29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Karani Chama cha Ushirika adhaminiwa na marehemu

Nyemo Malecela -Kagera

MKUU wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Deodatus Kinawilo ameshangazwa na karani wa Chama cha Ushirika cha Kaibanja, Sweetbeat Mtembei kudhaminiwa na wadhamini waliofariki dunia.

Sweetbeat aligundulika kuwa alidhaminiwa na wadhamini waliokwishafariki baada ya kutokea ubadhirifu wa kahawa katika chama hicho cha ushirika kitendo kilichosababisha kutokomea kusikojulikana.

Kinawilo alisema kitendo cha karani huyo kudhaminiwa na watu ambao wamefariki kinaonyesha jinsi gani Ofisa Ushirika Wilaya ya Bukoba, Mutawajibu Lwiza hayuko makini na kazi yake.

“Mutawajibu alitakiwa kuhakikisha karani huyo anakuwa na wadhamini walio hai kwani wote waliomdhamini walishafariki.

“Yaani wafu wamdhamini vipi karani? Kitendo cha wafu kumdhamini karani ina maana kulikuwa hakuna umakini kwa ofisa Ushirika,” alisema Kinawilo.

Kufuatia utata uliojitokeza kwa wadhamini wa karani wa chama hicho, Kinawilo alimwagiza Mkurugenzi amwondoe Ofisa Ushirika wa Wilaya hiyo pia akamwagiza OCD kuwakamata mwenyekiti wa chama hicho pamoja na wajumbe wote wa bodi ya chama hicho, ikiwa ni pamoja na kumtafuta karani ambaye haijulikani alipo.

Karani huyo pamoja na wajumbe wengine wa bodi ya chama hicho wanadaiwa kufanya ubadhirifu wa kahawa kilo 25,632 zenye thamani ya Sh milioni 28,195,200 ambayo haionekani ghalani.

Aidha ukaguzi umebaini kuwa karani huyo pamoja na wenzake wanakabiliwa na tuhuma za upungufu wa kahawa kilo 1,595 yenye thamani ya Sh milioni 1,754,500 iliyosafirishwa kutoka chama hicho kwenda Kiwanda cha Bukop kilichopo Bukoba Manispaa.

Pia Kinawilo alimwagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Bukoba kuhakikisha unafanyika uchaguzi wa haraka ili kumpata ofisa ushirika wa wilaya mwingine na yule aliyekuwepo aondolewe na kupangiwa kazi nyingine.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa ndani wa Chama cha Ushirika cha KCU, Robart Kateka, alisema ukaguzi umebaini kutokuwepo kwa umakini kwa wajumbe wa bodi ya chama katika zoezi la kupokea kahawa kutoka kwa wananchi.

Kwamba bodi ya chama na karani walikusanya kahawa bila kuzingatia ubora wa kahawa ambayo ilikuwa ni mbichi na kusababisha kukataliwa kiwandani Bukop Ltd.

Alisema sehemu ya kahawa hiyo ilianikwa baada ya kufika Bukoba mjini na nyingine kuanikwa katika chama cha ushirika.

“Imebainika kuwa kiwango kikubwa cha kahawa kisichokuwa na ubora kilipokewa kutoka kwa wafanyabiashara na walanguzi.

“Hadi sasa jumla ya wakulima 46 bado wanakidai chama hiki cha ushirika jumla ya Sh 2,441,300 sawa na kilo 22,183 kahawa ambayo haipo ghalani na haijulikani wapi ilipo,” alieleza.

Kateka alisema bodi ya chama hicho ilikuwa inaundwa na wajumbe watano ambao ni Hamida Maulid (mwenyekiti), Lukia Lucas (Makamu Mwenyekiti), na wajumbe Zena Muhamed, Jason Mwegarura na Abdul Ibrahim.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles