sasa wananchi wengi wana uelewa wa uchotwaji wa fedha hizo na wengi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, waliamua kuchagua viongozi wa upinzani kutokana na wizi huo wa fedha.
Ni wazi kuwa msimamo wa Rais Kikwete leo, utatoa mwanga na hatima ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.
Chadema
Chadema cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai Rais Jakaya Kikwete atatumia hotuba yake leo kutetea uchotwaji wa fedha hizo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho, Arcado Ntagazwa alisema chama hicho kimepata taarifa kutoka vyanzo vyake ndani ya Ikulu.
“Tunazo taarifa kuwa Rais Kikwete amejipanga kuuhadaa umma kwa kisingizio cha uchunguzi wa Ikulu ili kuwalinda Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake Eliakim Maswi ambao ni miongoni mwa watuhumiwa wanaotakiwa kufukuzwa kazi, kushtakiwa na kufilisiwa,” alisema.
Ntagazwa ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, alitoa wito kwa Rais Kikwete kutoa hotuba itakayowawajibisha wote walioshiriki katika kutekeleza wizi huo.
Ntagazwa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, mbali na watu waliotajwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wapo wengine ambao walihusika lakini hawakutajwa na kamati hiyo.
“Watu wengine wanaotakiwa kuwajibishwa ni Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Silviacius Likwelile, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felicesmi Mramba,” alisema.
“Gavana Ndulu hawezi kukwepa uwajibikaji kwenye jambo hili kwa kuwa alilifahamu na kulilidhia na ni imani yangu, Rais Kikwete ataueleza umma wa Watanzania hatua atakazowachukulia na kuachana na visingizio vya miamala iliyochukuliwa katika Benki ya Mkombozi,” alisema.
Alisema Mkuya kwa upande wake, wakati fedha zinachotwa kati ya Septemba na Desemba, mwaka jana alikuwa akikaimu nafasi ya waziri wa fedha.

Maazimio ya Bunge
1 Harbinder Singh Seth na wengine
Bunge linaazimia kwamba, TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Vyombo vingine husika vya Ulinzi na Usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, dhidi ya watu wote waliotajwa na Taarifa Maalumu ya Kamati, kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na Miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusika katika vitendo vya jinai.
2 Mitambo ya IPTL

Bunge linaazimia kwamba, Serikali iangalie uwezekano wa kuichukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa mujibu wa sheria za nchi.

3 Mapitio ya Mikataba ya Umeme ( Azimio la Kamati teule ya Richmond)

Bunge linaazimia kwamba, Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti la Mwaka 2015/2016, Serikali iwasilishe Taarifa ya Utekelezaji wa Mapitio ya Mikataba ya Umeme;

4 Kitengo cha Rushwa kubwa
Bunge linaazimia kwamba; Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda TAKUKURU, kwa lengo la kuanzisha Taasisi mahususi itakayoshughulikia kupambana na kudhibidi vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

5 Majaji

Bunge linaazimia kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aunde tume ya kijaji ya uchunguzi, kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujuluzi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania. (Makofi)

6 Benki ya Stanbic na Benki Nyingine

Bunge linaazimia kwamba, mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow kuwa ni Taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (Institutions of Money Laundering Concern).
7 Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu na Bodi ya TANESCO

Bunge linaazimia kwamba, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri Mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.

8. William Ngeleja, Victor Mwambalaswa na Andrew Chenge

Bunge linaazimia kwamba, Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya mkutano wa kumi na nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao katika kamati husika za Bunge.
Katika mkutano huo na wazee wa Dar es Salaam Rais Kikwete anatarajiwa kuweka wazi juu ya sakata la utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge likiwemo la kuwawajibisha viongozi wanaotajwa kuhusika moja kwa moja katika kashfa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles