25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

KARIA, WAMBURA KUONGOZA TFF

Na ASHA MUHAJI -DODOMA

WALLACE Karia ndiye bosi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho hilo, huku Michael Richard Wambura akiutwaa umakamu wa Rais.

Karia ameshinda wadhifa huo katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo, uliofanyika jana kwenye Hoteli ya St Gasper, mkoani hapa, kwa kupata kura 95, hivyo kuwashinda kwa mbali wapinzani wake watano waliokuwa wakiwania nafasi hiyo na kuambulia kura kiduchu.

Waliozidiwa kete na Karia ni Ally Mayay Tembele ambaye alipata kura 9, Shija Richard (kura 9), Imani Madega (kura 8), Frederick Mwakalebela (kura 3) na Emmanuel Kimbe (kura 1).

Kwenye nafasi ya urais, Wambura ameibuka mshindi kwa kura 85, akiwashinda Mwenyekiti wa FA Dodoma Mlamu Ng’hambi (kura 25), mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars Mtemi Ramadhani (kura 3) na mdau Robert Selasela aliyeambulia kura 2.

Kwenye nafasi za Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, wamechaguliwa wajumbe 13 kuwakilisha kanda 13 zilizogawanywa kwa mujibu wa Katiba ya TFF, ambapo kanda ya 1 yenye mikoa ya Kagera na Geita mshindi ni Salum Chama, aliyepata kura 92.

Kanda ya 2 yenye mikoa ya Mara na Mwanza mshindi ni Vedastus Rufano, aliyeibuka mshindi kwa kura 67, huku kanda ya 3 inayojumuisha mikoa ya Shinyanga na Simiyu, ikiwakilishwa na Mbasha Matutu (kura 67).

Kanda ya 4 yenye mikoa ya Arusha na Manyara mshindi ni mwanamama pekee katika uchaguzi huo, Sara Chao, aliyejikusanyia kura 57.

Kanda ya 5 (Kigoma na Tabora) itawakilishwa na Issa Mrisho (kura  80), wakati Kenedy Pesambili yeye akiwa mjumbe wa Kanda ya 6, yenye mikoa ya Katavi na Rukwa, baada ya kupata kura 72.

Kwenye Kanda ya 7 yenye mikoa ya Mbeya na Iringa, Elius Mwanjala aliibuka mshindi kwa kupata kura 61, James Mhagama akipata kura 63 kuiwakilisha Kanda ya nane yenye mikoa ya Njombe na Ruvuma, huku

Kanda ya 9 yenye mikoa ya Lindi  na Mtwara ikiwakilishwa na Dustan Ditopile, aliyepata kura 74.

Kanda ya 10, Singida na Dodoma aliyeibuka mshindi ni Mohammed Adei, aliyepata kura 38.

Kanda ya 11 Pwani na Morogoro, inawakilishwa na Francis Kumba (kura 72), wakati Kanda ya 12 Kilimanjaro na Tanga mshindi ni Khalid Mohammed (kura 38) na Kanda ya Dar es Salaam ambayo ilikuwa ikitolewa macho zaidi, mshindi akiwa ni Lameck Nyambaya, ambaye amepata kura 41.

Mara baada ya uchaguzi huo, Kamati ya Utendaji yote, kuanzia Rais, Makamu na Wajumbe waliapishwa na Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini, Wakili Ibrahim Mkwawa. Waliapishwa kuitii katiba ya TFF na sheria za BMT.

Aidha, viongozi wa Shrikisho la soka Ulimwenguni (Fifa) na wale wa Afrika (Caf) wamedai kuridhishwa na zoezi zima la uchaguzi lilivyoendeshwa.

Taasisi hizo zimeamua kushuhudia uchaguzi kufuatia figisu za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikiikabili TFF. Viongozi hao ni Veron Masengo-Omva  (Fifa) akiwa ndiye mkuu wa msafara huo, pamoja na Solomon Madege pia Fifa. Suleiman Waberi na Leodeger Tenga, wao waliiwakilisha CAF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles