26.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kasekenya azindua Baraza la Wafanyakazi CRB, atoa maagizo

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amezindua Baraza la Wafanyakazi la Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), huku akilitaka kuleta uwazi na kuondoa manung’uniko mahali pa kazi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi leo Oktoba 22,2024 jijini Dar es Salaam, Mhandisi Kasekenya amesema mahali popote ambapo Baraza la Wafanyakazi likifanya kazi kwa weledi migogoro baina ya Menejimenti na wafanyakazi haitatokea kutokana na kupunguza kero na changamoto baina yao.

“Baraza lilete uwazi, liondoe manung’uniko ili liwe chachu ya kuleta tija na ufanisi mahali pakazi,” amesema Kasekenya.

Aidha amelitaka Baraza hilo kushirikiana na Menejimenti kuhakikisha mipango na mikakti ya CRB inafikiwa hususani katika mkakati mpya wa kuwawezesha makandarsi wazawa kupata fursa nyingi katika miradi ya ujenzi inayoendelea nchini.

Alisisitiza Baraza kuwa chombo cha ushauri, usuluhishi na utetezi wa haki za watumishi ili kutetea maslahi na hali bora za wafanyakazi.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mrisho Mrisho amehimiza Baraza hilo kuweka misingi bora itakayowezesha kupata wajumbe bora, wachapakazi na waadilifu na kusisitiza Baraza hilo kuwa fursa kuboresha utendaji kazi wa CRB na kutaka Menejimenti kutoa ushirikiano kwa Baraza ili kufikia malengo.

Aidha, Mrisho ameitaka Menejimenti ya CRB kuwapatia wajumbe wa Baraza hilo mafunzo ya kutosha ili kuwawekea misingi katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Naye, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Mhandisi, Rhoben Nkori ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi hiyo amesema uanzishwaji Baraza hilo ni mwelekeo chanya kwani katika kipindi kifupi cha uanzishwaji wake wajumbe 39 wamejiunga kama wajumbe wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE).

“Tunashukuru TUGHE Mkoa wa Dodoma kwa ushauri na utaalamu wa kusaidia kuanzishwa kwa Baraza hili, tunaomba ushirikiano zaidi kuendelea kuwezesha Baraza hili ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa,” amesema Mhandisi Nkori.

Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la CRB, Mhandisi, Ezekiel Kitalu, ameishukuru Menejeimenti ya CRB kwa ushirikiano unaompa na kuahidi watajitahidi kuhakikisha wafanyakazi wengi wanajiunga na TUGHE na kuwezesha mahitaji ya watumishi yanafika kwa Menejimenti kwa wakati.

Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi CRB ni maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliyoyatoa hivi karibuni kuzitaka Taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo kuhakikisha zinakuwa na mabaraza ya Wafanyakazi ili kuleta tija na ufanisi mahala pakazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles