OTHMAN MIRAJI, UJERUMANI
USHINDI wa Felix Tshisekedi kama Rais Mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambao umetangazwa karibuni na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo ni nafasi ya kihistoria kwa Bara zima la Afrika kuweza kupiga hatua mbele.
Ikiwa kweli Tshisekedi, kiongozi wa mojawapo ya vuguvugu muhimu za kiraia katika Kongo, atakuwa rais wa nchi, basi huenda itawezekana kwa nchi hiyo kujitoa kwenye mkwamo unaojikuta kila wakati ndani ya mduara wa matumizi ya nguvu na vita vya wenyewe kwa wenyewe Kongo, yenye wakaazi milioni 90 na iliyoko kijiografia katika moyo wa Afrika, imekuwa katika michafuko tangu ilipopata uhuru kutoka ukoloni wa Kibelgiji mwaka 1960.
Uchaguzi wa Disemba, 2018 haujawa tu wa amani katika historia ya sasa ya nchi hiyo, lakini Tshisekedi anaweza kuwa raia wa mwanzo kuingia katika uongozi kwa njia ya amani tangu pale zilipotokea vurugu mara tu baada ya Kongo kupata uhuru. Tukio hili la sasa linaachana na ule utamaduni wa kisiasa uliojengeka hadi sasa kwamba madaraka yanapatikana tu kwa mtutu wa bunduki.
Bahati mbaya uchaguzi wa Tshisekedi una dosari ambayo yeye mwenyewe hawezi kuiondoa. Watu wengi wanashuku kwamba kumekuwapo njama au uchakachuaji katika kuchaguliwa kwake. Kwa Wakongomani wengi na pia kuna hoja zenye nguvu, ni kwamba mgombea mwingine wa upinzani, Martin Fayulu, ndiye mshindi wa kweli. Lakini mwanasiasa Fayulu hakubaliki kwa majenerali wa jeshi wenye nguvu na wanaomzunguka Rais Joseph Kabila anayeacha sasa madaraka. Majenerali hao wanamuangalia Fayulu kuwa ni mgombea wa wapinzani walioko uhamishoni na ambao huenda baadaye wakawa wapinzani wao wa kijeshi. Kwa hivyo wanaona hamna budi Fayulu azuiliwe kuingia madarakani.
Hata hivyo, utawala wa Kabila sasa umefanya uchakachuaji ulio wa bayana kuifaidia kambi yake na kuzuia kitisho cha kutokea mapambano ya kijeshi. Udanganyifu huo haujawa tu wa waziwazi ili kumzuia Fayulu, lakini pia kuficha kuonekana kabisa hadharani kwamba wananchi wameukataa utawala wa Kabila.
Kwa vyovyote vile, Tshisekedi ataingia madarakani akiwa na tatizo kubwa juu ya uhalali wa utawala wake na swali linaloulizwa ni gharama gani atalipia kwa kuwapo yeye madarakani? Swali lingine ni uhakika na dhamana gani itambidi yeye Tshisekedi atoe ili majenerali wa Kabila angalu wamuachie atawale kwa utulivu?
Tujiulize, lakini Je, haya si mafanikio makubwa kwamba kambi ya utawala uliopita wa Kabila imeshindwa katika uchaguzi huu? Viongozi wote wawili wa upinzani, Tshisekedi na Fayullu, ukizichanganyisha pamoja kura zao (asilimia 38.57 na asilimia 34.83), kwa mujibu wa matokeo rasmi, wamepata zaidi ya asilimia 73 ya kura. Hivyo, yaonesha wote wawili wamepata imani kubwa ya wananchi wa Kongo ambao wanataka mabadiliko.
Pindi rais mpya ataweza kuusuka pamoja upinzani wote na kuwa kitu kimoja na kusonga mbele na mageuzi, basi atastahiki kusaidiwa kimataifa ili aijenge Kongo mpya na si tena aanguke kama muhanga wa kuendelea matumizi ya nguvu katika nchi hiyo, kama yale yaliyoshuhudiwa katika tawala zilizopita. Pindi rais mpya atakapoingia madarakani mambo yataendelea kama yalivyokuwa kabla, basi Kongo itazidi kusambaratika na tusisahau kwamba mustakbali wa Afrika unaitegemea sana Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
La mwisho na hili ni muhimu, Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo ina siku 14 kutoka sasa kuyathibitisha matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Mikoa mitatu ya nchi hiyo, ikiwamo Beni na Butembo (Mashariki ya nchi), Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikataza kufanywa uchaguzi Disemba 30, 2018. Sababu iliyotolewa ni ghasia katika mikoa hiyo na kuenea ugonjwa wa Ebola. Uchaguzi katika mikoa hiyo badala yake umepangwa kufanywa Machi mwaka huu.
Idadi ya wapiga kura katika mikoa hiyo ni zaidi ya watu milioni moja, zaidi kuliko tafauti ya kura alizopata Tshisekedi dhidi ya Fayulu. Vipi yatakavyokuwa mambo pindi Fayulu atamshinda Tshisekedi kwa kura nyingi sana, tuseme kura laki nane, katika mikoa hiyo wakati Tshisekedi atakuwa ameshatangazwa mshindi na Mahakama ya Katiba hapo kabla? Hiyo ni mikoa inayodhibitiwa na watu wanaompiga Kabila. Hilo ni swali gumu kulijibu. Fayulu Ameshatangaza kwamba anakusudia kuyakataa kisheria matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi. Kishindo hicho!
Yaonesha bado kashehe ya Uchaguzi wa Kongo haijamalizika bado.